NA ABDI SULEIMAN.
MKUU wa Wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, amesema ndani ya Wilaya yake anakusudia kubuni vyanzo vipya vya utalii, ikiwemo utalii wa kiislamu ambao unaonekana ni mpya na haujaibuliwa.
Mkuu huyo alisema wilaya hiyo imejaaliwa kuwa na vivutio hivyo vingi, ambavyo inaonekana havijajulikana na vinawezekana kuvutia wageni wengi na wenyeji kutembelea.
Aliyaeleza hayo katika kikao baina ya wajumbe wa kamati ya Utalii Wilaya ya Mkoani na Maafisa kutoka Kamisheni ya Utalii Pemba, juu ya kuimarisha utendaji wa kazi wa kamati hiyo.
Alisema utalii wa uislamu ndio unaokubalika ndani ya Kisiwa cha Pemba, kwani kimejaaliwa kuwa na miskiti mingi mikongwe na kisiwa cha Misali moja ya kisiwa kinachotajwa sana.
“Wapo watu wanaokwenda uarabuni kuangalia misikiti na wageni wengi wanaokwenda kufujifunza mambo mengi, wanalipa fedha kubwa za kigeni,”alisema.
Aidha aliwatakata wajumbe wa kamati hiyo, kuvifahamua vivutio vyote vya utalii vyote vilivyomo ndani ya Wilaya ya Mkoani na kuanza kuviubua.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema sekta ya utalii inachangia fedha za kigeni kwa kiasi kikubwa ndani ya Nchi, hivyo anatamani siku moja Mkoani iweze kuwa kama Wilaya za Unguja kiutalii.
“Tumejaaliwa kua na bandari hii kubwa, melo kubwa za kiutalii lazima zipitie bandari yetu na wageni wake, sasa hapa ni fursa kwetu kuanza kujipanga kwa kufanya vitu mbali mbali vya kiutalii wageni wakiondoka waweze kununua,”alifahamisha.
Mapema afisa mipango Kamisheni ya Utalii Pemba Mohamed Ali Juma, alisema sera ya Utalii inasema suala la mazingira lazima liwe endelevu, ili kila mtu kunufaika na mazingira na utalii wake.
“Wageni wengi wanapokuja pia wapo wanaongalia suala la mazingira ya sehemu yakoje, ikiwa mazingira mabaya basi hawataweza kufanya kazi na mazingira mazuri ndio rafiki kwao,”alisema.
Nae Afani Othman Juma alisema ipo haja kwa wajumbe wa kamati ya Utalii Wilaya ya Mkoani, kuandaliwa safari ya kuvitembelea vivutio vyote vya utalii vilivyomo ndani ya Wilaya hiyo na kuanza kuvifahamu.
Hata hivyo aliitaka Kamisheni ya Utalii Pemba, kuhakikisha kuitaarifu kamati ya Utalii ya Wilaya hiyo kwa kila kitakachofanyika ndani ya Wilaya, ili nao waweze kufahamu na sio kuwashtukizia.
Kwa upande wake kaimu Afisa Utamaduni Wilaya ya Mkoani Fatma Hamad Salum, alisema maadili kwa asilimia kubwa yanavunja na wageni wanaokuja, hivyo wazazi wanapaswa kuwadhibiti vijana wao ili kutokuiga mila na silka za kimagharibi.
Afisa Utalii kutoka Wizara ya Utalii Pemba Khalid Kombo, alisema kamati ya Utalii Wilaya ya Mkoani, lazima iwe na mpango kazi wake ambao utawaonyesha shuhuli zao wanazizifanya na watakazo zifanya.
Mapema Afisa Utalii Kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba Sadi Saim Ali, alisema kamati hizo zimejaaliwa kua na majukumu mengi ambayo yanapaswa kutekelezwa, ikiwemo kulinda, kukuza na kuendeleza Utamaduni wa kiasili wa mzanzibari.
MWISHO