NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WANANCHI wa Vikunguni shehia ya Ng’ambwa Wilaya ya Chake Chake wameiomba Serikali kuwafikishiwa huduma ya maji katika kituo chao cha afya, ili kuepuka usumbufu wanaoupata hasa kwa akinamama wanaokwenda kujifungua.
Walisema kuwa, kituo cha afya kinahitaji maji muda wote ili kuwasaidia wagonjwa wanaokwenda hapo, ingawa wanalazimika kwenda kuomba kwa majirani wanaoishi karibu na kituo hicho, jambo ambalo linawasababishia usumbufu mkubwa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wananchi hao walisema, akina mama wanaokwenda kujifungua ndio wanaopata shida zaidi, kwani wanaweza kukaa muda mrefu bila kusafishwa, hali ambayo inaweza kumsababishia magonjwa mengine.
Mwananchi wa kijiji hicho Fatma Khamis Mbarouk alisema, wamekuwa wakipata shida wanapokwenda na wazazi katika kituo hicho kutokana na ukosefu wa maji, jambo ambalo linawapa usumbufu kwani katika kijiji hicho kuna shida ya maji kwa sasa.
“Mpaka jana nimemleta mzazi hapa kituo cha Afya, ilinibidi nikaombe maji nyumba ile pale, sasa wakati mwengine na hapo unapokwenda kuomba pia mtu hana, kwa hiyo ni mtihani”, alisema.
Nae mwananchi Anu Juma Hamad alieleza kuwa, kwa vile hawapati maji safi na salama katika kijiji chao, kuna haja ya kuchimbiwa kisima katika kituo hicho cha Afya ili iwarahisishie wauguzi na madaktari wa kituo hicho kufanya kazi kwa ufanisi.
“Kitakapochimbwa kisima itawarahisishia madaktari kufanya kazi zao kwa ufanisi na urahisi na pia kwetu wananchi itatusaidia kuepukana na usubufu wa kuhodisha nyumba za watu kuomba maji”, alisema.
Wauguzi wa kituo cha Afya cha Vikunguni Shuwekha Bakar Salum na Time Malik Haji walisema kuwa, ni mwezi wa nne sasa wanakosa huduma ya maji safi na salama katika kituo chao, jambo ambazo linazorotesha utoaji wa huduma.
“Maji ni lazima katika kituo cha Afya chochote, bila ya maji hatuwezi kufanyakazi vizuri, kwa sasa tunalazimika kuwaambia hawa wanaoleta wazazi waende wakaombe maji ya kupata kumuhudumia mzazi wao”, walisema.
Afisa Mchamini Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilal Ali alieleza kuwa, katika kituo kilichokuwa na hali nzuri ya maji ni Vikunguni ingawa kipindi hiki cha kaskazi shida ya maji imejitokeza kila pahala.
“Kama Wizara tuna mpango kwa kila kituo kinachozalisha kuhakikisha tunapeleka huduma ya kuchimba kisima cha dharura, kwa Wilaya ya Chake chake tumeanza na kituo cha Afya Pujini na maji tayari yameshapatikana”, alisema Mdhamini huyo.
Alisema kuwa, pia watachimba kwenye vituo vyengine ambavyo ni Tundauwa, Wesha na Vikunguni, hivyo aliwataka wananchi wawe wastahamilivu wanafanya juhudi ya kuwasiliana na ZAWA ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana”, anasema.
“Jana tulipeleka maji katika hospitali ya Wilaya Vitongoji kwa njia ya magari kwa hiyo na vikunguni tutapeleka maji hayo kwa njia ya magari kwa kipindi hiki kwenye shida ya maji, ili kuona kuwa huduma zinaendelea kutolewa katika kituo hicho”, alisema.
Hata hivyo kituo cha Afya Vikunguni kinakabili wa ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, hali ambayo inazorotesha utoaji wa huduma pamoja na kusababisha usumbufu kwa wananchi.
MWISHO.