Tuesday, January 14

KAMATI YA BUNGE ARDHI, MALIASILI NA UTALII YARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI WA MIRADI HIFADHI YA TAIFA TARANGIRE

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekagua ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Kuro na mradi wa ujenzi wa jengo la kupumzikia abiria wenye thamani ya shilingi milioni 700 ikiwa ni sehemu ya miradi ya UVIKO – 19 tarehe katika Hifadhi ya Taifa Tarangire tarehe 14.3.2023.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii , Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) amesema miradi hiyo ina manufaa makubwa kwa Taifa katika kuongeza idadi ya watalii nchini.
“Tunampongeza na kumshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kutoa fedha nyingi na maelekezo ya kuendelea kusisitiza utekelezaji wa miradi na kwa namna ya kipekee tunaipongeza Wizara na TANAPA, tumeridhika na kazi iliyofanyika” alisema Mhe. Mnzava.
Akizungumzia mradi wa maboresho ya kiwanja cha ndege cha Kuro, Mhe. Mzava amesema kuwa ni jukumu la menejimenti kuhakikisha ukarabati unafanyika mara kwa mara kwani uwepo wa kiwanja hicho utaongeza thamani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema miradi hiyo ni muhimu na wanatarajia itakamilika kwa wakati ili dhamira ya serikali itimie ya kuendelea kupokea watalii wengi nchini.
“Tunataratajia miradi hii ikamilike kwa wakati na tunameahidi mpaka mwezi Julai 2023 miradi hii yote itakuwa imekamilika na tunamshukuru Mhe. Rais kwa fedha za UVIKO – 19 ambazo zimesaidia sana kuboresha miundombinu katika Hifadhi zetu.” alieleza Mhe. Masanja.
Kwa upande wake Kamishina wa Uhifadhi, William Mwakilema wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), amemuahidi Mwenyekiti wa Kamati hiyo kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na kamati.
“Tumeelekezwa kuwa tuhakikishe miradi hii inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa pamoja na kufanya ukarabati mara kwa mara nasi tunamuahidi Mwenyekiti na kamati yake kuwa tutatekeleza hayo yote” alisema Kamishina Mwakilema .
Sanjari na hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA Jenerali Mstaafu George Waitara, amesema kuwa shirika limefikia asilimia 87 ya utekelezaji wa miradi yote inayotokana na fedha za UVIKO-19.
“Tumepokea fedha zote na hadi sasa tumefikia asilimia 87 ya utekelezaji wa miradi yote katika shirika inayotekelezwa katika hifadhi za Kilimanjaro, Burigi Chato, Saa Nane, Saadani, Mkomazi, Serengeti, Nyerere, Katavi, Gombe na hapa Tarangire” alisema Jenerali Mstaafu Waitara.
Hifadhi ya Taifa Tarangire ni miongoni mwa Hifadhi za Taifa Tanzania ambayo ni maarufu kwa uwepo wa makundi makubwa ya tembo wenye maumbo makubwa, ikiwa na miti mikubwa ya mibuyu.