Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed ameitaka kampuni ya CRJE Tanzania iliopewa kazi ya kujenga kituo cha mabasi katika eneo la kijangwani kuhakikisha wanazingatia viwango na kukamilisha mradi huo ndani ya wakati uliopangwa.
Waziri Dk. Khalid ametoa agizo hilo wakati aliposhiriki na kushuhudia zoezi la utiaji saini wa ujenzi wa kituo hicho hafla iliofanyika katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo.
Zoezi la utiaji saini kwa upande wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) imewakilishwa na Mkurugenzi Muendeshaji wa Mfuko huo ndugu Nassor Shaaban Ameir na kwa upande wa Kampuni ya CRJE imewakilishwa na meneja wao XU CHANG.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la utiaji saini Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed ameupongeza uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) kwa uthubutu pamoja na ubunifu wao wa kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha, Mhe. Waziri ameutaka uongozi wa ZSSF kuhakikisha wanasimamia kwa karibu ujenzi wa kituo hicho kwa kuteua mshauri elekezi ataekasimamia kwa upande wa Serikali na kuhakikisha ujenzi huo unakamilishwa kwa viwango vinavotakiwa.
Pamoja na mambo mengine Waziri Dk. Khalid amesema ZSSF inakwenda kurejesha historia kwa kukijenga kituo cha mabasi katika eneo hilo kwani mnamo miaka ya 1970 eneo hilo lilikua likitumiwa kwa shughuli kama hizo.
Pia, Mhe. Waziri amepongeza ushirikiano mzuri ulitolewa na askari wa UMAWA kwa kukubali kupisha ujenzi wa kituo hicho na kuhamishia Afisi zao katika eneo jengine lililotolewa na Serikali.
Nae Mkurugenzi Muendeshaji wa mfuko wa Hifadhi ya Jamii Ndugu Nassor Shaaban Ameir amesema ZSSF imeamua kujikita katika ujenzi wa vituo vitatu vya mabasi kwa hatua ya awali lengo likiwa ni kutatua changamoto na kuwaondoshea usumbufu wananchi katika huduma ya usafiri.
Amebainisha vituo hivyo vitajengwa katika eneo la Kijangwani, Malindi pamoja na katika eneo la Mnazi mmoja huku wakisogeza huduma ya ujenzi wa vituo hivyo nje ya mji kulingana na uhitaji.
Vile vile Mkurugenzi Nassor amemuomba Mhe. Waziri kupitia wizara anayoisimamia kuziagiza mamlaka za usafiri pamoja na mabaraza ya manispaa na mabaraza ya miji kuanza kutunga kanuni na kuandaa utaratibu wa kutumika kwa vituo hivyo mara vitakapokamilika.
Kwa upande wake Meneja wa kampuni ya CRJE Tanzania XU CHANG ameeleza kwamba, kampuni yao itahakikisha inajenga kituo hicho katika ubora unaotakiwa na kumaliza kwa wakati uliopangwa ambapo wanakusudia kuingiza vifaa vya ujenzi vya kisasa katika kutekeleza kazi hiyo ya ujenzi.
Ujenzi wa Kituo hicho unatarajiwa kugharimu jumla ya Shilling Billlioni nane milioni mia sita nasabiini, laki nne na arubaini na tisa mia tatu ishirini na moja nukata mbili moja (8,670,449,321.21) na kinakadiriwa kuwa na maduka sabiini na nane (78), sehemu za kupata huduma kutolea fedha sita, sehemu za kutoa huduma za chakula tano pamoja na huduma za vyoo ambapo ujenzi wake utachukua miezi kumi (10) hadi kukamilika kwake.