NA ABDI SULEIMAN.
MKURUGENZI wa Jumuiya ya PEGAO Kisiwani Pemba Hafidh Abdi Said, amewataka Viongozi wa Majimbo, Serikali na Masheha kushirikiana na wananchi wa shehia husika katika kutatua changamoto zinazowakabili ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Alisema wananchi wamekuwa wakikukabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo suala la amaji safi na salama, umeme kwa baadhi ya vijiji, barabara, madaraja, elimu, vituo vya afya kufuata masafa marefu, changamoto ambazo zinaweza kutatua iwapo viongozi hao watasimamia ipasavyo majukumu yao.
Mkurugenzi huyo aliyaeleza hao katika mkutano na waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari Pemba, uliofanyika katika ofisi za Jumuiya ya PEGAO Chake Chake Pemba, ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya uongozi unaendeshwa na TAMWA-Zanzibar, ZAFELA na PEGAO kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway.
Aidha alisema katika mradi huo wahamasishaji jamii wamefanikiwa kuibua kero 44 kwa mwaka 2022, kufuatia mikutano 36 walioifanya katika Wilaya nne za Pemba.
“Wilaya hizo ni Wete kero 12, Micheweni 12, Chake Chake tisa (9) na Mkoani 11, tayari baadhi yao zilipatiwa ufumbuzi 17 na watendaji wa serikali baada ya ufuatiliaji, na wananchi kunufaika na maendeleo yao,”alisema.
Hafidhi alisema kero 10 zilitatuliwa katika kipindi kifupi cha uhamaishaji jamii, ambapo kero zote ikiwa zitaachiwa zitaathiri zaidi wanawake kufikia lengo lao la kushiriki katika nafasi za uongozi.
Hata hivyo Pemba imeshauri jamii, masheha na viongozi wa serikali kushirikiana kwa pamoja kupitia kamati za shehia kwa lengo la kuandaa mikutano, ili kujadili changamoto zinazowakabilia wananchi na kupatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo alisema viongozi wa serikali za mitaaa wanawajibu wa kuandaa mikuntano ngazi ya jamii ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili ili kujenga jamii yenye kufuata misingi ya usawa wa kijinsia kwa watu wote
katika kutambua umuhimu wa mwanamke, sheria na sera mbali mbali za zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya wanawake kushiriki katika demokrasia na uongozi, katiba ya zanzibar 1984, dira ya zanzibar 2050 zote zinatambua hilo,”alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa Tamwa Pemba Fat-hiya Mussa Said, alisema jamii imepata uwelewa wakutosha kutoka kwa wahamasishaji jamii, katika kuibua kero na kuweza kuzitatua.
“Hebu sote tuangalie kijiji cha mlindo kulikua na shida ya daraja, lakini wahamasishaji wetu baada ya kufanya mikutano na wananchi kufahamu dhamira ya wahamasishaji wetu, sasa kila kitu kipo sawa na watu wanapita,”alisema.
Aidha alisema jitihada mbali mbali zimefanywa katika kuwaandaa wanawake juu ya kuingia katika dektrasia na siasa, kupitia mafunzo mbali mbali walioyatoa kwa watia nia.
Kwa upande wake mratibu wa PEGAO Dina Juma, alisema ili mradi huo uweze kufanikiwa waandishi wa habari ni watu muhimu katika kuhamaisha jamii, juu ya kushiriki katika nafasi za uongozi na demokrasia.
MWISHO