Sunday, November 24

Watia nia kugombea nafasi za uongozi washauriwa.

NA ABDI SULEIMAN.

WATIANIA wanawake Ksiwani Pemba, wameshauriwa wakati wa uchaguzi utakapofika kuhakikisha wanarudisha fomu mapema kabla ya siku ya mwisho, ili kama kuna kasoro ziweze kutatuliwa mapena na sio kuwekewa pingamizi na wagombea wenzao.

Ushauri huo umetolewa na afisa kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar upande wa Pemba Shekha Kitwana Sururu, wakati akiwasilisha mada katika mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wanawake 35 wenyedhamira ya kugombea kutoka vyama mbali mbali vya siasa Pemba,

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania,Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na ubolozi wa Norway na kufanyika Kisiwani Pemba.

Afisa huyo aliwataka wanawake hao watia nia kubadilika na kuhakikisha wanafika mapema katika tume ya uchaguzi na kuwasilisha fomu zao.

“Tusifichane humu ndani hebu mmoja hapa aseme kama yeye alikuja mapema, sisi tumeshazowea kuwaona wagombe wanawake ile siku ya mwishi tena baada ya dakika tano ndio wanarudisha fomu, hebu fikirieni kama fomu ina kasoro kweli muda huo tutaweza kusaidiana ndipo siku ya pili unakuta wamewekewa pingamizi,”alisema afisa huyo.

Alisema changamoto kubwa nyengine ni wanawake kushindawa kupewa nafasi ndani ya vyama vyao, wakati wa uchaguzi unapofika huku wengi wao wanatolewa mapema na wengine kuharibiwa fomu zao ndani ya vyama vyao.

Naye Afisa Kutoka Mamlaka ya kuzuwia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) Pemba Kasima Ali Yussuf, alisema wanawake wanapaswa kujiamini sana, wakati wauchaguzi utakapofika kwa kutokufumbia macho masuala ya rushwa.

Alisema wanawake wanashindwa kufikia malengo katika kuingia majimboni kutokana na ukimya wao, pale wanapoona rushwa inatembea.

“ZAECA ipo kisheria zaidi na kuna matukio mengi waliyakamata katika uchaguzi uliopita, na kuyawasilisha katika vyama husika sasatunazeni mapema hapa,”alisema.

Naye Muwezeshaji katika mafunzo hayo Sabahi Mussa Said, alsiema muda upo kwa wanawake watia nia kwenda Tume ya Uchaguzi kupata elimu mbali mbali na sio kusubiri muda wa uchaguzi unapokaribia, ili kuweza kujipanga mapema sasa.

“Hii ni fursa adhimu kwenu kwenda sasa hivi tume ya uchaguzi na sio kusubiri, uchaguzi au kampeni zinakaribia kila kitu kinahitaji kuwekwa sawa muda huu,”alisema.

Naye Mwezeshaji kutoka Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Dkt.Salum Suleiman Ali, alisema wanawake wanayo nguvu ya ushawishi, iwapo watajua namna ya kuitumia kwa kujenga hoja na kuwa karibu na jamii, ili iweze kuwasaidia na kufikia malengo ya kushika nafasi za uongozi bila vikwazo.

Nao baadhi ya washiriki katika mafunzo hayo Asha Mohamed Ali kutoka UDP na Aziza Bakar Said, walisema kila unapofika muda wa uchaguzi baadhi ya wanawake wanarudishwa nyuma na vitisho vinavyotokea kipindi hicho.

MWISHO