Sunday, November 24

MWAMBE watakiwa kushirikiana kupambana na vitendo vya udhalilishaji, KUKHAWA

NA SAID ABRAHAMAN, PEMBA.

WANANCHI wa Shehia za Mwambe Wilaya ya Mkoani wametakiwa kushirikiana pamoja katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekithiri katika Shehia hizo.

Hayo yalielezwa na Katibu wa Jumuia ya Maimamu Zanzibar Kisiwani Pemba Yussuf Abdalla Ramadhani wakati alipokuwa akifunga kikao Cha tathimini juu ya vitendo hivyo Kwa Wana Kamati wa Shehia hizo kilichofanyika katika Ofisi za jumuia ya KUKHAWA Chake Chake Pemba.
Alieleza kuwa ipo haja ya Wana jamii ya Muambe kuwa kitu kimoja katika kusimamia maadili ya watoto wao pamoja na kufuatilia Kwa ukaribu nyendo za wao Ili kuona vitendo hivyo vinaondoka kabisa katika jamii yao.

“Ni vyema kudhamiria Kwa makusudi na kuweza kutafuta muarubaini ya matendo hayo, kwani tukiangalia Kwa undani Kuna makundi matatu katika jamii zetu ,kundi la watoto wadogo,kundi la vijana na kundi la wazee,: alieleza Yussuf
Aidha Yussuf alieleza kuwa Kwa mtazamo wa awali ni vyema Wana Kamati kuwatunia vizuri walimu wa Madrasa katika kufanikisha jambo Hilo kwani Bado walimu wa Madrasa Wana nafasi kubwa katika jamii huku wazazi wakishiriki kikamilifu katika jambo Hilo.
“Ni vizuri kwanza kuanza na hili kundi la watoto wadogo kwani Hawa walikuwa wanakuwa na mambo yao, ikiwa tutafanikiwa kundi hili tuende Kwa wafunzi wa Skuli,” alieleza Katibu.
Sambamba na hayo Katibu huyo alitanabahisha kuwa jambo Hilo ni kubwa na ni vyema wakubali kuwa linastahiki ustadi wa Hali ya juu hasa Kwa nyakati za Sasa Kwa sababu mitandao imekuwa ni tatizo kubwa.
Mapema Katibu huyo aliupongeza uongozi wa jumuia ya KUKHAWA Kwa kubuni mbinu ambazo zinafaa katika kukomesha vitendo vya udhalilishaji Kwa Muambe lakini hata ndani ya Kisiwa Cha Pemba.
Akifungua kikao hicho Mratibu wa KUKHAWA Pemba Hafidh Abdi alisema kuwa lengo la kikao hicho ni kupanga mikakati ambayo itaweza kuondoa tatizo lililopo katika Shehia za Muambe.
Hafidh alisema kuwa Kwa upande wa jumuia yao imefanya kazi kubwa katika kutoa elimu ndani Shehia hizo na hivyo ikaona ni vyema Sasa kushirikiana na jamii Kwa kupata msukumo wa kuondosha jambo Hilo.
“Tumeona ni vyema Sasa kurudi katika ili kufanya mambo ya ziada Kwa kubadilishana mawazo yatakayoweza Kujenga taifa letu,” alifahamisha Abdi.
Nae Mratibu wa mradi wa kataa ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto Zulekha Maulid Kheri alieleza kuwa licha ya Wana jamii ya Muambe kuanza kuchukuwa hatua za kukomesha vitendo hivyo lakini Bado juhudi kubwa inatakiwa kufanywa ili kuona vitendo vya udhalilishaji vinamalizika katika shehia yao.
Aidha Zulekha alifahamisha kuwa ni busara zaidi Kwa jamii hiyo kutumia njia za kiimani katika kufanikisha jambo Hilo.
“Kwa Sasa tumedhamiria kuweka Kambi ya wiki moja katika Kijiji Cha Muambe Kwa kuwatafuta Mashekhe mbali mbali ambao wataweza kutoa daawa ya kiroho kila Kona ya Kijiji hicho,” alisema Zulekha.
Nao Wana jamii hao walisema kuwa jambo ambalo wanataka kulianzisha ni kuondoa ngoma nyakati za usiku.
“Hizi ngoma za usiku ni tatizo kubwa kwetu kwani watoto Huwa wanaaga wanakwenda kwenye ngoma lakini hatimae hawafiki huko na kwenda sehemu nyengine ambayo kwao sio salama,” walisema Kamati hiyo
Mbali ya hayo lakini pia waliendelea kusema wataweka msimamo kuona waendesha bodaboda wote ni marufuku kupakia mtoto mdogo bila ridhaa ya wazee wake.
                 MWISHO