Thursday, February 27

TAASISI YA TAQWA YAWASAIDIA FUTARI MAYATIMA 2010 PEMBA

MKURUGENZI wa taasisi ya TAQWA Dk, Salha Mohammed Kassim akizungumza na wananchi katika hafla ya kuwakabidhi Chakula watoto mayatima huko katika Skuli ya Msingi Ole, (PICHA NA SAID ABDULRAHMAN PEMBA)

OFISA Mdhamini wa tume na mipango Kisiwani Pemba Khamis Issa Mohammed akizungumza na wananchi Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud wakati wa hafla ya kuwakabidhi Chakula Kwa ajili ya futari iliyotolewa na taasisi ya TAQWA huko katika Skuli ya Msingi Ole,(PICHA NA SAID ABDULRAHMAN PEMBA)

TAASISI ya TAQWA  imekabidhi Msaada wa vyakula wenye thamani ya zaidi ya  Tsh 18 milioni Kwa watoto mayatima wapatao 2010 Kisiwani Pemba Kwa ajili ya futari ya  mwezi mtukufu wa ramadhani.

Vyakula vilivyotolewa ni pamoja na unga wa ngano,mafuta ya kupikia,tende pamoja na sukari.
Akizungumza katika hafla hiyo,Ofisa Mdhamini wa Ofisi ya Rais,tume na mipango Khamis Issa Mohammed Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud alisema kuwa jambo ambalo limefanywa na taasisi hiyo ni la kuigwa na taasisi pamoja na wananchi Kwa ujumla.
Alieleza kuwa suala la kuwapatia Chakula mayatima hao ni suala muhimu na la msingi kwani inawapelekea kujikisikia faraja katika nyonyo zao na kuwaondoshea upweke wa kuondokewa na baba zao.
Aidha Khamis aliutaka uongozi wa taasisi hiyo kuendelea kusaidia mayatima hao kila panapostahiki na Mwenyezimungu atawapa nguvu ili waweze kufanikisha malengo yao.
Sambamba na hayo Ofisa huyo aliwataka wazazi na walezi wa watoto hao kuwalea Kwa busara, hekma na kuzingatia kuwa watoto hao ni mayatima.
“Niwaombe sana wazazi na walezi wa watoto hawa kuwa nao karibu na kuwapatia mambo yote stahiki ikiwa ni pamoja na elimu kwani uyatima wake haujamfanya awe mtu dhalili,” alisema Khamis.
Mapema Ofisa huyo alifahamisha kuwa jambo la sadaka ni la watu wote, hivyo aliwataka wananchi pamoja na taasisi mbali mbali kushirikiana pamoja katika kutekeleza jambo hilo.
“Lakini Kwa kipekee niwaombe Mashekhe wetu waweze kutilia mkazo suala Hili la kutoa sadaka hasa Kwa watoto wetu Hawa mayatima ili na wao waweze kujiona wamo katika jamii,” alieleza Khamis.
Nae Mkurugenzi wa taasisi ya TAQWA Dkt, Salha Mohammed Kassim aliwataka wazazi na walezi kutokubali watoto wao kuwapeleka Katika vituo vya kulelea mayatima.
Alieleza kuwa endapo watoto hao watapelekwa Katika vituo hivyo watakosa mapenzi ya familia zao na hivyo kujiona wao wametelekezwa na familia zao.
“Ninavyowaomba wazazi wenzangu tushirikiane pamoja na tuzidi kuwalea watoto wetu iwe jua, iwe mvua ni vyema tu tuweze kubaki na watoto wetu ili waone upendo wetu,” alifahamisha Dkt, Salha .
Mapema Dkt, Salha alifahamisha kuwa lengo la taasisi yao ni kushughulikia watoto mayatima ambao wanaishi majumbani mwao.

“Kazi kubwa ambayo tunaifanya ni kuwasaidia watoto hao katika nyanja ya elimu, Chakula pamoja afya,” alisema Dkt, Salha.

Sambamba na hayo, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa taasisi yao sio ya Kiserikali Bali imekuwa ikisaidiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake.
Nae Mratibu wa jumuia ya kuhifadhisha kur-ani na kituo Cha mayatima Ile Kianga Sultan Nassor Hamad alieleza kuwa taasisi ya TAQWA imekuwa ikishirikiana na jumuia yao kwa kutoa futari kwa kaya 553 ambapo kaya hizo Zina watoto mayatima zaidi ya 850.
“TAQWA ni taasisi ambayo tumekuwa tukishikiana nayo na imekuwa ikifanya kazi kubwa kwani kila mwaka Huwa wanatoa sadaka kama hii na mwaka huu sadaka hii imeongezeka ukilinganisha na mwaka Jana,” alifahamisha Sultani
“Niwaombe sana wazazi na walezi wa watoto mayatima kufanya usajili ili pale ambapo patatokea sadaka ya aina yeyote ile iwe ni rahisi Kwao kuweza kuwatambua idadi yao lakini pia hata sehemu ambazo wanaishi,” alisema Sultan.
Nao wazazi wa watoto hao Maryam Ali na Fatma Salim walieleza kuwa wamefarajika sana Kupata Msaada huo na kueleza kuwa hiyo sio mara ya kwanza kupata futari hiyo kutoka Kwa jumuia ya TAQWA.
Hata wazazi hao walisema kuwa ingependeza zaidi kupatiwa kupatiwa nguo Kwa watoto wao kwani ndio jambo ambalo linawatatiza hasa katika kipindi hichi Cha kuelekea Skukuu.
             MWISHO