Friday, January 10

Washauriwa kulima mazao mbadala, wakati wa msimu wa kilimo unapofika kukabiliana na soko.

NA ABDI SULEIMAN.

WAKULIMA wameshauriwa kulima mazao mbadala, wakati wa msimu wa kilimo unapofika ili kukabiliana na soko la uuzaji wa bidhaa wanazozalisha.

Ushauri huo umetolewa na Afisa wa Maendeleo ya Kilimo Wilaya ya Wete Makame Hamad Said, kwenye mkutano wa tathmini ya utekelezaji wamradi wa Amani na Maendeleo kwa Vijana na wanawake unaotekelezwa kwa pamoja na NCA, ZANZIC, ELECT-ND na kufadhiliwa na Ubalozi wa Norway.

Alisema mara nyingi unapofika msimu wa kilimo wakulima wengi huzalisha tungule na wanapokwenda sokoni, hukosa bei halali ambayo wangeweza kurudisha gharama za udhalishaji.

Afisa huyo alisema wakulima kabla ya kuanza kulima, wanapaswa kuliangalia soko likoje, na watakachozalisha kiwe cha kipekee na sio kufanana na wakulima wote.

“Leo utaona msimu mzima kila mkulima analima tungule, haangalii kama mimi nilime chengine ili niweze kuliteka soko, mwisho wasiku bidhaa zinakosa soko,”alisema.

Naye Afisa Kilimo Wilaya ya Chake Chake Rashid Mohamed, alisema Wizara ya Kilimo jukumu lake ni kutoa elimu kwa wakulima, ili mradi ukimalizika wakulima waweze kuendelea na shuhuli zao za kilimo.

Aidha alisema vizuri vikundi kuachana na kulima kwa kutegemea mvua, badala yake walime kwa kuangalia mahitaji ya soko na kutumia umwagiliaji.

Akiwasilisha tathmini ya vikundi vya Kilimo Mtaalamu wa Kilimo Mfaume Khamis Juma, alisema mwaka 2022 walianzisha 45 vya ufugaji wa kuku na vikundi 36 vya kilimo, ambao waliwafikia wafunguja 410 na wakulima 300.

Alisema waliweza kutoa elimu juu ya ufugaji bora wa kuku wa kisasa na kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kwa wakulima, pamoja na ufuatiliaji wa vikundi hivyo.

“Tayari tulishawatembelea wakulima na kuwapatia ushauri nasaha juu ya shuhuli zao wanazozifanya ili tuweze kupata tija zaidi, “alisema.

Akizungumzia mafanikio alisema waliweza kuvifikia Vikundi 81 vyenye wanachama 710, na kuwaunganisha wakulima na wauzaji wa pembejeo za kilimo na ufugaji, wakulima kupitia shuhuli hizo ni biashara kama vile mayai, kuku, mboga mboga na kushawishi zaidi ya wakulima 300 ili kuachana na kilimo cha kimazowea na kuingia kilimo cha kukabiliana na Tabianchi.

Kwa upande wa Changamoto alisema ni kuongezeka kwa bei ya pembejeo ya kilimo na ufugaji, ukosefu wamasoko kwa wazalishaji wa mboga mboga na kuku na ukosefu wamaji ya uhakika.

Alisema matarajio yao ni kuongeza idadi ya wakulima na wafugaji na kuhamaisha ufundishaji wa kilimo boroa cha mboga mboga na matunda.

Wakiwasilisha taarifa za utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa Interfeath Zanzibar Mchungaji Shukuru Maloda, alisema wanashajihisha mazungumzo ya dini mbali mbali kwani dini zote zinashajihisha suala la amani nchini.

Kwa upande wake Mchungaji Benjamini Kisaga, alisema vikoba wanachama wengi ni wakulima na wafugaji, vikoba makoongwe, Chake Chake, Wete na Micheweni.

Alisema changamoto iliyotokana katika vikundi hivyo watu wanapokopa wanashindwa kurudisha kwa wakati, wapo wanachama ambao wamenufaika na vikomba hivyo.

Kwa upamde wake muakilishi kutoka NCA Herieth Josephat, alisema wanakusudia kutowa taaluma kwa walengwa wao, ili waweze kuibuwa mahitaji kabla ya kuanza uzalishaji.

Hata hivyo alisema vijana wanapolima wanakumbana na changamoto kubwa ya soko, huku wakilima zao moja na wanapaswa kupatiwa mafunzo kabla ya kuanza uzalishaji ili waweze kukwepana na changamoto za masoko.

MWISHO