Sunday, November 24

WAKATI NI SASA WA MAGEUZI KULINDA FEDHA ZA UMMA – DKT MWINYI.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kwamba Serikali zote Mbili, ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zitaendelea kuungamkono Shughuli za Ukaguzi wa Ndani, ili kulinusuru Taifa kutokana na vihatarishi dhidi ya Raslimali na Fedha za Umma.

Dokta Mwinyi ameyasema hayo leo kupitia Hotuba yake iliyowasilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, wakati wa Hafla ya kufungua Mkutano wa Pili wa Utawala wa Sekta ya Umma na Ukaguzi wa Ndani, ulioandaliwa na Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA) huko Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini-Magharibi, Unguja.

Amesema, Serikali inalitambua fika jukumu hilo na inathamini mchango muhimu, kutoka kwa Wakaguzi wa Ndani, wa kurutubisha utawala bora katika mashirika ya umma, sekta binafsi, na kwenye uimarishaji wa mazingira ya udhibiti, pamoja na kukabili vihatarishi, ndani ya Sekta ya Umma kwa ujumla.  

Mheshimiwa Dokta Mwinyi amesema kuwa Taasisi za umma, katika ngazi zote, zinatarajiwa kutumikia maslahi ya jamii, ambapo ili kufikia huko, tegemeo kubwa liko kwenye vyombo vya usimamizi, kuja na mikakati bora ya kiuongozi, kutandika mwelekeo sahihi na dira stahiki, pamoja na kufuatilia utekelezaji kwa ajili ya kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Ameongeza kuwa Wakaguzi wa Ndani wanalo jukumu la msingi katika kuhakikisha kwamba taasisi za umma zinaendeshwa kwa umakini, ufanisi na kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa, hasa kwa kubaini maeneo yanayohitaji msukumo zaidi na kutoa mapendekezo.

“Naomba nikuhakikishieni kwamba Serikali zetu zote mbili zitaendelea kukuungeni mkono kwa njia zote zitakazohitajika, katika kustawisha utoaji-huduma wenu kwa Watanzania, kwani tunaelewa pia taasisi za umma katika ngazi zote hutegemea ukaguzi, utekelezaji na usimamizi makini wa huduma za jamii”, amesema Mheshimiwa Dokta Mwinyi, ambaye hotuba yake hiyo imeibua hoja na mifano kadhaa ya ‘madudu’ yanayoibuliwa mara kwa mara katika Ripoti za Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Dokta Mwinyi amefahamisha kuwa utawala bora siyo sera madhubuti na kanuni pekee, bali pia ni pamoja na ufanisi katika ufikishaji huduma na usimamizi maridhawa wa rasilimali za umma, na kwamba huu ndio muda hasa wa kujipanga upya na kuwezesha mageuzi kwenye mwelekeo wa ufikishaji huduma, utakaoinua maisha na amali za watu.

Aidha Dokta Mwinyi ameongeza kwa kusema, “kufuatia msukumo wa jamii uliopo, juu ya kuongeza uwazi wa kiutendaji, uwajibikaji na ufanisi kwenye matumizi ya fedha za umma unaoendelea ndani na nje ya nchi, Kazi za Bodi, Kamati za Utawala, Maafisa Masuuli, Wakaguzi wa Ndani na wadau wengine, nazo zinabadilika pia, ambapo nyenzo zake kuu kama utawala bora kwenye maeneo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia, zimekuwa si ngeni tena nchini mwetu; tumeona athari zake na tunaweza kukadiria jinsi zitakavyoathiri maendeleo ya nchi yetu”.

Pamoja na kueleza ahadi kwamba Serikali zimejidhatiti kuzitatua changamoto zinazowakabili wakaguzi wa ndani, Dokta Mwinyi ameeleza matumaini yaliyopo kwa Mikutano hiyo ambayo maudhui yake yanasisitiza umuhimu wa kujipanga upya na kuziletea mageuzi taasisi za umma na zile za binafsi, ili ziwahudumie wananchi, kwa ufanisi na vizuri zaidi, na kukidhi mahitaji na matarajio ya wananchi yanayozidi kuongezeka, pia kwa kujali maslahi ya wote.

Na katika nasaha zake, huku akiwasihi Wajumbe kujiongeza, kujifunza na kubadilishana mawazo kwaajili ya kujenga ufanisi, Dokta Mwinyi ameongeza kwa kusema, “nakusihini muendelee na juhudi hizi za kupigiwa mfano, nikiwahakikishia uungwaji mkono wa Serikali usioyumba kwenye kazi hii adhimu; kwa pamoja tuna uwezo wa kupiga hatua kubwa kwenye lengo letu shirika, la kuhakikisha utawala madhubuti wa shughuli za kukabili vihatarishi kwenye sekta zote za kiuchumi”.

Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Zanzibar, Bi Fatma Mohamed amesema dhana ya uwajibikaji ni ya umuhimu wa pekee kwa matumizi sahihi ya raslimali za umma, na hilo ni katika mambo ya msingi yaliyokuja kupalilia na kuakisi uanzishaji wa Jukwaa la Wakaguzi wa Ndani ya Nchi, ambayo ni sehemu ya Mkutano huo.

Amebainisha changamoto mbali mbali zinazoendelea kuikabili kada ya Ukaguzi wa Ndani, katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla, zikiwemo kutokuwepo sheria inayosimamia Shughuli za Ukaguzi wa ndani kwa Sekta ya Umma; Uelewa finyu wa kazi za ukaguzi wa ndani kwenye taasisi, hasa katika mnasaba wa matumizi ya teknolojia; na kutokuwepo Muundo wa Kamati za Ukaguzi.

Naye, Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania, Bi Zelia Nyenza, akipongeza juhudi za Serikali katika kuzingatia sasa manufaa ya wakaguzi wa ndani, amebainisha pia kuwa Mikutano hiyo inalenga kutoa fursa kwa wadau kubadilishana mawazo, uzoefu na mbinu bora kabisa za kushughulikia na kuleta mageuzi ya kiutawala kwenye tassisi zote za umma na binafsi, kukaribisha majadiliano ya majopo ya wateule wa fani zinazohusika, hotuba za kutanabahisha na vikao vya kubadilishana fikra, ambavyo hupelekea kutoa maoni na maazimio yanayotekelezeka, sambamba na mbinu na mikakati ya kufikia lengo la pamoja la mageuzi, katika sekta ya umma kwa maslahi ya watu wote.

Wanaojumuika, katika Vikao vya Mkutano huo wa Utawala Bora, ni pamoja na Kamati za Bodi, Wajumbe wa Vitengo vya Uongozi; Wakaguzi wa Nje; Wakaguzi wa Ndani; Wahasibu Wakuu wa baadhi ya Taasisi; Wadau wengine Muhimu wa Maswala ya Utawala kutoka Sekta ya Umma; Mwenyekiti wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika, Bw. Pius Maneno, sambamba na Makatibu Wakuu wa Wizara za Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Ujumbe wa Mkutano huo wa Siku Mbili, unaowajumuisha Wajumbe kutoka Sekta mbali mbali za Ukaguzi, kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ni ‘KUJIPANGA UPYA, MAGEUZI, KWA MASLAHI YA UMMA’.