Friday, November 15

Waziri  Lela amepiga marufuku matumizi ya upinde wa rangi zinazotuhumiwa kuwa ni alama ya mapenzi ya jinsia moja

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe, Lela Muhamed Mussa, amepiga marufuku matumizi ya upinde wa rangi zinazotuhumiwa kuwa ni alama ya mapenzi ya jinsia moja kwa Skuli zote za Serikali na Binafsi

Akitoa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma za Skuli ya Seeds of Light inayomilikiwa na Taasisi ya Cr Hope Foundation iliyopo Kizimkazi amesema, kufanya hivyo kunakusudia kuondoa hofu kwa jamii kuhusiana na uwepo wa vitendo hivyo ndani ya jamii.

Amesema Wizara imejiridhisha kutokuwepo na vitendo vinavyoashiria tuhuma hizo ndani ya Skuli hiyo baada ya kufanya uchunguzi kuanzia umiliki wa Skuli, vifaa vinavyotumika, taaluma za walimu pamoja na njia wanazotumia katika kufundishia na kuona hakuna dalili ya tuhuma zilizotolewa.

Aidha, Waziri Lela Amefahamisha kuwa, kupitia tume hiyo iliyoshirikisha wadau wa elimu kupitia taasisi mbali mbali iliweza kufanya mahojiano na wanafunzi na wazazi wao ili kupata taarifa sahihi ambapo waligundua kuwepo kwa ukarimu mkubwa kwa wanafunzi na walimu wenye lengo la kuwafanya wanafunzi waweze kusoma vizuri

Mhe, Lela akizungumzia kuhusiana na vifaa vya kufundishia na vya matumizi mengine vilivyokutumika katika Skuli hiyo ikiwemo vitabu na dawa amesema dawa hizo zimefanyiwa uchunguzi na kukutwa vipo salama ambapo baadhi ya vitabu vilichukuliwa na taasisi ya elimu kwa uchunguzi zaidi

Hivyo amewaomba wazazi kuwa makini na kujiridhisha na Skuli wanazowapeleka watoto wao ili kuwalinda na vitendo vitakavyoweza kuwaathiri pamoja na kuwaomba wanajamii kuepuka kuitumia mitandao ya kijamii kwa kutumia habari zinazoweza kuleta taharuki