MBUNGE wa Jimbo la Mkoani kupitia CCM ambae pia ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Makame Mbarawa Mnyaa amekabidhi pampu moja ya maji Kwa mamlaka ya maji (ZAWA) yenye thamani ya Tsh 28milioni Kwa ajili ya Kisima Cha Ulenge katika shehia ya Chokocho .
Akikabidhi pampu hiyo huko Ulenge Chokocho, Mbunge huyo alieleza kuwa Nia ya Serikali zote mbili ni kuhakikisha zinatatua changamoto zote zinazowakabili wananchi wake.
Profesa Mbarawa alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo katika Kisima hicho ni miundombinu pamoja na Visima wenyewe kukauka kutokana na jua kuwa Kali.
“Kwa bahati mbaya sana hapa tunavyo Visima lakini pampu yetu ya kusukumia maji iliharibika na hivyo kufanya wananchi wa eneo hili kukosa huduma ya maji safi na salama Kwa muda Sasa,” alieleza Profesa Mbarawa.
“Kama Mimi ni Mbunge wa Jimbo hili la Mkoani ni wangu kushirikiana na wananchi pamoja na Viongozi wa Jimbo hili katika kuhakikisha matatizo yaliyopo katika jamii tunayatatua,” alisema Mbunge huyo.
Sambamba na hayo Mbunge huyo alifahamisha kuwa mbali na Kisima hicho lakini pia Kuna Visima vyengine ambavyo vimechimbwa lakini Hadi sasa vimekuwa na changamoto ya pampu.
“Shida sio pampu Bali tunawaomba wenzetu wa mamlaka ya maji (ZAWA) kutupatia aina ya sampuli ya pampu ambayo inafaa ili tuziweze kuzitafuta na baadae tuweze kuwakabidhi ili maeneo mengine nayo yaweze kupata huduma ya maji safi na salama Kwa masaa 24 Kwa Siku,” alisema Mnyaa.
MBUNGE huyo aliupongeza uongozi wa mamlaka ya maji Kisiwani Pemba pamoja Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Mkoani Kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao.
Nae Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji (ZAWA) Kisiwani Pemba, Omar Mshindo alieleza kuwa jambo alilolifanya Mbunge huyo ni muendelezo wa shughuli zake katika Jimbo Hilo Kwa lengo la kuwatatulia wananchi wake changamoto walizonazo.
Mshindo alifahamisha kuwa huo ni wajibu wake kama Mbunge kushirikiana na wananchi pamoja na Serikali katika kuondoa kero zilizopo ndani ya Jimbo lake.
“Ninamshukuru sana Mbunge Kwa kutupatia pampu hii na naahidi kuwa kuanzia kesho pampu hii tutaifunga hapa kisimani ili wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji,” alieleza Mkurugenzi.
“Mbali ya Kisima hicho lakini pia viko vyengine ambapo navyo vikipata pampu vitaweza kuondosha tatizo la maji katika maeneo yote ya Chokocho na hivyo kuandika historia ya tatizo la maji ndani ya sehemu hii,” alieleza Mshindo.
Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa Kwa upande wa Mamlaka ya maji wamejipanga vizuri Kwa Hilo kwani mabomba yapo Kwa ajili ya Kazi hiyo.
Mapema Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Mkoani Omar Ngwali Dadi aliwataka wananchi kuthamini juhudi za Mbunge huyo Kwa kuitunza pampu hiyo na kuweka ulinzi katika eneo Hilo.
“Tunampongeza Muheshimiwa Mbunge Kwa jitihada zake hizi anazozichukuwa na pia ninawasihi wananchi wenzangu kuyathamini sana tunayofanyiwa na Mbunge, tuitunze pampu yetu hii ili kuweze kufanikisha kila kilichokusudiwa,” alisema Mwenyekiti.
Sambamba na hayo Omar aliwasisitiza wananchi kuthamini sana maendeleo hayo kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi yanayotekelezwa na Mbunge wao.
Nae mwananchi Haji Makame alimshukuru sana Mbunge huyo Kwa juhudi zake binafsi anazozichukuwa kuhakikisha wananchi katika Jimbo lake anawasaidia kutatua changamoto ya maji
Aidha Haji alisema kuwa baada ya ya kufungwa itaweza kuwaondoshea shida ya maji katika katika shehia yao kwani hapo awali huduma ya ilikuwa ikipatikana Kwa mgao.
MWISHO