NA ABDI SULEIMAN.
WAJUMBE wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), wamesema uwepo wa maji mengi katika kisima cha maji Junguni, Jimbo la Gando Wilaya ya Wete, nikutokana na kutokuharibu mazingira yao kwa ukataji wa miti.
Wamesema hali ya mazingira eneo lililopo kisima hicho ni mazuri na yakuvutia, hali inayofanya upatikanaji wa maji kuwa mkubwa tafauti na maeneo mengine.
Hayo yameelezwa na mmoja ya wajumbe wa bodi hiyo Mohamed Aboud Mohamed, wakati akitoa nasaha zake kwa wananchi wa shehia hiyo, mara baada ya kukagua kisima hicho kilichojengwa kwa fedha za UVIKO 19, wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi hiyo Pemba.
Alisema wananchi wa Junguni wameheshimu mazingira kwa kiasi kikubwa, hali inayoonyesha maeneo mengi ya shehia yao yana maji ya kutosha.
“Tujitahidi kuendelea kutunza na kuhifadhi mazingira yetu yaliotunzunguka, leo sote tunaona faida yake, majiyanavyotoka kwa wingi wenyewe munaseme yanafika sehemu kubwa na munataka sasa mashine kuzimwa ili ipumzishwe,”alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka hiyo Zanzibar, Balozi Mstaafu Meja Jenerani mstaafu Issa Suleiman Nassor, aliwashuhukuru wananchi wa junguni kwa juhudi zao kulinda na kuheshimu miundombinu hiyo ya maji ambayo muda mrefu wakiihitaji.
Alisema serikali inatumia fedha nyingi katika uwekeaji wa miundombinu ya maji, Visima vipo kila sehemu lengo ni kuondosha tatizo la maji na kuwapunguzia mzigo akinamama na watoto kufuata huduma ya maji masafa marefu.
“Sote ni mashaihidi wanawake ndio watafutaji wamaji wakubwa, hata muda wa usiku au alfajiri unaweza kumkuta anahangaikia maji ndani ya nyuma yake ili watu wawesalama,”alisema.
Hivyo aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanakuwa walinzi wazuri na walindaji wa miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma bora kwao.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa ZAWA Zanzibar Dr.Salha Mohamed Kasim, alisema hiyo ni hatua moja kubwa walioanza katika kuwaondoshea shida ya maji wananchi wa junguni, kwani bado wanaendelea kujenga visima vya ziada.
Alisema tatizo la maji ni kubwa ila wanajitahidi kuziondosha changamaoto zinazojitokeza ili kuona wananchi wote wananufaika na huduma hiyo ya maji.
Mapema akitoa maelezo kwa wajumbe wa bodi, Mkurugenzi wa ZAWA Tawi la Pemba Omar Mshindo Bakari, alisema ujenzi wa kisima hicho umetokana na fedha za UVIKO 19, ambapo kwa sasa kisima hicho kinauwezo wakuzalisha lita elfu 50 kwa saa limoja.
“Kwa sasa vile vijiji ambavyo huduma ya maji ilikua haifiki sasa inafika, yote ni kutokana na juhudi za serikali yetu ya mapinduzi katika kuwapatia huduma ya maji wananchi, mikakati yetu ni kupeleka maji njau kutoka junguni,”alisema.
Kwa upande wake Mwananchi wa Junguni Ali Suleiman Ali, aliwaomba wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ZAWA, kuwajengea tangi la kuhifadhi maji ili kuweza kuipumzisha mashine yao ambayo imekua ikifanyakazi masaa 24 bila kupumzika.
Naye Massoud Ismail Juma aliishukuru SMZ na ZAWA, kwa kuhakikisha wananchi wajunguni wananufaika na huduma ya maji safi na salama, kwani hawakutegemea kama Ramadhani wataimaliza salama usalimini kwa tatizo la maji.
Jumla ya Visima 27 za vyaji safi na salama vimechimbwa Kisiwani Pemba kupitia fedha za UVIKO 19, Mkoa wa Kaskazini Pemba una visima 10 na Kusini Pemba ina visima 17 na matangi matano ya kuhifadhia maji Pemba.
MWISHO