Friday, January 10

TAHADHARI JUU YA TETESI ZA UGONJWA USIOJULIKANA MKOANI KAGERA.

Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Wizara ya Afya imepokea taarifa za uwepo wa ugonjwa ambao bado haujajulikana katika kata za Maruku na Kanyangereko wilaya ya Bukoba vijijini Mkoani Kagera.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari na Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Tumaini Nagu leo Machi.16.2023 jijini Dodoma imebainisha kuwa , jumla ya watu 7 kutoka vijiji vya Bulinda na Butayaibega wanasadikika walipata dalili za homa , kutapika, kutokwa na damu katika maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi huku wawili wakiendelea .

Prof.Nagu amewataka wananchi kuchukua hatua na tahadhari mbalimbali ikiwa ni pamoja na mtu yeyote mwenye dalili za homa , kutapika, kuharisha, kutoka damu na mwili kuishiwa nguvu anashauriwa kuwahi Kituo cha kutolea huduma za afya mapema kwa ajili ya uchunguzi na matibabu, kutoa taarifa mapema kwenye kituo cha kutolea huduma kilicho karibu au kupiga simu namba 199 bila malipo.

Prof.Nagu ameainisha tahadhari zingine ni pamoja na kuepuka kumgusa mgonjwa au majimaji ya mwili mfano mate ,machozi, damu, mkojo na kinyesi yatokayo kwa mgonjwa au mtu yeyote mwenye dalili huku tahadhari ikitolewa kujikinga na majimaji yoyote iwapo kutakuwepo na ulazima wa kumhudumia mgonjwa.
Kuhusu suala la usafi.

Prof.Nagu amehimiza kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono ili kujikinga na magonjwa yote ya kuambukiza na kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono na kuweka mkazo wa kushirikiana na wataalam wa afya katika shughuli za misiba na mazishi.

Hata hivyo,Prof. Nagu amesema kwa upande wa Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu na kuchukua hatua za kuthibiti ili usisambae ikiwa ni pamoja na Sampuli kutoka kwa wagonjwa na waliofariki zimechukuliwa ili kubaini chanzo na kuthibitisha aina ya ugonjwa huo, ufuatiliaji wa watu wenye viashiria vya ugonjwa kwenye jamii na vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na waliotengamana na wagonjwa hao ili kuwapa huduma stahiki za kimatibabu.