Sunday, November 24

WADAU wa Bandari Pemba waomba kupatiwa skana ya kupimia magari ya mizigo na uchungu wa mizigo

NA ABDI SULEIMAN.

WADAU wa Bandari Kisiwani Pemba, wameitaka bodi ya wakurugenzi ya shirika la Bandari Zanzibar, kuhakikisha wanaipatia mashine ya kuchunguzia mizigo mikubwa (Skana) bandari ya Mkoani, ili kuweza kubainika kwa mizigo inayobebwa na magari makubwa yanayowasili bandarini hapo kutoka Unguja au Mkoani Tanga au Tanzania bara.

Wadau hao wamesema kuwa mizigo mingi inayopakiwa ndani ya magari makubwa wanashindwa kuikangua kwa undani, kwani inakuwa imeshapangwa na kupangia au kushusha mzigo mmoja mmoja ni gharama jambo linalotia chagia kutokufanyika kwa kazi vizuri.

Wakichangia maoni yao katika kikao cha pamoja baina ya wadau hao wa bandari na Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya shirika la Bandari Zanzibar, mkutano ulipofanyika katika bandari ya Mkoani Pemba.

“Unajua kuna baadhi ya magari mizigo inatiwa ndani na huwezi kuona kilichomo kwa haraka, uwepo wa mashine hiyo ya kuchunguzia mizigo itatusaidia sisi kubaini hichokitu, ikiwa kikosalama au sio salama,”alisema.

Aidha mmoja ya wadau hao Bakari Juma Haji, alishauri bodi hiyo kutafuta boti maalumu ya uwokozi ndani ya bandari hiyo, ili kusaidia pale panapotokea majanga bandarini hapo.

“Kumekua na matukio mengi yanatokea katika wilaya ya mkoni ya kuzama watu, tukio kama hili linapotokea na boti ipo basi uokozi unafanyika kwa haraka sana,”alisema.

Naye Hassan Matora Hassan alisema wakati umefika kwa wakusanyaji kodi bandarini hapo, kuwa na mfumo mmoja wa kukusanya kodi hizo ili kupunguza usumbufu wakati wautoaji wamizigo bandarini.

“Utakuta magari mengi yamesima wahusika unaambiwa ukitaka kulipa uwende hapa na hapa, lakini kama kungekua na taasisi moja tu inakusanya pesa zote na baadae wanagawana katika vitengo tafauti,”alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nahaat Mohammed Mahfoudh, alisema tayari maandalizi ya kununua mashine kadhaa za kuchunguzia mizigo ndani ya magari kwa unguja na Pemba, ili kupunguza matatizo yanayojitokeza katika bandari hizo.

Kwa upande wa eneo la abiria kujengwa, alisema tayari michoro imeshakamilika kwa ajili ya ujenzi wa eneo hilo, litakalowafanya abiria kupata kupumzika.

Naye Mjumbe wa bodi hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama shirika la Bandari Zanzibar Omar Khamis Ali, alisema ipo haja ya kuwepo kwa chombo maalumu kwa ajili ya bandarini hapo, kwani TPA wanaboti maalumu kwa ajili ya dharira inapotokea.

Kuhusu Skana ya kuchunguzia mizigo, alisema ni jambo zuri kwa ajili ya kuchunguza mizigo bandarini hapo, kwani kuna mizigo inatoka Tanga au Tanzania bara ila ndani hujuwi kuna kitu gani chengine kimewekwa.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya shirika la Bandari Zanzibar Joseph Abdalla Meza, aliwasisitiza wadau hao wa bandari kutoa mashirikiano ya pamoja kwao na viongozi wa bandari, ili kuhakikisha lengo la serikali linafikiwa.

MWISHO