Friday, November 15

Walimu wa Vikundi vya Kijaluba iSAVE Zanzibar watakiwa kusaidia kukuza uwezo wa watu wenye ulemavu Kiuchumi

 

Walimu wa vikundi wakijifunza kwa vitendo namna ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kushiriki katika vikundi vya kuweka na kukopa hisa bila vikwazo kulingana na hali za ulemavu wao.
Afisa mradi wa Kijaluba iSAVE Zanzibar kutoka TAMWA Zanzibar, Mohamed Salim Khamis akitoa mafunzo kwa walimu wa vikundi na wawakilishi wa jumuiya za watu wenye ulemavu.

KATIKA kuhakikisha lengo la kushughulikia vikwazo vinavyowarudisha nyuma watu wenye ulemavu kiuchumi katika jamii Zanzibar, walimu wa vikundi na wawakilishi wa jumuiya za watu wenye ulemavu wametakiwa kufanya kazi kwa ukaribu na watu hao kupitia vikundi vya hisa ili kuwawezesha kujiinua kiuchumi.

Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo maalum kwa walimu wa vikundi na wawakilishi wa Jumuiya za watu wenye Ulemavu yaliyolenga kuwajengea uwezo namna ya kuendesha vikundi na kufahamu mbinu za kuwezesha kubadili mitazamo hasi ya jamii kwa watu wenye ulemavu kujiingiza katika shughuli za kujipatia kipato kupitia vikundi vya hisa.

Katika mafunzo hayo ambayo ni utekelezaji mradi wa Kijaluba iSAVE Zanzibar unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Shirikisho la Jumuiya za watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) na Chama cha Watu wenye Ulemavu Nchini Norway (NAD) yamewashirikisha jumla ya walimu na wawakilishi wa jumuiya za watu wenye ulemavu 28 (saba Pemba na 21 Unguja).

Imeelezwa kuwa kwa muda mrefu watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa elimu ya masuala ya kifedha kulingana na hali zao jambo ambalo linawafanya kushindwa kushughulikia vikwazo vyao katika jamii.

Afisa mradi huo kutoka TAMWA Zanzibar, Mohamed Salim Khamis alisema mradi unatumia walimu na wawakilishi wa jumuiya za watu wenye ulemavu kutoka katika shehia kwa lengo la kusaidia ufikishaji wa elimu ya vikundi vya kuweka na kukopa kwa walengwa ili kuwa na matokeo ya haraka ya kuwainua watu wenye ulemavu kiuchumi kupitia vikundi hivyo.

Alieleza ili vikwazo vya watu wenye ulemavu viweze kushughulikwa, ni lazima walimu na wawakilishi hao kutambua na kutumia mfumo stahiki wa uendeshaji wa vikundi vya hisa kwa watu wenye ulemavu ili waweze kushiriki kikamilifu katika hatua zote muhimu za uwekaji wa hisa.

Alifahamisha kwamba mradi umeandaa mwongozo maalum wa utekelezaji katika kusimamia uendeshaji wa vikundi vya hisa kwa lengo la kuongeza ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli za kiuchumi kwenye jamii.

“Katika kufikia lengo letu la kuongeza ujumuishi unaolenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi, mradi umeandaa mwongozo ambao unaweka mazingira rafiki ya kukuza uwezo wa watu wenye ulemavu kiuchumi kwa kujenga mitazamo chanya juu ya ushiriki wao na kujiingiza katika shughuli za kujipatia kipato kupitia vikundi vya kuweka na kukopa,” alisema afisa huyo.

Alihimiza ili malengo hayo yaweze kufikiwa ni lazima walimu na wawakilishi wa jumuiya za watu wenye ulemavu kutumia mwongozo huo kusimamia na kuwaelimisha watu hao umuhimu wa ushiriki wao katika shughuli za kujipatia kipato bila kujali hali za ulemavu wao.

Kwa upande wake Fatma Abrahman ambaye ni mwalimu wa vikundi aliwataka walimu kushughulikia changamoto za watu wenye ulemavu bila kukata tamaa kulingana na hali za ulemavu wao ili kusaidia kujenga mitazamo chanya ya ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

“Walimu wa vikundi tunatakiwa tusikubali kushindwa na kukata tamaa katika kuwasimamia watu wenye ulemavu. Tuwaongoze kutokana na uhalisia na utaalamu wetu ili tuwasaidie kufikia maelengo na kuwawezesha watu kiuchumi kupitia vikundi vya hisa,” Fatma Abrahman.

Nae Is-haka Mahmoud kutoka wilaya ya Kusini Unguja alieleza mafunzo hayo yataongeza uwajibikaji kwa walimu wa vikundi na kuchochea mwamko kwa watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za kujiingizia kipato kupitia vikundi vya kuweka na kukopa na kuondoa hali ya utegemezi ambayo watu hao wengi wanakabiliana nayo kwenye jamii.

Alisema, “kujua majukumu na wajibu wangu mimi kama mwalimu wa kikundi inarahisisha sana utendaji kazi wangu na kufikia malengo ya mradi wa Kijaluba, pamoja na mafunzo ya kuendesha kikundi ambayo yatasaidia kubadili mitazamo ya jamii katika kanda yangu juu ya watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za kiuchumi jambo ambalo kwa muda mrefu linasababisha watu hao kukosa haki zao.”

Mradi wa Kijaluba iSAVE Zanzibar ni mradi jumuishi unaotekelezwa Zanzibar na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na SHIJUWAZA na Chama cha Watu wenye ulemavu nchini Norway (NAD) katika wilaya mbili za Chake chake kwa upande wa Pemba na Kusini kwa Unguja ukiwa na lengo la kuwezesha watu wenye ulemavu na kuwajengea uwezo kuhusu mitazamo chanya ya ushiriki katika shughuli za kujipatia kipato kupitia vikundi vya kuweka na kukopa.