Thursday, January 2

DC Chake Chake, amani ndio kila kitu zipo nchi zinaitaka baada ya kuipoteza

NA ABDI SULEIMAN.

MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, amesema yapo mataifa mbali mbali duniani yalikuwa na uwezo mkubwa wa kiuchumi, lakini kutokana na amani kutoweka mataifa hayo sasa yameanza kudorora kichumi na huduma nyngine muhimu.

Alisema ipo haja wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba, kuendelea kujifunza kwa mataifa ambayo sasa wananchi wamewanakosa amani ili isije ikatoka nchini.

Mkuu huyo aliyaeleza hayo wakati akifungua mavunzo ya siku mbili kwa wajumbe wa kamati ya amani Kisiwani Pemba, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Amani na Maendeleo kwa Vijana na wanawake unaotekelezwa kwa pamoja na NCA, ZANZIC, ELECT-ND na kufadhiliwa na Ubalozi wa Norway.

Alisema vijana wanapopewa mafunzo ya amani, wakaelewa na kutekeleza basi taifa litakua liko salama, tukiamini kwamba Zanzibar na Tanzania vijana wako zaidi ya 50%.

“Vipo viashiri vya uvunjifu wa amani katika nchini, ni wajibu wetu kuhakikisha tunapigania kutoweka ikiwemo madawa ya kuleva, udhalilishaji, ubakaji, magenge yanapelekea uvunjifu wa amani,”alisema.

Akizungumzia Suala la uchumi, alisema mwelekeo ni kuboresha uchumi hasa kilimo cha mboga mboga, uwepo wa mradi huo utaweza kuunga mkono pale serikali ilipofikia, imani ni kwamba vijana wengi wataweza kujiajiri na sio kukaa barazani.

Hata hivyo alipongeza viongozi wa INTERFEITH Pemba kwa kuja na mradi huo, huku akiwataka viongozi wa dini mbali mbali kushirikiana na kuondosha vitendo vinavyoweza kuharibu amani nchini.

Naye Mratibu wa Interfeath Zanzibar Mchungaji Shukuru Maloda, alisema lengo la mkutano huo ni kujengea uwezo kamati juu ya kusimamia na kurakibisha shuhuli za amani ndani ya Kisiwa cha Pemba, pamoja na kuwakumbusha viongozi wadini nafasi zao.

Alisema Viongozi wa dini wanawajibu mkubwa wa kuendelea kuhakikisha vijana wanasaidia kwa hali na mali, ikizingatiwa wanamchango mkubwa kwa taifa.

Naye mratib wa mradi huo Pemba Dorren Bwogi, alisema katika ujenzi wa mani wanafanya kazi na viongozi wa dini, vikundi mbali mbali vya kijamii, lengo ni kuhamaisha upendo na amani, ili nchi iweze kustawi amani na upendo muhimu sana, wanahamiasisha vijana na jamii waweze kujitambua kuheshimu imani za watu wengine na kujitambua.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa INTERFAITH Pemba Shekhe Yussuf Abdalla, alisema taasisi hiyo ipo kwa ajili ya kusaidia shuhuli za kijamiikupitia wafadhili mbali mbali.

Naye mchungaji Benajamini Kisaga, alisema kamati yao Pemba ina wajumbe 11 na lengo ni kudumisha amani ndani ya kisiwa cha Pemba, pamoja na kuwaunganisha wananchi wote kuwa kitu kimoja bila ya kujali dini.

MWISHO