Monday, November 25

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI

HOTUBA YA MHESHIMIWA DK HUSSEIN MWINYI, RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI KATIKA HOTELI YA GOLDEN TULIP ZANZIBAR

TAREHE 03 MEI, 2023

Mheshimiwa Nape Moses Nnauye;

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,

 

Mheshimiwa Tabia Maulid Mwita;

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,

 

Mheshimiwa Mhandisi Andrew Kundo;

Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,

 

Mheshimiwa Idrisa Kitwana Mustafa;

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,

 

Ndugu Mohammed Khamis Abdulla;

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,

Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,

 

Ndugu Fatma Hamad Rajab;

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,

Vijana, Utamaduni na Michezo,

 

Ndugu Selestine Kakele;

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,

Mawasilinao na Tekenolojia ya Habari,

 

Ndugu Rose Reuben;

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa

Habari Wanawake Tanzania TAMWA,

 

 

 

 

 

 

Dkt. Zlatan Milisic, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa,

 

 

Profesa Hubert Gijzen;

Mkurugenzi wa UNESCO Kanda ya Afrika Mashariki,

 

Ndugu Michel Toto; Mwakilishi wa UNESCO Ofisi Kuu

 

Ndugu Gerson Msigwa;

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na

Msemaji Mkuu wa Serikali,

 

Viongozi wote wa Serikali na Taasisi za Habari Tanzania,

 

Ndugu Wahariri na Waandishi wa Habari

kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa Ujumla,

 

Viongozi wa Vyama vya Siasa,

 

Viongozi wa Dini,

 

Wageni Waalikwa,

 

Mabibi na Mabwana

Assalam Alaikum

Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uhai na afya njema na kutuwezesha kukutana hapa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani. Natumia fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Shirika la UNESCO pamoja na Uongozi wa Chama cha Waandishi Wanawake TAMWA kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho haya.

 

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Nimefurahi kusikia kuwa Maadhimisho haya ya miaka 30 ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayofanyika hapa Zanzibar kwa mara ya kwanza, yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali kupitia Idara ya Habari MAELEZO  na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Umoja wa Mataifa, washirika wa maendeleo, waandishi wa habari na vyombo vya habari vya mtandaoni na nje ya mtandao. Vile vile, kuna mchango wa mashirika ya kiraia na watetezi wa haki za binaadamu, watafiti, wasomi na wadau mbali mbali wa habari.

 

Nakupongezeni kwa kubuni kauli mbiu ya Maadhimisho isemayo “Kuunda Mustakabali wa Haki” Kauli mbiu hii inahimiza uhuru wa kujieleza kama kichocheo cha haki nyingine zote za binadamu. Kwa muktadha huo, lengo la maadhimisho haya ni kulinda uhuru wa vyombo vya habari duniani ambapo Serikali zinapata nafasi ya kukutana na wadau wote kwa madhumuni ya kujadili uhusiano, na muingiliano wa mabadiliko ya utendaji kazi, usawa wa kijinsia ndani na nje ya vyombo vya habari pamoja na usalama wa waandishi wa habari.

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Natambua kuwa mada mbali mbali zimejadiliwa katika matukio na mikutano ya makundi tofauti. Kumefanyika maonyesho ambapo pamoja

 

 

na mambo mengine yameonyesha bidhaa za maarifa, michoro na ubunifu katika vyombo vya habari, utafiti, mabadiliko ya kidijitali na uhuru wa kisanii. Nimefurahi kusikia kuwa hafla ya kutoa tuzo kwa wanahabari na washirika wenye mchango mkubwa katika sekta ya habari imefanyika kwa lengo la kutambua jitihada zao katika kuiendeleza tasnia hii ya habari. Kutokana na shughuli mbali mbali zilizofanyika, inadhihirisha kuwa maadhimisho haya ni jukwaa muhimu katika kuibua changamoto za kisera pamoja na  kuangalia namna bora ya uboreshaji wa mazingira ya uendeshaji wa vyombo vya habari katika nchi.

 

Kwa hakika Serikali zetu zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinathamini na kuheshimu sana uhuru wa vyombo vya habari. Uhuru huo umeendelea kukua siku hadi siku kwa pande zote mbili za Tanzania. Taarifa kutoka Idara ya Habari – MAELEZO kwa upande wa Tanzania bara zinaonesha kuwepo kwa magazeti 312 yaliyosajiliwa nchini hadi tarehe 20 Februari, mwaka huu 2023 ambapo baada ya Uhuru wa Tanganyika, kulikuwa na magezeti 10 tu. Vile vile, kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hadi mwezi Februari, 2023 jumla ya Redio 218, Televisheni 68, Redio za kimtandao 8, Televisheni za mtandao 391, blog na majukwaa 73 na cable operators 53 zimesajiliwa Tanzania Bara ambapo taarifa za baada ya uhuru zinaonyesha tulikuwa na Kituo kimoja cha Redio cha Tanganyika. Halikadhalika, hakukuwa na kituo cha Televisheni hata kimoja, blogs wala majukwaa ya mtandaoni.

 

 

Kwa upande wa Zanzibar, vile vile  kumekuwa na kasi kubwa ya usajili mpya wa vyombo vya habari hasa vya kielektroniki kupitia Tume ya Utangazaji. Takwimu za tume hiyo zinaonesha kuwa jumla ya TV 21 za kawaida na 38 za mitandaoni zimesajiliwa. Aidha, jumla ya Radio 27 zikiwemo za masafa ya FM na za jamii zimesajiliwa. Kwa mujibu wa Tume ya Utangazaji Zanzibar ongezeko kubwa la usajili wa vyombo vya habari limeonekana zaidi kati ya mwaka 2020 hadi 2023. Tumeona na wenzetu Tanzania Bara nao wamefanya vizuri katika eneo hili.

 

Kwa upande mwengine, Idara ya Habari Maelezo Zanzibar nayo imekuwa ikiendelea na usajili wa majarida na magazeti. Takwimu zinaonesha kuwa magazeti na majarida 71 yamesajiliwa kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2023. Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Shirika la Magazeti ya Serikali ni vyombo vya habari vya Serikali ambavyo navyo vimekuwa vikifanya kazi kubwa za kutoa taarifa kwa umma.

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa idadi ya vyombo vya habari nchini kumechangiwa zaidi na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano. Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa Sheria, Kanuni na Taratibu zetu ndizo zinaruhusu uanzishwaji wa vyombo hivi. Bila ya shaka, wingi wa vyombo vya habari  unaongeza uhuru wa kujieleza na uhuru wa kusambaza habari.

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Katika kufanikisha utoaji wa habari kwa umma kupitia mitandao ya kijamii, tunaipongeza Serikali  ya Jamhuri ya Muungano kwa kufanya marekebisho ya Kanuni za Utangazaji na kupunguza tozo zilizokuwa zinalipwa na watoa huduma za mitandao ya maudhui mbali mbali nchini zikiwemo blogs, redio za mtandaoni na televisheni za mtandaoni. Hatua hizi zilizochukuliwa na Serikali zinalenga kukuza dhana ya uhuru wa vyombo vya habari na kutanua wigo wa utoaji na usambazaji wa habari nchini. Hii ni kuonesha dhamira njema ya Serikali katika kupanua uhuru wa vyombo vya habari ambazo ni miongoni mwa haki zinazotambuliwa katika Katiba zetu.

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Katika kujenga mazingira mazuri ya utoaji na upatikanaji wa habari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza kufanya mapito ya Sheria zilizokuwa zikilalamikiwa na wadau mbali mbali wa habari ndani na nje ya nchi yetu ikiwemo Sheria ya huduma za Habari Na. 12 ya 2016. Marekebisho ya Sheria hii yamesomwa kwa mara ya kwanza kupitia muswada wa marekebisho ya sheria mbali mbali katika mkutano wa Bunge la 12, mwezi Februari,2023. Mchakato wa marekebisho ya sheria hii utakapo malizika na kuanza kutumika, inatarajiwa kwamba itaweka mazingira  mazuri na rafiki ya ufanyaji kazi wa vyombo vya habari na wanataaluma.

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Kuhusu sheria ya Habari kwa upande wa Zanzibar Serikali tayari imeshaandaa mswada wa sheria hiyo ambao madhumuni yake ni kufuta Sheria iliyopo ya Usajili wa Magazeti, Wakala wa Habari na vitabu nam.5 ya mwaka 1988 na marekebisho yake nam.8 ya mwaka 1997 na kutunga Sheria mpya ya Huduma za Habari na Mambo yanayohusiana na hayo.

 

Mswada huo hivi sasa uko katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na ni matarajio yetu kwamba tutakuwa na sheria nzuri sana inayohusiana na masuala ya habari.

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Tanzania inatambua na kuthamini jukumu kubwa la vyombo vya habari pamoja na mchango wao katika maendeleo ya taifa letu. Kupitia vyombo vya habari, wananchi wameweza kupata taarifa kuhusu shughuli na mipango ya Serikali, na kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli na mipingo hiyo. Aidha, kupitia vyombo vya habari, imekuwa ni rahisi kutoa elimu kwa wananchi, siyo tu elimu kitaaluma lakini pia elimu ya uzalishaji na ujasiriamali. Muhimu zaidi, vyombo vyetu vya habari vimechangia sana katika kulinda na kudumisha

 

 

amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Aidha, vyombo vya habari vimekuwa na nafasi kubwa katika kuitangaza nchi yetu pamoja na kuijengea taswira chanya kimataifa.

 

Napenda nipongeze jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na vyombo vya habari katika kufichua vitendo viovu ambavyo katika kipindi cha nyuma vilikuwa haviripotiwi. Vitendo hivi ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino. Kadhalika, mila potofu za kuwaficha watoto wenye ulemavu. Ufichuaji wa vitendo vya aina hii umechangia kwa sehemu kubwa katika kuchukua hatua za kisheria na hatimaye kuvikomesha kabisa na kujenga jamii iliyo bora. Zaidi ya yote kwa sisi wanasiasa, vyombo vya habari vimekuwa vikitusaidia sana katika kuwaeleza wananchi kuhusu sera na mitazamo yetu kuhusu Tanzania tunayotaka kuijenga, na kuwahimiza wananchi kushiriki katika michakato ya kisiasa na chaguzi na hivyo kukuza demokrasia nchini. Hivyo, nitumie hadhara hii kuwashukuru na kuwapongeza wanahabari wote wa Tanzania Bara na Zanzibar kwa mchango wenu mkubwa katika ujenzi wa Taifa letu.

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Ni matumaini yangu kuwa vyombo vya habari vinaweza kutoa mchango ulio bora zaidi endapo nyinyi waandishi wa habari mtazingatia uzalendo, weledi na maadili ya taaluma yenu. Kinyume chake, tasnia yenu inaweza kufifisha jitihada za maendeleo na hata kuhatarisha amani, umoja na

 

mshikamano wa kitaifa. Nyinyi ni mashihidi wa madhara makubwa ambayo baadhi ya nchi hapa Duniani zimekumbana nayo baada ya waandishi wa habari kushindwa kufuata misingi ya taaluma yao na kuingia kwenye propaganda za kichochezi ambazo zimekuwa chanzo cha machafuko. Kwa mantiki hiyo, pamoja na kwamba leo tunaadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, lazima tutambue kuwa hakuna uhuru usio na mipaka, wala hakuna uhuru bila wajibu. Hivyo tunapoadhimisha siku hii, tutambue pia umuhimu wa kuwa na uzalendo wa nchi yetu.

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Nimefurahi kuona jitihada zinafanywa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo  katika kukuza uhuru wa vyombo vya habari. Ninawapongeza sana viongozi wa Wizara hizi mbili  kwa jitihada zenu katika kutekeleza majukumu yenu. Ninawasihi muendelee katika mwelekeo huo lakini msiache kuvisimamia vyombo vya habari ili vitekeleze majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea.

 

Natambua kuwa masuala mengi mmeshayajadili katika majopo yenu mbali mbali kwa siku mbili mlizokuwepo hapa. Hata hivyo, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, naomba nitoe wito kama ifuatavyo:

 

  • Kwanza, Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani itumike kama fursa ya kuweka mkazo mkubwa katika uhuru wa kujieleza ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binaadamu.

 

  • Pili, siku hii itumike kuandaa hafla zinazoangazia uhusiano kati ya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na haki zingine.

 

  • Tatu, siku hii ishirikishe wahusika wote kwa madhumuni ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari, kuimarisha uhuru wa kujieleza, na kuweka mazingatio kwamba haki za binaadamu ni kitovu cha kufanya maamuzi katika ngazi ya kimataifa, kikanda na kitaifa.

 

  • Nne, tuadhimishe siku hii kwa kutimiza ahadi zilizotolewa na kila nchi Mwanachama wa Umoja wa Mataifa ili kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

 

  • Tano, jumuiya na wadau mbali mbali wa uhuru wa vyombo vya habari watumie siku hii kusherehekea kwa kuungana na mashirika yanayotangaza masuala ya mazingira, haki za wanawake, haki za watoto, haki za kiasili, haki za kidijitali, vita dhidi ya ufisadi na mengineyo.

 

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanahabari,

Namalizia hotuba yangu kwa kutoa shukrani zangu tena kwa kupata mwaliko wa kuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho haya ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka huu wa 2023. Natoa shukurani kwa  Shirika la UNESCO kwa kuendelea kuwa mfadhili kiongozi katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani bila  kuchoka. Serikali zote mbili za Tanzania zinawaahidi ushirikiano wa kutosha katika kukuza teknolojia ya kidijitali ili kuharakisha maendeleo.

 

Baada ya kusema hayo, nakutakieni nyote kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yenu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu Amani, Umoja na mshikamano.

 

Mungu Ibariki Afrika

Mungu Ibariki Tanzania

Asanteni kwa kunisikiliza