Sunday, November 24

RC SALAMA azindua mradi wa ALIVE kwa Mkoa wa Kaskazini Pemba

NA ABDI SULEIMAN.

MKUU wa Mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, amewataka wazazi kuwafunza watoto wao maadili mema, ili waweze kujimbanuwa na kujitambuwa na kujiepusha kujiingiza katika mambo maovu.

Aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Pemba, wakati alipokuwa akizungumza na wazazi, Walimu na maofisa wa Elimu Wilaya na Mkoa huo, mara baada ya kuzindua rasmi mradi wa kuwafundisha watoto stadi za maisha na maadili, afrika Mashariki (ALIVE).

Alieleza kuwa kuwafundisha watoto stadi za maisha ni muhimu sana kwani yanampelekea kuwa kijana bora mwenye kujiamini ,kujitunza na kujitambuwa na kuleta maamuzi yalliosahihi.

Mkuu huyo wa Mkoa alifahamisha kuwa kila kijana ni muhimu katika ushiriki wa mambo mbali mbali ikiwemo malezi , kielimu kwa vile ndio nguvu kazi ya Taifa.

“Katika utafiti uliofanya na taasisi ya Alive wakishirikiana na taasisi ya milele Foundation imebaini kuwa umri wa Vijana kati ya miaka 13 hadi 16 wamekabiliwa na matizo mbali mbali ambayo yanahitaji usimamizi kutoka kwa jamii iliowazunguka”, alisema.

Alisema rika hilo linahitaji usaidizi wa mambo mbali mbali ikiwemo malezi,matunzo kwani ni rika lililo katika mazingira hatarishi kwani linaweza kujiingiza katika mambo maovu kama vile uvutaji wa madawa ya kulevya, wizi nk.

Akizungumzia suala la TEHAMA kwa Wanafunzi aliwasisitiza wazazi kuwafunza elimu hiyo ili waweze kujikombowa kwa kutumia teknolojia hiyo kwani sasa hivi Dunia imebadilika vyenginevyo Dunia itawabadilisha kwa kuachwa nyuma.

Alisema katika kuwafundisha Elimu hiyo wawasimamie na kuwaelekeza kutumia teknolojia hiyo kwa kulinda Mila,silka na Utamaduni wao kwa kutafuta mambo ya kimaisha ikiwemo masomo ambao ndio msingi imara wa maisha yao ya baadae.

RC,Salama aliwataka wazazi kutokuwa na ubaguzi wa Elimu kwa watoto wao kwani ndio kitu muhimu kwa maisha ya mtoto hivyo ni vyema kubadilika kwa kutowa usawa kwa watoto wote.

Aliwataka kila mmoja kuwa tayari kutowa mashirikiano yake katika kuwakombowa Wanafunzi juu ya matumizi ya Tehama na upungufu wa stadi za maisha.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya alisema Ofisi yake itashirikiana na Wadau wengine  ikiwemo wazazi, Walimu ili waweze kuwakombowa Vijana na mambo mbali mbali ikiwemo Elimu na stadi za maisha.

Alieleza kuwa anaipongeza taasisi ya ALiVE kwa utafiti uliofanya ndani ya Wilaya hiyo kwa Vijana wa rika la miaka 13 hadi 16 kwani amejuwa wapi pa kuanzia na kuweka mkazo.

“Nashukuru sana taasisi hii ya Alive kwa utafiti uliofanya kwani umempa nafasi ya kuelewa wapi pa kuanzia katika kuwakombowa Vijana wa Wilaya hiyo”, alisema.

Kwa upande wake meneja upimaji wa Mradi huo wa ALIVE Ramadhani Ali Matimbwa alisema Stadi za maisha ni nyenzo muhimu kwa Vijana katika kupata uelewa wa mambo mbali mbali ya kijamii,kiutamaduni na kimaisha.

Alieleza kuwa lazima wapatiwe Stadi za maisha kwa uzuri zaidi ili waende na kuishi katika mfumo bora wa maisha kwa kuweka mbele tamaduni zao.

“Nawaomba wazazi mushirikiane na taasisi mbali mbali ili Vijana wetu waweze kujifunza maadili mema na ya kujitambuwa “, alisema.

Matimbwa aliwataka Vijana kujifunza sera za mambo mbali mbali ili kuelewa kipi kinafanyika katika nchi yao.

Hata hivyo Ofisa kutoka taasisi ya milele Foundation Fatma Khamis aliwataka Wanafunzi kuvitumia vituo vya TEHAMA vilivyoko katika maeneo mbali mbali ili kupata uelewa wa mambo tafauti tafauti ya maslahi nao sambamba na kujiamini.

. MWISHO.