BAKAR MUSSA-PEMBA.
WAZAZI na walezi wametakiwa kushirikiana na Wizara ya Elimu ili kusimamia maadili ya Vijana wao ili vizazi vilivyopo na vinavyokuja viweze kurithi Utamaduni ili kuondowa mmong’onyoko wa maadili .
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba , Matar Zahor Massoud huko katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Mji wa Chake Chake kisiwani humo wakati akizungumza na wazazi , walezi na wadau mbali mbali wakati akizinduwa ripoti ya utafiti wa Stadi za maisha uliofanywa na taasisi ya ALIVE ikishirikiana na milele Foundation.
Alisema kuwa bila ya kuwepo kwa mashirikiano ya dhati baina ya wazazi na wadau mbali mbali mmong’onyoko wa maadili yataendelea kuporomoka na kuifanya jamii kuishi bila ya kuzingatia stadi zao za maisha na hatimae kupata kizazi kisicho na muelekeo.
Matar alieleza ni vyema kila mmoja atumie tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo ili kupata uelewa wa kasoro zao na kuzipatia ufumbuzi kwa kuzifanyia kazi ipasavyo.
“ Taifa lolote haliwezi kupiga hatuwa kimaendeleo bila ya kuwa na tafiti zilizofanyika ama kufanya wenyewe”, alisema RC.
Aliitaka jamii kuweka mbele uzalendo ili Taifa liweze kwenda mbele kwa maslahi ya vizazi vilivyopo na vinavyokuja kwani inaonekana kwa mujibu wa tafiti hizo kuna mapungufu katika sekta mbali mbali ikiwemo Elimu.
Mkuu huyo wa mkoa wa Kusini Pemba aliiagiza Wizara ya Elimu kijitathmini juu ya kuweka mkazo katika suala zima la ufundishaji kwani kuna changamoto kubwa kwa wanafunzi asilimia 71% wa Wilaya ya Chake Chake na 92%kwa wanafunzi wa Wilaya ya Mkoani hawana ujuzi wa kusoma na stadi za maisha kwa vijana wa miaka 13-17.
Aidha alisema katika utafiti huo uliofanywa na taasisi ya ALIVE kwa vijana wa rika hilo la miaka 13-17 wa kaya 183 za Wilaya ya Mkoani na kaya 173 za Wilaya ya Chake Chake katika maeneo 10 ya Chake Chake na 10 ya Mkoani , asilimia 43% wa Vijana wa Chake Chake na asilimia 59% wa Mkoani hawana ujuzi wa kidijitali na stadi za maisha.
“ Ndugu zangu huu ulimwengu umegubikwa na Utandawazi wa Teknolojia ya Mawasiliano yaani TEHAMA hivyo ikiwa gap ni hili tutafikia wapi huko mbele watachwa nyuma vijana wetu”, alisema.
Mdau kutoka Ofisi ya Elimu Wilaya ya Chake Chake ambae jina lake halikupatikana , alisema Wizara imekuwa kutoka ikiboresha mitaala ili kuongeza kiwango cha Elimu na kukuza maadili ya wanafunzi.
Alieleza kuwa ni vyema sasa Wizara ya Elimu ikaimajiimarisha zaidi kwa ufundishaji wa wanafunzi tokea madarasa ya maandalizi ili wanafanuzi waweze kukuwa kimaadili zaidi.
Aidha aliishauri taasisi ya ALIVE kuwasaidia wanajamii kwenye ufundishaji wa sehemu zote mbili zikiwemo Skuli na madrasa kwa kuwafundisha vijana Stadi za maisha na maadili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa masheha wilaya ya Chake Chake Khamis Iddi Songoro aliwataka wadau wote kila mmoja kutekeleza wajibu wake katika kusimamia maadili kwa vijana kwa kuzingatia mila, silka na tamaduni zao.
Alisema kukosekana usimamizi kwa Vijana kumesababisha kujiingiza katika matendo maovu ambayo hayaendani na maadili , mila , silka na tamaduni zao na hivyo kukiacha kizazi kuendelea kupotea siku hadi siku kwa vile hakina elimu ya kutosha.
Sheha Songoro aliisifu taasisi ya ALIVE kwa kushirikiana na Milele Zanzibar Faundation kwa utaratibu wao walioufanya kwa mara ya kwanza katika tafiti alizowahi kuziana kurejesha mrejesho kwa walengwa ili kuelewa kasoro zao na kuzifanyia kazi.
“ Tokea kufahamu kwangu ni mara ya kwanza kuona taasisi zinafanya utafiti na kuwashirikisha wadau mbali mbali na hatimae kurejesha mrejesho kwa wale walioshirikiana nao, lazima niwapongeze ALIVE”, alisema.
Hata hivyo Mwanafunzi Asha Khamis kutoka Skuli ya Pondeani Sekondari, alisema ni vyema kwa wazazi kutekeleza wajibu wao kwani kuna baadhi ya wazazi wanakwepa majukumu yao hata kuangalia madaftari ya watoto wao muda huo hawana.
Alieleza kutokana na wanafunzi kutofuatiliwa maendeleo yao sio kwa kuhudhuria Skuli au mambo mengine ya Stadi za maisha kuna baadhi hujiingiza katika mambo yasiofaa na kutokufanya vyema kwenye mitihani yao sambamba na kuvunja maadili.
“ Lakini niseme yote kwa yote kuvunja maadili kwa baadhi ya wanafunzi linatokana na tabia ya mwanafunzi mwenyewe”, alifahamisha.
Mkutano huo wa uzinduzi ya tathmini ya stadi za maisha na maadili uliwakutanisha wadau mbali mbali wakiwemo wakuu wa Wilaya , masheha, makatibu Tawala wa Wilaya, maofisa Elimu wa Wilaya na Mkoa , Walimu na baadhi ya wanafunzi .
MWISHO.