Friday, November 15

WAKULIMA Kisiwani Pemba waneshauriwa kulima Kilimo hai ili kuondokana na utumiaji wa mbolea za kikemikali katika mashamba yao.

NA ABDI SULEIMAN.
WAKULIMA Kisiwani Pemba waneshauriwa kulima Kilimo hai ili kuondokana na utumiaji wa mbolea za kikemikali katika mashamba yao. .
Hayo yalielezwa na Mkuu wa Idara ya maendeleo ya Kilimo Kisiwani Pemba Asha Omar Fakih Kwa niaba ya Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo Idrisa Hassan wakati wa kukabidhi vyeti Kwa vikundi 9 ambavyo vimepata elimu hiyo Kwa ihsani ya Milele Foundation huko Chimba Wilaya ya Micheweni Pemba.
Alisema kuwa Kilimo hai ni jambo muhimu  sana na Lina umuhimu Mkubwa kwani linazingatia afya Kwa Mkulima lakini pia hata Kwa mlaji.

Asha alifahamisha kuwa hivi Sasa wakulima wengi wamekuwa walimu na kutumia madawa kupindukia jambo ambalo ni hatari Kwa afya ya mwanaadamu pamoja na ardhi ambayo inayotumika.
Mkuu huyo alisema kiukweli Kilimo hai kina tija na soko lake ni zuri ingawa Kwa visiwani soko halina uhakika.
“Ipo haja Kwa wenzetu Milele Zanzibar Foundation na wafadhili wengine ambao tunashirikiana nao katika Hili kuweza kutafuta eneo tukaweza kuwa na soko la Kilimo hai kwani wako watu wengi ambao wanapenda kula vyakula ambavyo havina kemikali,” alisema Asha.
Sambamba na hayo Mkuu huyo wa Idara alibainisha kuwa hivi Sasa Kuna wimbi kubwa la wagonjwa wa kansa nchini kutokana na vyakula wanavyotumia kuwa na kemikali.
“Hivi Sasa wakulima wengi tumekuwa ni wataalamu na tumekuwa tunajiamulia wenyewe dawa gani mtu aweke katika shamba lake, ukiangalia Kuna baadhi ya wakulima wanadiriki kuweka dawa ya wanyama katika mashamba yao jambo ambalo ni hatari Kwa afya ya mwanaadamu,” alieleza Asha.
Mapema Meneja wa Milele Zanzibar Foundation Kisiwani Pemba ambao ndio wafadhili wa mafunzo hayo, Abdalla Said Abdalla  alifahamisha kuwa taasisi yao kupitia mradi wa Kilimo hai ulianza 2019 umeweza kuwafikia wakulima 1190 na kuwasaidia pembejeo za mbegu pamoja na kuwafundisha mafunzo Bora ya Kilimo bila ya kemikali.
Aidha Milele imejipanga kutoa mafunzo zaidi Kwa wakulima na kusaidia kufikia masoko Kwa mashirikiano na taasisi ya TOAM.
“Kupitia kituo chetu Cha ubunifu tumeweza kutengeneza mbolea ya mwani ambayo iko kwenye majaribio ya mwisho Kwa ajili kutumika”, alisema Meneja Abdalla.
Hata hivyo Abdalla alieleza kuwa changamoto kubwa iliyopo ni uelewa mdogo Kwa jamii kuhusu Kilimo hai kwani wengi wanadhani Kilimo hai hakiwezekani.
“Changamoto nyengine ni ukosefu wa pembejeo za Kilimo hai kwani Bado ni tatizo na wakulima wengi wanategemea mvua na hii inachangia mavuno kuwa hafifu,” alisema Abdalla.
Nae Mkufunzi kutoka Shirika la Kilimo hai Tanzania (TOAM) Mapambano Peter alieleza kuwa lengo la mradi huo ni kuhakikisha mbinu na teknolojia za kilimo hai zinakuwa sehemu ya mifumo ya kisheria,’program’ na miongozo mbalimbali ya kitaifa ili uzaliahaji,usalama wa Chakula na ufikiaji wa masoko.
“Mradi huu unatekelezwa katika Nchi 9 za Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya,Uganda,Rwanda,Benin,Ethiopia,Mali, Nigeria,Senegal na Madagascar,” alisema Mapambano.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Tumbe Wilaya ya Micheweni Said Saleh Salim aliitaka taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kuendelea kuwaunga mkono wakulima katika Kilimo hicho licha changamoto zilizopo hasa suala zima la mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa upande wangu naahidi kushirikiana wakulima na Viongozi katika Kilimo hichi ili kuona faida kubwa inapatikana Kwa wakulima wetu,” alifahamisha Said.
Nae Mkulima kutoka Wambaa Mkoani Pemba Hafidh Juma Ali alieleza kuwa faida kubwa ambayo inapatikana katika Kilimo hai ni kuitunza ardhi na kuifanya kuwa na rutba muda mrefu.
“Lakini pia faida kubwa zaidi ambayo inapatikana ni usalama wa Chakula na hili ndilo jambo la msingi kabisa,” alisema Hafidh
Katika hafla hiyo jumla ya vikundi 9 viliweza kukabidhiwa vyeti ikiwa ni pamoja na Kikundi Cha Kitandu,Daya Cooperative, Tujali wakati, Mwanamke Kazi, Tuaminiane, Tupendane, Jambo group na Uwamambo.