NA ABDI SULEIMAN.
MWAKILISHI wa Jimbo la Wawi Wilaya ya Chake Chake,Bakar Hamad amewataka wananchi wa Jimbo Hilo kushirikiana pamoja katika kuleta maendeleo ndani ya Jimbo lao.
Bakar aliyasema hayo huko katika Ukumbi wa Kiwanda Cha Makonyo Wawi Chake Chake wakati alipokuwa akitoa neno la shukurani Kwa Wananchi waliohudhuria katika dhifa ya futari aliyoiandaa Kwa wananchi wa Jimbo lake.
Mwakilishi huyo aliwataka wananchi hao kuendeleza mshikamano uliopo nchini jambo ambalo litaweza kuleta manufaa Kwa kizazi Cha Sasa na Cha hapo baadae.
Aidha Bakar aliwahakikishia wananchi kuwa atakuwa pamoja nao na kuahidi kuunga mkono juhudi zao katika kuleta maendeleo katika maeneo yao na jimboni Kwa ujumla.
Sambamba na hayo Mwakilishi huyo aliwasisitiza wananchi hao kuendelea kufanya mema katika mwezi huu mtukufu wa ramadhani hasa katika kumi hili la mwisho kwani ni kundi ambalo ndani yake Muna usiku wenye heshima kubwa.
“Ndugu wananchi wenzangu ninalowaombeni kwenu ni kuwatakia Dua nyingi Viongozi wetu wa kitaifa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Hassan Mwinyi ili waweze kuliongoza vyema taifa hili,” alisema Bakar.
Mapema akitoa shukurani Kwa niaba ya wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo Ustadh Iman Mohammed Ali alieleza kuwa kitendo alichokifanya Kiongozi huyo ni Cha kuwapatia swadaka hiyo ni jambo la kupigiwa mfano.
Aidha Ustadh Iman alifahamisha kuwa jambo Hilo ni wajibu wake kwani ameweza kuwaunganisha wananchi wake na kuweza kuwa kitu kimoja.
“Hata wakati wa Mtume Muhammad (S.A.W) zama alipopewa utume alianza kulingania mtu mmoja mmoja mpaka akafikia kuutangaza uislamu Kwa ulimwengu mzima,” alisema Ustadh Iman.
“Bila ya shaka lengo la Muheshimiwa Mwakilishi kutukusanys hapa Siku ya Leo ni Kwa ajili ya futari, kwa upande wake hahitaji chochote kutoka kwetu isipokuwa ni kutaka radhi kutoka Kwa Mola wetu,” alifahamisha Ustadh Iman.
Hata hivyo Imani alifahamisha kuwa jambo la kuftarisha linapaswa kufanywa na kila muumini ambae amepewa Dhamana na ni vizuri kulifanya kwani linaleta upendo katika jamii
MWISHO