NA ABDI SULEIMAN.
WIZARA ya elimu na mafunzo ya amali Kisiwani Pemba, imepokea Msaada wa vyakula wenye thamani ya Tsh 33,618,000/- Kwa Skuli 16 zenye dahalia kutoka Kwa taasisi za Ifraj na Milele Zanzibar Foundation Kwa ajili ya mwezi mtukufu wa ramadhani.
Skuli ambazo zimepatiwa Msaada huo ni pamoja na Madungu Sekondari, Fidel Castro, Dk, Salim Ahmed, Dk, Aman, CCK, Dk, Idrisa, Chasasa, Utaani, Pindua, Kengeja Ufundi, Amini Islamic,Vitongoji VTC,Daya VTC, Istiqama pamoja na Ambasha.
Akipokea Msaada huo huko katika Ofisi za Milele Foundation, Ofisa Mdhamini wa Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Pemba Mohammed Nassor alieleza kuwa amefarajika sana Kupata Msaada huo kwani umekuja muda muafaka.
Ofisa huyo alifahamisha kuwa jambo ambalo wamelifanya taasisi hizo ni kitendo cha Uzalendo Mkubwa na nijambo lakupigiwa mfano kwani Kuna wengi na Wana uwezo lakini wanashindwa kusaidia wenzao.
” Milele Zanzibar Foundation imekuwa ikisaidia sana katika sekta ya elimu Unguja na Pemba na hii sio mara ya kwanza Kwa taasisi hizi kutoa mchango wake kwa wanafunzi,” alisema Mdhamini.
“Hichi ambacho kimetolewa na ndugu zetu Hawa ni kikubwa sana kwani Kuna wengi ambao wanacho lakini wanashindwa kuwasaidia ndugu zao hata katika kipindi Cha mwezi mtukufu wa ramadhani,” alisema Mohammed.
Sambamba na hayo Ofisa huyo aliwataka walimu wakuu wa Skuli hizo kukisimamia Chakula hicho ili kiweze kutumika kama ilivyo kusudiwa.
“Napiga marufuku Kwa wapishi wote kutumia simu wakati wakiwa kazini kwani kumekuwa na uharibifu Mkubwa wa Chakula, hivyo kuanzia Sasa sitopenda kuona mpishi wakati wa jikoni yeye anashughulikia simu,” alisema Ofisa Mdhamini.
Mapema Mohammed aliwataka wanafunzi kushughulikia masomo Yao hasa katika kipindi hichi Cha mfungo wa ramadhani na kusisitiza kuwa familia zao zinawategemea wao.
“Ole wake mwanafunzi yeyote ambae atajishughulisha na vitendo vya udhalilishaji tutamfukuza na hatutounga mkono vitendo hivyo, niwaombe wanafunzi Kwa hili tushirikiane Kwa pamoja Ili tuweze kutokomeza vitendo hivyo,” alisema Ofisa.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Milele Zanzibar Foundation Abdalla Said alisema kuwa Msaada huo sio wa mwanzo kutoa Kwa Skuli zenye bonding Kwa upande wa Kisiwa Cha Pemba.
Alieleza kuwa tokea mwaka juzi walianza zoezi hili ambapo Kwa mwaka huu wameweza kusaidia Skuli 16 zenye bonding huku akimtaka Ofisa Mdhamini kufikiria kama Kuna Skuli yeyote ambayo imesahauliwa kutoa taarifa ili nayo iweze kupata Msaada huo.
“Kwa Siku ya tutaweza kupatia wanafunzi wetu ambao wanaishi dakhalia vyakula ambavyo vitaweza kuwasaidia katika mwezi huu mtukufu wa ramadhani na tumeweza kuchukuwa Skuli za Serikali lakini pia na zile binafsi,” alifahamisha Abdalla
“Vyakula ambavyo tutaweza kuwapatia ni pamoja na mchele paketi 196, unga wa ngano paketi 63, sukari paketi 46, mafuta ya kula box 42 pamoja na tende box 116,” alieleza Abdalla.
Sambamba na hayo Abdalla alifahamisha kuwa mbali na kutoa msaada huo Kwa wanafunzi lakini pia wamedhamiria kufanya kama hivyo Kwa familia 5200 na tayari zoezi Hilo limeshaanza.
“Nitoe wito Kwa wananchi kuwa Kwa mwaka huu hatutokuwa na Msaada wowote ambao utatolewa hapa ofisini, hivyo hatutapendelea kuona wananchi wanakuja hapa kudai futari,” alieleza Abdalla.
Nae Mratibu wa NGO’s Kisiwani Pemba Ashraf Hamad Ali alizipongeza taasisi hizo Kutokana na kujitolea kwao kusaidia jamii.
Alisema kuwa lengo la Serikali kuruhusu taasisi hizi kufanya kazi ni kuweza kuisadia Kwa Yale mambo ambayo wanaweza kufanya hivyo bila ya tatizo lolote.
“Serikali haikufanya makosa kuipa kibali Milele Zanzibar Foundation kufanya kazi zake hapa, imekuwa ni taasisi moja wapo ambayo imekuwa bega Kwa bega katika kutatua changamoto Kwa jamii, tunawapa hongera waanzilishi wa jumuia hizi,” alisema Ashraf.
Sambamba na hayo aliwataka wanafunzi kujitahidi sana katika masomo Yao na kuacha kushiriki mambo ambayo hayana tija kwao.
“Kwa upande wa walimu wangu tuendelee kujitolea kwani kazi ya ualimu malipo yake ni Kwa Mwenyezimungu tu hakuna pengine,” alifahamisha Ashraf.
Akitoa neno la shukurani Kwa taasisi hizo Kwa niaba ya wenzake, Mwanafunzi Fatma Salim Mohammed (Madungu) alisema kuwa Milele imekuwa ikiwasaidia sana na kueleza kuwa Hilo sio la mwanzo.
Alieleza kuwa Milele imeweza kuwaondoshea tatizo la maji ambalo lilikuwepo Skulini kwao Kwa muda mrefu Kwa kuwapatia matangi ya kuhifadhia maji.
“Lakini pia tumefarajika Leo hii kusikia Milele wametudhamini kitoweo Cha nyama ya ng’ombe, hii kwetu ni faraja kubwa sana kwani dakhalia ni nadra sana Kupata vitu kama hivi,”alisema mwanafunzi huyo,