Friday, November 15

KUNDI la Pili la watalii 107 kutoka Mataifa Mbali mbali duniani wamewasili Kisiwani Pemba.

NA ABDI SULEIMAN.

 

KUNDI la Pili la watalii 107 kutoka Matifa Mbali mbali duniani wamewasili Kisiwani Pemba, huku 88 kati yao ni kutoka taifa la Marekani.

 

Watalii hao ambao wamefika katika bandari ya Mkoani na kwenda kutembelea maeneo mbali mbali yenye vivutio vya kiutalii ambavyo vinapatikana ndani ya kisiwa hicho.

 

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea watalii hao, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, alisema nia ya Serikali ya awamu nane ni kuhakikisha kwamba Pemba inafunguka zaidi kiutalii, kama ilivyo adhma ya Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi, kuifungua Pemba kiutalii na kiuwekezaji.

 

Alisema ujio wa watalii hao wengi wao ni kutoka nchini Marekani, hivyo Pemba ni faraja ujio wao kwani wageni wangi wanapita katika mlango wa bandari ya Mkoani.

 

“Ujio wa watalii hao kwangu mimi kama mkuu wa Wilaya ni faraja, anafarajika kuwa wageni wanapita katika mlango wa bandarui ya mkoani, bandari ambayo inaharakati nyingi za uingiaji na upokeaji wa wageni,”alisema.

 

Aidha alisema wageni hao watasaidia kukitangaza kisiwa cha Pemba kiutalii, pia watachangia katika pato la uchumi kwa kutembelea maeneo ya kihistori na mambo ya kale na wananchi wataweza kuuza bidhaa zao wanazozifanya.

 

“Ziara hii nimuhimu, Pemba ya sasa inazidi kufunguka kiutalii na wananchi kuchangamkia fursa ya utalii na watalii, naziomba kampuni zinazoleta wageni kuendelea kuleta wageni Pemba ni sehemu salama kwa sasa,”alisema.

 

Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Pemba Zuhura Mgeni, alisema watalii hao wataweza kutembelea vivutio mbali mbali vya kiutalii vilivyomo ndani ya Kisiwa hicho.

 

“Watalii hawa wataweza kujionea mazingira mazuri ya Pemba, ikiwemo popo wa Pemba, vitalu vya miche ya mikarafuu na majengo ya asili na kiutamaduni,”alisema.

 

Hata hivyo alisema ni kubwa kwa wananchi wa Pemba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwani viongozi wamejitahidi kuitangaza kiutalii kisiwa cha Pemba.

Naye Mkurugenzi wa EA Holidays Pemba Duwe Daudi alisema hii ni Meli ya pili ndani ya siku saba kuwasili kisiwani Pemba, ambapo awamu ya kwanza watalii 103 na awamu ya pili watalii 107 na kufanya jumla ya watalii 210 kuwasili Pemba.

 

alisema watalii hao wataweza kutembelea vivutio mbali mbali vya kiutalii, huku mikakati yao ni kuongeza meli tatu ndani ya mwaka huu moja kuwasili Mwezi wa Sita na Nyengine mwezi wa tisa na 12.

 

Hata hivyo alisema vitu vilivyochangia kuwasili kwa watalii hao ni, kutokana na ujio wa Royal Tour iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, ambao Pemba iliweza kufika.

 

Watalii hao ni kutoka mataifa ya Marekani, Berarusi, Uwengereza, Urugwayi, South Africa, Sishel, Ureno, Italii, Israil, Ufaransa, Kanada na Austaralia.

MWISHO