NA HANIFA SALIM, PEMBA.
KAMISAA wa Sensa ya watu na makaazi Zanzibar mwaka 2022 Balozi Mohamed Haji Hamza amewapongeza waandishi wa habari Kisiwani Pemba kwa kuwa sehemu ya kufanikisha zoezi la sensa lililofanyika Agost 28 mwaka jana.
Alisema, waandishi wa habari ni wadau muhimu ambao walichangia kwa kiasi kikubwa ufanikishaji wa zoezi hilo hivyo, aliwataka waandishi hao pia kuwa sehemu ya uhamasishaji matumizi ya takwimu za sensa ya watu na makazi mwaka 2022.
Balozi Hamza aliyasema hayo, alipokuwa akifunguwa semina ya uhamasishaji matumizi ya takwimu za sensa ya watu na makazi mwaka 2022 iliyowashirikisha waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali Kisiwani Pemba, iliyofanyika ukumbi wa kiwanda cha makonyo Wawi Chake chake.
“Tokea mwanzo tumeanza vizuri sana, mumetimiza wajibu mkubwa sana katika kufanikisha jambo hili, mumenipa faraja sana tangu kuanza hadi kumaliza zoezi nawapongezeni sana”, alisema.
Aidha alisema, ili wananchi, Serikali, taasisi, wahisani, wadau mba ukoli mbali pamoja na waandishi wa habari ambao ni sehemu muhimu ya wadau waweze kupata idadi nzuri ya sensa, lazima wahakikishe matokeo ya sensa yanawafikia waliofikiwa na matumizi yake yanakuwa sahihi kwa malengo yaliyokusudiwa.
Akitoa maelezo mafupi kuhusu matokeo ya sensa na mwongozo wa matumizi Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar Salim Kassim Ali alisema, Agosti 28 mwaka 2022 Tanzania ilifanya zoezi la sensa ambapo baada ya sensa walifanya uchambuzi wa takwimu na kutoa matokeo ya mwanzo ya sensa.
“Ofisi ya Taifa ya takwimu tunaendelea na kuchakata takwimu hizi za sensa lakini kwa umuhimu wake na kuona watumiaji ni wananchi ndipo tukaona tukutane na waandishi wa habari na wadau mbali mbali kufanya semina hii ya uhamasishaji matumizi ya takwimu za sensa”, alisema.
Nae Kaimu Mtakwimu mkuu wa serikali Pemba Said Mohamed alisema, takwimu ni muhimu katika kuhuisha sera , katika kutunza mipango mbali mbali ya maendeleo na ni muhimu katika kufanya matumizi sahihi ya nchi yao.
Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya waandishi wa habari Bakar Juma Mussa alisema, uandishi wa habari wenye takwimu ndio unaoleta uhalisia wa wanaohitaji huduma hivyo aliiwaomba viongozi wasiwe wachoyo wa kuwapa takwimu waandishi kwa maslahi ya Watanzanzia.
Hata hivyo akifunga semina hiyo Ofisa Mdhamini Tume ya mipango Pemba Khamis Issa aliwaomba waandishi wa habari, kuzifikisha taarifa hizo kwa walengwa ili malengo ya kufanyika sensa ya watu na makaazi liweze kufikiwa.