Friday, February 28

‘Udugu wa leo ni kitu’ wameomba kufikishiwa huduma ya maji katika shamba lao.

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA.

WANAKIKUNDI cha watu wenye ulemavu cha ‘Udugu wa leo ni kitu’ kilichopo Vikunguni shehia ya Ng’ambwa Wilaya ya Chake Chake wameomba kufikishiwa huduma ya maji katika shamba lao, ili waweze kuzalisha zaidi.

Walisema kuwa, kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili, waliamua kuanzisha kilimo cha mboga mboga na uatikaji wa miche ya mikaratusi na mivinje kwa lengo la kujipatia kipato kitakachowasaidia kupata fedha za matumizi.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini kwao wanakikundi hao walisema kuwa, kutokana na hali yao ya ulemavu waliyonayo walihitaji watatuliwe changamoto zote kwa vile wameamua kujiajiri wenyewe.

“Tumeanzisha kilimo kwa lengo la kujikomboa na umaskini lakini inafika wakati tunakata tama kutokana na kukabiliwa na changamoto ambazo zinazorotesha shughuli zao za kilimo”, walisema.

Katibu wa kikundi hicho Nassir Suleiman Hamad alisema kuwa, kilimo chao cha mboga mboga kimewapa mafanikio kwa kiasi fulani kwani wanapata fedha za kujikimu, ingawa kipindi cha jua mafanikio ni madogo kutokana na ukosefu wa maji.

“Hali zetu ndio hizi tulizonazo, hatuwezi kufanyakazi vizuri lakini tunajitahidi ili tupate angalau pesa ya chakula, hivyo tunaomba msaada ili tuzalishe kwa wingi, jambo ambalo litasaidia kupata fedha nyingi”, alisema Katibu huyo.

Aidha aliiomba Serikali kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu, kwa sababu kutokana na hali yao hawawezi mizunguko na waliwahi kufuatilia ingawa waliona ni usumbufu kwao.

“Pia tunaiomba Serikali inunue miche kutoka kwetu kwa ajili ya kuwapatia wananchi kama vile wanavyofanya miaka yote, hii watatusaidia sisi kutupa msukumo na hamasa ya kuendelea kuatika miche’’, alieleza.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Anu Juma Hamad alisema, inaweza kufika mwezi maji hayajatoka, jambo ambalo linawarudisha nyuma kwa sababu mazao yao na miche yote hunyauka na hatimae kuwasababishia hasara.

“Tunapofanya shughuli zetu za kilimo tunatumia nguvu na pesa, hivyo ikiwa vipando vitaharibika watakula hasara na hawatafikia lengo la kujikwamua kimaisha’’, alifahamisha Mwenyekiti huyo.

Anu alieleza kuwa, hawana mipira ya kumwagilia maji hali ambayo inawafanya wachote maji kwa mikono, ingawa hawawezi kuacha kwani wanawahudumia watoto wao.

Mjumbe wa kikundi hicho Halima Salum Nassor alieleza kuwa, wanalima, tungule, nyanya, mabilingani, pilipili, kuatika miche ya mivinje na mikaratusi, hivyo wanaiomba Serikali kuwatatulia changamoto zinazowakabi, ili kujikwamua na umasikini.

Kwa upande wake Ofisa Mdhamini Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Ahmed Abubakar Mohamed alisema, Serikali imepanga kuwawezesha wananchi wote kiuchumi ili wajikwamue na umasikini.

“Kuna mipango  kwenye Serikali ya kuwawezesha wakulima wote kwa kuwapatia mikopo, lakini pia watu hawa wenye ulemavu wafike Idara ya watu wenye ulemavu Chake Chake Pemba wakaelezee changamoto zao, baadae Idara itaenda kuwakaguwa na watasaidiwa ikiwa kuna uwezekano wa kusaidiwa, kwa sababu wapo wengi ambao tumeshatatua changamoto zao”, alisema.

Kuhusu changamoto ya maji katika kijiji hicho, Ofisa uhusiano wa Mamlaka ya Maji Pemba (ZAWA) Suleiman Anass Massoud amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo kwa wananchi wa Vikunguni na kusema kuwa jitihada za kuondosha tatizo hilo tayari zimeshafanyika kwani mashine zipo njiani kufika.

Hata hivyo alieleza kuwa, uongozi wa Mamlaka tayari umeshafanya jitihada za kuagizisha mashine nyengine na wanatarajia kupokea mashine 40 ikiwemo ya kisima chao, ingawa kwa kipindi cha mwezi wa Ramadhani walipanga kusambaza maji kwa njia ya magari mpaka pale mashine husika zitakapofika.

MWISHO.