Friday, November 15

UWT YAWAPA ONYO WANAWAKE

NA MARYAM SALUM, PEMBA.

MWENYEKITI wa UWT Taifa Mary Pius Chatanda amewataka wanawake wenzake kuacha tabia ya kuwanyanyasa  na kuwatelekeza watoto kwani hilo sio jambo la busara kwa jamii na hata mbele ya Mungu.

Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti huyo katika Kiwanja chakufurahishia watoto kilichopo Tibirinzi Chake Chake kwenye wiki ya siku ya mwanamke Duniani ambapo huadhimishwa kila ifikapo machi 8 ya mwaka.

Alisema kuwa suala la malezi kwa  watoto sio la mzazi mmoja ni jukumu la kila mmoja ndani ya jamii ili kuondosha changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza.

Alieleza kuwa sio jambo la busara kwa mzazi kutupa mtoto ama kutelekeza mtoto kwa sababu tu yakukosa huduma ama mahitaji kutoka kwa mwenza wake.

“Tusitupe watoto kwani hatujui hapo mbeleni mtoto huyo unaemtupa atakuja kuwa nani katika jamii, hivyo tulee watoto wetu kwa kila hali ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili wa Kijinsia ambao umeshamiri ndani ya jamii zetu,” alisema Mwenyekiti huyo.

Alifahamisha kuwa siku ya wanawake Duniani yalianza kutimiza miaka  112 tangu kuasisiwa kwake, ambapo kwa Tanzania ilianza mwaka 1911, kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta viwandani nchini Marekani ambapo waliandamana na kupinga mazingira duni ya kazi kama vile ukosefu wa huduma za kijamiina vitendo vya unyanyasaji.

Alisema kuwa suala la Ukatili wa Kijinsia ni suala la kupambana nalo kwa kushirikiana pamoja ili kuhakikisha halipati nafasi.

“Wapo akinamama wengi hupigwa na waume zao, na pia wapo watoto wadogo hutelekezwa na wazazi wao ama familia zao kutokana na sababu mbali mbali ambazo hazina msingi,” alieleza mwenyekiti huyo

Alifahamisha kuwa kufuatia hali hiyo mnamo mwaka 1977 Umoja wa mataifa ulithibitisha azimio lililozitaka nchi wanachama kuadhimisha siku ya wanawake ifikapo machi 8 ya kila mwaka nakuenzi mchango wa wa wanawake katika ujenzi wa Taifa husika.

“Hapa Tanzania siku ya mwanamke Duniani ilianza kudhimishwa mwaka 1997, hivyo tunaendelea kudhimisha kila mwaka katika Mikoa na kitaifa ambapo sherehe hizi huadhimishwa kila baada ya miaka mitano, alifahamisha.

Alisema  kuwa sherehe hizi ni  tathmini niutekelezaji wa sera mpango wa mikakati na miongozo mbali mbali  itakayo faa iliyoandaliwa na kwa ajili yakuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, mfano ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 sura ya 9 imeeleza  bayana kwamba kuanzishwa kwa madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya kulelea watoto.

“Hivyo kila mmoja wetu anaona wazi jinsi wanavyofanya kazi katika madawati hayo, hivyo niwaombe wananchi kutoa mashirikiano katika kupiga vita ukatili wa Kijinsia”, alieleza.

Alifahamisha kuwa kumekuwa na shida katika suala zima la ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto ni jambo  ambalo lipo miongoni mwa familia, wanawake wapo wengine wanapigwa mpaka unashangaa kutokana na kipigo kama vile anapigwa nguruwe.

“Lakini wapo wengine pia wanawanyanyasa watoto wao, kwakuwaacha watoto na kujilea mwenyewe jambo ambalo linapelekea mtoto huyo kushinda mitaani, barabarani, kitu kinachopelekea  sura mbaya nchini,” alifahamisha Mwenyekiti Mery.

Aidha aliwataka  wanawake na walezi kwa ujumla kurudi kwa Mungu wao kwa kuswali na kuomba dua, ili kuweza kulea watoto wao kwa misingi mizuri na yenye maadili kwa maendeleo.

“Tanzaznia tumeingiliwa na matatizo makubwa ya ubakaji, ya ulawiti, tumeingiliwa na mataifa kutoka nje hadi wengine wameanzisha skuli kwa masuala hayo hata Wizara ya Elimu imegundua hilo, hivyo tuswali ili tuondokane na mambo maovu,” alisema.

Wakati akimkaribisha Mwenyekiti wa UWT Taifa katika hafla hiyo Makamu Mwenyekiti wa  UWT Zainab Khamis Shomari(MNEC), alisema kuwa lengo la kuchaguliwa kuwa viongozi kwenye Jumuia ni kuimarisha Jumuia, Kiuchumi Kisiasa na Kimaendeleo.

“Hivyo nafasi mliotupatia tutaiheshimu tutailinda kwa kadri ya uwezo wetu hivyo tunaomba mashirikiano yenu ili tuweze kufikia malengo, na kutekeleza majuku yale ambayo katiba ama kanuni ya UWT inavyowaongoza,” alisema.

Alieleza kuwa kutokana na dhamana walizopatiwa ndani ya Jumuia watafanya kazi bega kwa bega  na  viongozi wenzao pamoja na wananchama katika kuhakikisha wanaiweka ccm madarakani pale ifikapo 2025.

“Sisi akinamama tupo wengi kwa mujibu idadi ya Sensa ya mwaka huu na ndio wapiga kura wakubwa na wengi, hivyo ifikapo 2025 tuone kwamba asilimia hiyo imekwenda kwa mwanamke mwenzetu katika kumchagua kuwa Rais,” alieleza.

Hivyo aliwataka akinamama wa Jimbo la Chake Chake kuhakikisha wanachangamkia fursa mbali mbali zinazotolewa na Serikali katika kujikita zaidi kwenye masuala mbali mbali ya kimaendeleo kwa maslahi ya taifa.

Kwa upande wake Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Anna Athanas Paul alieleza mwaka huu wameweza kupokea jumla ya kesi 1360  za ukatili wa Kijinsia.

“Hivyo  kutokana na idadi hii kwa mwaka huu tunahitaji mashirikiano kutoka kwa jamii ili kupinga vitendo hivyo,” alifahamisha Naibu Waziri huyo.

Nae Katibu Mkuu wa UWT Philis M.Nyimbi(MNEC), alifahamisha kuwa mkusanyiko wa wanawake katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani ni kuthamini mchango uliotolewa na wanawake wenzao katika kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia duniani.

Mapema Naibu Katibu Mkuu Zanzibar  Tunu Juma Kombo alisema kuwa lengo la siku ya wanawake duniani ni kufikia kwenye malengo yakimaendeleo.

Hata hivyo aliwataka  wanawake wenzake siku hiyo sikusherehekea tu pekee, pia ipo haja kutoa mashirikiano yakuhakikisha wanapambana kupiga vita vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, ili kufikia malengo.

MWISHO.

 

 


Warning: file_get_contents(): http:// wrapper is disabled in the server configuration by allow_url_fopen=0 in /data/40/5/71/99/5397425/user/6768456/htdocs/portal/wp-content/plugins/xt-visitor-counter/xt-visitor-counter.php on line 48

Warning: file_get_contents(http://api.xtrsyz.org/xt-visitor-counter/default.php?domain=www.pembapress.club&time=1731634549): Failed to open stream: no suitable wrapper could be found in /data/40/5/71/99/5397425/user/6768456/htdocs/portal/wp-content/plugins/xt-visitor-counter/xt-visitor-counter.php on line 48