THUREYA GHALIB – PEMBA.
NENO Uchumi wa Buluu likitamkwa linaleta faraja kwa kila Mwananchi wa Zanzibar,kwani wengi wao wanalitafsiri kama ni ukombozi wa kiuchumi unaotokana na vilivyomo ndani ya Bahari.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi ameunda Wizara maalum ya uchumi wa Buluu, ilikuweza kuwasaidia wananachi wake na kuinua uchumi wa Nchi.
Inaaminika kwamba Bahari ni moja ya eneo kubwa lenye rasilimali nyingi lakini bado halijawahi kutumika vilivyo na hivyo kuwafanya wananchi kubakia kwenye Umaskini wakati nyenzo za kuondokana zimo mikononi mwao.
Kwa kuliona hilo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi ameianzisha Wizara ya uchumi wa buluu tu ,kwa dhamira kubwa ikiwa kuwakomboa wananchi wake katika umaskni kupitia nyanja hiyo.
Katika kampeni zake za kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar katika kiwanja cha skuli ya Micheweni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa kaskazini Pemba alizungumzia maneno haya:-
Nanukuu “Nimekuwa nikizungumzia uchumi wa buluu katika hotuba zangu nyingi kwa maana ya utalii, uvuvi, mafuta, gesi na viwanda vinavyotumia malighafi za bahari, lakini haina maana tutasahau kilimo bado kilimo kitapewakipaumbele”alisema
Kwa mukhtadha huo amewataka ,wananchi kuunda vikundi mbalimbali vikiwemo vya ufugaji samaki,majongoo bahari na wakulima wa mwani.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haiko nyuma kama ahadi ya Rais aliyotowa imeamuwa kuwasaidia Wananchi ambao wamejikita katika miradi hiyo nyenzo za kuweza kufikia azma hiyo ya Serikali ili kuweza kufaidika na dhana hiyo ya uchumi wa Buluu.
Mwandishi wa Makala hii ameamua kugusia kipengele kimoja cha uchumi wa Buluu juu ya ufugaji wa majongoo bahari ,ili kuweza kwani inaonekana kuwa faida kubwa katika soko la nje.
Ni mwendo wa takriban saa moja kutoka katika Bandari ya Wete mpaka katika kisiwa cha Uvinje ,kilichopo Wilaya ya Wete, Mkoa wa kaskazini Pemba ili kupata maelezo kutoka kwa mfugaji wa majongoo haya.
Na huko ndipo alipokutana na wanakikundi cha juhudi na maendeleo , ambacho kilianzishwa mnamo tarehe 16/9/2019.
WAFUGAJI WANASEMAJE KUHUSU MAJONGOO BAHARI
Wanakikundi hao wamefahamisha kuwa Jongoo bahari kikawaida anachukua muda wa miezi 8 hadi 12 kukuwa na kuvunwa.
Moja ya sifa ya Majongoo hao hawahitaji chakula cha gharama kwa vile wanafyonza mchanga wa bahari ambacho ndio chakula chao.
Wanakikundi hao wanasema mpaka sasa aina ya majongoo wanayofugwa na kikundi hicho ni jongoo weupe ,lakini kwa siku zijazo wanania ya kufuga aina nyengine ya jongoo hao.
” Kwa hivi sasa tumekuwa tunafuga Majongoo aina moja lakini tunatarajia hapo baadae tufuge aina nyengine ili kuendana na Soko”,wanaeleza.
Kama tunavojua hakuna kila kitu lazima kianzie chini ndipo kipande juu ,basi na wanakikundi hawa walianza na ufugaji wa majongoo 13 tu na kwa sasa jambo linaloleta faraja kwao wanaozaidi ya majongoo 200.
Kwa upande wa uzazi wa majingoo hao , wanatagaa vifaranga na wanavichukua na kuvieka sehemu mbali na wale waliokuwa wakubwa ili kuwahifadhi waweze kuishi .
WAFUGAJI WAMEHAMASIKAJE KWA SASA?.
Wanakikundi cha Juhudi na maendeleo wa Kisiwa cha Uvinje wanasema wamehamasika na ufugaji wa majongoo bahari kwa lengo la kujiongezea kipato jambo ambalo linawasaidia katika kupiga hatua katika maisha yao.
Wanaeleza kuwa kila siku zinavyozidi kuenda, ndivyo wanavyozidi kuhamasika na Ufugaji wa majongoo hayo ,kwani wamekuwa wakipata ujuzi mpya kila wanaondelea na ufugaji huo.
“ Kila siku zinaposonga ndio tunahamasika zaidi kuhusu ufugaji wa majongoo bahari kwani tumekuwa tukipata ujuzi na mbinu za Ufugaji”, wanasema.
Mmoja kati ya Wanakikundi hao akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa kikundi hicho Sharif Hamad Haji alisema kuwa walihamasishwa na mmoja ya mfugaji wa majongoo kutoka Kisiwa cha Kojani , na kuelezewa faida na hasara zake ,ndipo walipoamua kuanza rasmi shughuli hiyo.
Anasema baada ya kupata taaluma hiyo walianzisha shamba na kuunda kikundi cha watu kumi na mbili na kuanza ufugaji wa majongoo bahari kwa awamu ya kwanza.
Anaeleza kuwa kwa hatua ya mwanzo walipata kasoro ndogo ndogo katika ufugaji wao,hivyo waliomba msaada kutoka Idara ya maendeleo ya uvuvi wawasaidie kuwaongoza ili kuondoa kasoro hizo.
“Mbali na kuwa Idara ya Maendeleo Uvuvi inachukua jitihada kubwa katika kutupa elimu na kusababisha faida kubwa kwetu,bali tunaomba wazidi kuwepo karibu na sisi kutueleza sheria zao ili tufanye shughuli zetu tukiwa salama”anaeleza Mwenyekiti huyo.
Anafahamisha waliwahi kuvuna mara tatu,pesa walizozipata ziliwasaidia kujikimu kimaisha pamoja na kuendeleza ufugaji wao na kununua nyenzo za kujengea uzio.
Mwenyekiti huyo alisema kutokana na kuhamasika uzalishaji umeongezeka na kulazimika kuongeza ukubwa wa shamba kutoka mita ishirini hadi kufikia mita ishirini na saba.
“Tumerefusha mita za kinga (kuta) ambazo zitakinga wale wanaotembea tembea katika eneo la shamba ili wasituharibie takriban mita 20 “anasema Sharif’
CHANAGAMOTO ZA UFUGAJI WA MAJONGOO BAHARI ZIKOJE?
Changamoto wanazozipata ni ukosefu wa taaluma kwao na wameiomba Serikali kuwapatia wataalamu kwenda kuwafundisha zaidi, sambamba na kukosa fedha za kujikimu na kutokuwa na nyenzo za kurutubisha vizuri mashamba yao.
Anafahamisha kuwa kwa vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapenda maendeleo kwa Wananchi wake, hivyo ilichukua jitihada za maksudi kupitia idara ya Maendeleo ya Uvuvi na kufika katika maeneo yao na kuona mashamba pamoja na kuyachukuwa majongoo kupelekwa katika monyesho mbalimbali.
Kwa Upande wake mmoja wa Mwanakikundi hicho Mboja Juma Makame anasema lengo la kujiunga na kikundi hicho ni kujikomboa na umaskini.
Anaeleza tangu wajiunge na kikundi hicho ameweza kufaidika na mambo mengi ikiwemo elimu pamoja na kufahamu faida mabli mbali za ufugaji wa majongoo hayo.
JEE SOKO LA KUUZIA MAJONGOO HAO
LIKOJE.
Wafugaji hao wanasema Soko la majongoo lipo vizuri soko la ndani jongoo bahari mmoja anauzwa kwa shilingi elfu tano (5,000/=), lakini soko la njee kilo moja ni zaidi ya shilingi elfu Thamanini (80,000).
Wanasema kwa sasa wanaweza kupata mahitaji yao ikiwemo kusomesha watoto,kupata chakula na mahitaji mengi ya kijamii na jongoo ambao wanauza ni jongoo wabichi.
JEE WATAALAMU WA UFUGAJI WA MAJONGOO
WANASEMAJE?.
Kwa upande wa Msimamizi wa shughuli za ufugaji wa mazao ya baharini kutoka idara ya maendeleo ya uvuvi Mohamed Salim Othman anasema shughuli hizi za ufugaji hapa Zanzibar zimeaanza katika miaka ya karibuni na kwa upande wa Pemba tayari wamekisha kuhamasika .
Anasema shughuli hiyo ilifanyika mara baada ya kufanyika takwimu na kuonekana rasilimali ya majongoo baharini imeanza kupotea ,tofauti hapo na zamani.
Anafahamisha kuwa mara baada ya kuonekana hilo ndipo walipoamua kushajihisha wavuvi ama watu wanaokaa karibu na bahari kuweza kufuga majongoo ili kuweza kuyanusuru yasipotee kabisa.
“Jambo ambalo lilisababisha kupotea kwa majongoo ,ni kutokana na kuzidi shughuli za uvuvi baharini ,hivyo tuliwazidi majongoo baharini na kusababisha kuanza kupotea na ikabidi wanapozaliwa wengi hufa kuliko wanaokuwa”anasema Msimamizi huyo.
Anaendelea kueleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuwarahisishia wafugaji kituo cha kuzalisha vifaranga Bait el raas ,miongoni mwa vifaranga hivyo ni majongoo bahari ,kaa na Samaki wa Mwatiko.
Anasema kuna mambo ya kuzingatia kabla ya kuanzishwa kwa ufugaji wa bahari ,hivyo kabla ya ufugaji ni muhimu kuonana na mtaalamu ili aweze kuwapa elimu wafugaji .
Hata hivyo anaeleza kuwa vyema Wananchi wakahamasika na ufugaji wa viumbe bahari,kwani itakuwa ni njia nzuri ya kumuunga mkono Rais wa Zanzibar Dk, Hussein Ali Mwinyi juu ya dhana ya uchumi wa buluu.
MWISHO.