Thursday, January 9

Wakati umefika wa sampuli za maradhi mbali mbali sasa kuchunguzwa Pemba baada ya kupelekwa Tanzania Bara-WAZIRI Mazrui

NA ABDI SULEIMAN.

 

WAZIRI wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, amewataka watalamu wa maabara kuzitunza maabara za kisasa zinazozinduliwa na kuvithamini vifaa vinavyowekwa, na kuboresha miundombinu iliyomo ili iweze kuinufaisha jamii ya Zanzibar na Tanzania.

 

Alisema Vifaa hivyo vimeweza kugharimu fedha nyingi, hivyo vinapaswa kuheshimiwa ili jamii iweze kunufaika hasa pale yanapotokea maradhi mbali mbali na kuweza kuchunguzwa.

 

“Sote leo mashahidi tupo hapa kwa ajili ya makabidhiano na uzinduzi wa maabara ya kisasa, maabara hii imegharimu Bilioni 3.5, niwashukuru American Rescue Plan Act of 2021 (ARPA), unaotekelezwa na shirika la Management and Development for Health (MDH) na UNICEF chini ya ufadhili wa CDC katika kuanzisha maabara mpya ya molekuli za baiolojia”alisema.

 

Waziri Mazrui aliyaeleza hayo huko katika maabara ya afya ya jamii Wawi Chake Chake Pemba, wakati wa hafla ya makabidhiano ya maabara ya kisasa ya kuchakata Molekuli za biolojia.

 

Aidha Waziri huyo alihimiza kuimarishwa kwa maabara za afya ya jamii kwa kuimarisha shughuli za uchunguzi na utafiti wa afya jamii ili kuongeza uelewa na utayari wakati wa milipuko ya maradhi inapotokea.

Alisema Serikali itahakikisha inaendelea kufanya kazi na wadau wa maendeleo katika kuboresha huduma za afya, ambapo wakati umefika wa sampuli za maradhi mbali mbali sasa kuchunguzwa Pemba baada ya kupelekwa Tanzania Bara.

Alisema msaada huo muhimu utasaidia kufanya shughuli za uchunguzi wa maradhi, yanayotishia jamii ya wananchi wa Pemba na Unguja kwa ujumla, kwani mfano mwengine wa jinsi misaada ya kifedha na kiufundi ya CDC invyosaidia kutekeleza hatua mabalimabli za afya ya jamii Zanzibar, katika uzuiaji na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza

Alifahamisha kwamba asilimia 40 ya mapato ya Zanzibar yanategemea utalii, kwa nchi kama hii ni muhimu kuwa na mifumo ya afya inayostahimili milipuko ya magonjwa, na yenye ufanisi katika kugundua na kukabiliana na dalili za awali za magonjwa ya mlipuko.

“Ni moja ya somo tulillojifunza kutoka na mlipuko wa UVIKO-19, ni kwamba hakuna mtu ulimwenguni aliye salama hadi kila mtu atakapokuwa salama,”alisema.

Hata hivyo alisema Wizara ya Afya Zanzibar imefurahi kupokea huduma mpya iliyoanzishwa katika Maabara ya Afya ya jamii Pemba, ambayo sasa ina uwezo wa kuchunguza maambukizi mapya na kufanya ufuatiliaji wa magonjwa yenye umuhimu wa afya ya jamii, kwa kutumia Next Generation Sequencing (NGS) ambayo ndiyo njia ya kisasa zaidi inayotumika duniani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alisema lengo la uwepo wa maabara hiyo ya kisasa ya uchunguzi wa maradhi mbali mbali Pemba, inakwenda sambamba na adhma ya Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi ya kuimarisha huduma za afya nchini.

Alisema sasa wananchi watajenga imani na serikali yao katika utoaji wa huduma bora Unguja na Pemba, kwani huduma zitakazotolewa zitakua bora zaidi na sasa basi kusafirishwa kupelekwa Unguja au Dar kwa ajili ya Uchunguzi.

“Niwaombeni waandishi wa habari hakikisheni jamii inafahamu kila kitu kinachofanyika hapa, hii ni maabara itakayoweza kuchunguza maradhi yote munayoyajua, kwa Tanzania hii ni ya pili na tunafahamu sote kama tiba ni gharama na serikali inajitahidi,”alisema.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr.Amour Suleiman Mohamed, alisema maabara hiyo imekuja kuondosha changamoto zilizokua zikijitokeza wakati wa mripuko wa COVID 19, sampuli zilikua zikichukua siku mbili tano hadi wiki kupatikana kwa majibu yake.

“Nilikua naumizwa na sampuli za COVIDI 19 Pemba, zikusanywe siku nzima halafu jioni zisafirishe, wakati mwengine mgonjwa anakufa hatujuwi tunafanya nini, uwekezaji huu unatufanya kutembea kifua mbele, tuwashukuru CDC na MDH kwa msaada wao,”alisema.

Aidha alifahamisha kwamba maabara hiyo ikitumika vizuri itaondosha tatizo la kusubiria majibu ya sampuli za magonjwa muda mrefu, sasa ndani ya saa 24 majibu yanapatikana ndani ya kisiwa cha Pemba.

Hata hivyo aliwataka wataalamu  nchini kuitumia maabara hiyo ipasavyo kwa ajili ya kuchunguzia maradhi mbali mbali ya mripuko na kuiweka Zanzibar salama ikizingatiwa watalii wanaofika kwanza wanahoji suala la afya.

Aidha kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MDH Dr.David Sando, alisema MDH inafanya kazi katika kuboresha utoaji wa huduma ya magonjwa yanayoambukiza na yasioambikiza, pamoja na kusaidia huduma za kinamama.

Alisema Tanzania MDH imesaidia vitu vya Uchunguzi katika maabara mbali mbali kwa lengo la kufanya uchunguzi wa magonjwa ya mripuko na yasio ya mripuko ambayo hujitokeza na kuathiri jamii iliyokubwa.

Alifahamisha kwamba kuanzishwa kwa maabara hiyo Zanzibar ni muhimu katika kuboresha upatikanaji wa vipimo vya UVIKO 19, na kusaidia kuimarika kwa uwezo wa ufuatiaji, kupunguza muda wa kusubiria na kuimarika kwa maandalizi na kinga ya magonjwa ya mripuko.

Aliseam Zanzibar inawakaazi Milioni 1.8 na zaidi ya watalii 390,000 wanatembelea visiwani humo kila mwaka na suala la kwanza kwa wageni wanaulizia huduma za afya.

Aidha alisema MDH inasaidia huduma na matengenezo ya vifaa vya usalama wa Viumbe na kununua vifaa vya kupima maabara kwa ajili ya kujilinda na magonjwa ya mripuko kama ebelo, MonkeyPox, Homa ya Manjano na vimelea vyengine.

“Msaada huo unajumuisha kuimarisha shughuli za ufuatiliaji na uwezo wa uchunguzi kupitia ITF, CARES na ufadhili wa ARPA, sasa shuhuli zote za ufuatiliaji na utoaji wa majibu zitafanyika ndani ya maabara hii ya sasa na hata COVID 19 tunaweza kupima hapa na kupata majibu,”alisema.

Mapema Afisa Mtendaji Mkuu Maabara ya Afya ya Jamii Wawi Pemba Dr.Said Mohamed Ali, alisema lengo la Maabara hiyo ya kisasa ni kusaidia SMZ katika utambuzi wa maradhi ndani na nje ya nchi.

Aidha aliwataka wananchi kufahamu kuwa, hali ya maradhi haitambuliki, hivyo lazima kila mmoja kuwa salama muda wake na kuhakikisha anachunguza afya yake ipasavyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za kinga Wizara ya Afya Zanzibar Dk.Salim N. Slim, alisema uwepo wa vifaa hivyo vitaimarisha sekta ya utalii Zanzibar, kwani watalii wengi wanaokuja wanaangalia kwanza suala la afya liko vipi nchini.

 

MWISHO