Wednesday, January 15

IPDO yapanda miti 1,000 Pemba.

 SAID ABRAHMAN-PEMBA.

MKUU wa Wilaya ya Wete Dkt, Hamad Omar Bakar ameungana na wana jumuia ya IPDO ya Kinyasini Wete pamoja na wananchi wa Shehia hiyo na Vitongoji vyake katika uzinduzi wa upandaji miti katika Skuli ya Sekondari Kinyasini.

Akizungumza baada ya zoezi hilo,Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi hao kuilinda miti hiyo ili lengo lake liweze kufikiwa.

Dkt, Hamad alifahamisha kuwa lengo la upandaji miti ni kuhifadhi mazingira, hivyo aliwasisitiza wananchi hao kuendelea kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao ili kuweza kuzuia mmong’onyoko wa ardhi pamoja na kuzuia upepo ili usiweze kuharibu vipando vyao.

Sambamba na hayo aliwataka wananchi  kutoruhusu kufungwa kwa mifugo ya aina yeyote katika shamba hilo na ni vyema kuweka utaratibu mzuri ambao utaweza kutoa adhabu kwa yeyote atakaepatikana na kosa la kufunga mifugo katika eneo hilo.

“Kazi tuliyoifanya ni kazi ya Ibada na malipo yake tutayapa huko tunakokwenda,kubwa ni kujitahidi kuilinda Miche hii,” alisema Dk,Hamad.

Mapema Dkt, Hamad alifurahishwa sana kwa matokeo  mazuri ya mitihani yao ya mwaka jana kwani hapo awali Skuli Sekondari Kinyasini likuwa ni miongoni mwa Skuli ambazo zilikuwa hazifanyi vizuri.

“Ninawapongeza sana walimu wangu kwa juhudi kubwa ambazo mmezichukuwa katika kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika mitihani yao, hii isiwe ndio mwisho bali iwe ni muendelezo wa kupatikana kwa matokeo mazuri katika Skuli yetu,” alisema Dkt, Hamad.

“Na nyinyi wanafunzi mujitahidi sana kwa yale mazuri  ambayo yamefanywa  na waliotutangulia na sisi tuyaendeleze ,” alieleza Dkt, Hamad.

Nae Katibu Tawala Mkoa wa Kaskazini Pemba Ali Bakar Ali aliipongeza Skuli ya Sekondari Kinyasini kwa kuwa ni miongoni mwa Skuli ambazo zimechaguliwa kushiriki katika shindano la kuhifadhi mazingira ambalo limedhaminiwa na Benki ya NMB.

Katibu Ali aliushauri uongozi wa Skuli hiyo kuishughulikia vizuri Miche hiyo na pale ambapo kutakuwa na hitilafu yeyote ni vizuri kuwasiliana na wataalamu wa misitu ili kuweza kupata ushauri mzuri.

“Niwaombe sana walimu na wanafunzi endapo kutatokezea tatizo lolote katika Miche hii musisite kufanya mawasiliano na wataalamu wetu wa misitu ili kuweza kupata maelekezo kutoka kwao,” alisema Katibu Ali.

Nae Ofisa Mdhamini wa Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Pemba Mohammed Nassor Salim alieleza kuwa kitendo walichokifanya wananchi hao cha kupanda miti ni kitendo cha ibada na wamejiwekea fungu kwa Mola wao.

Aliwasisitiza wananchi hao kuitunza Miche hiyo kwa nguvu zao zote ili yale malengo yaliyokusudiwa yaweze kutimia.

“Niipongeze Benki ya NMB kwa kuweza kuweka shindano hili na kuzishirikisha Skuli mbali mbali za Tanzania bara na Zanzibar, lakini pia niseme tu kuwa NMB imekuwa wadau wakubwa katika kusaidia sekta ya elimu hapa nchini,” alisema Ofisa huyo.

Nao wananchi wa Kinyasini  walieleza kuwa changamoto kubwa iliyopo ni wafugaji ambapo waliahidi kwenda nao  sambamba na yeyote ambae atapatikana na hatia ya kufuga mfugo wake katika eneo hilo, watamchukulia hatuwa.

Aidha wananchi hao wametoa tahadhari kwa mtu yeyote ni marufuku kukata mti wa Skuli bila ya ridhaa ya uongozi wa Skuli hiyo.

“Kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu yeyote kukata miti ya Skuli na atakayepatina hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” walisema wananchi hao.

Katika hafla ya uzinduzi huo jumla ya miti 1000 iliweza kupandwa na wananchi hao.

 

MWISHO.