Thursday, November 14

NCA yawahimiza vijana katika suala la utunzaji wa Amani

NA ABDI SULEIMAN.

 

AFISA Uchechemuzi na mawasiliano kutoka shirika la NCA Nizar Selemani Utanga, alisema NCA limekua mastari wambele katika kuhakikisha vijana wanahamasika katika suala zima la utunzaji wa amani nchini.

 

Alisema msafara wa vijana kuhamaisha amani na utengemano wa jamii kupitia kauli mbiu yake “Amani Yetu, Kesho Yangu”, unawaleta pamoja mabalozi wa amani, vijana, vikundi vidogo za fedha, wanaume, wanawake, vijana, taasisi za , dini , viongozi wa dini, viongozi wa serikali, vyombo vya habari na asasi za kiraia kutoka Pemba.

Msafara huu wa amani ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Amani na Utengamani wa Kijamii-Zanzibar na Tanzania Bara, unaotekelezwa na Norwegian Church Aid, ZANZIC/ KKKT DMP na Ofisi ya Mufti Zanzibar kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.

Afisa uchachemuzi Nizar aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, Kisiwani Pemba wakati wa ziara ya msafara huo kwa wilaya mbali mbali za Pemba.

Aidha alisema malengo ya msafara huo ni kuona Viongozi wa Dini na Vijana waliowezesha wameimarisha mashikamano wa kijamii na amani endelevu kwao.

Alisema vijana walijipanga kikamilifu ili kukuza amani na uwiano wa kijamii, ushirikishwaji katika Nyanja za kitaifa na kikanda, kuhamasisha wanawake na vijana kujiunga na kilimo kinachostahamili mabadiliko tabianchi ilikuweza kuondokana kwenye kundi la umasikini.

Alifahamisha kwamba ili kukuza uelewa zaidi na kuthamini amani na mshikamano wa kijamii, NCA na watendaji wa imani wataendeleza kazi nzuri ya kamati za dini mbalimbali, mabalozi wa amani wa vijana, wazalishaji wa kilimo kwa kubadilishana mbinu bora na hadithi za mafanikio kupitia mashairi, kaswida, hadithi za mabadiliko ya hati kutoka kwa walengwa.

Alisema mpango huo unachangia ukamilishaji wa mpango endelevu SGD, hakuna umaskini, Usalama wa Chakula na Lishe, Ubora wa afya na ustawi, Ajira stahiki na Maisha bora, Kupambania usawa, Ujenzi wa taasisi imara yenye Amani na usawa.

Kwa upande wa Vipaombele vya NCA nchini Tanzania, ni Usawa wa Kijamii, Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia, Kuimarisha taasisi za kidini, huduma za afya endelevu inazotolewa na asasi za kidini.

Naye mjumbe kutoka kamati ya Viongozi wa dini Haji Mussa Khatib, alisema lengo la kamati hiyo ni kuhamasisha amani nchini, na kuona Zanzibar inarudi katika hali yake ya amani.

Alisema hivi sasa kuna mataifa mbali mbali yanakuja kujifunza Zanzibar kutokana na uwepo wa amani nchini, hali hiyo imetokana na michango ya viongozi wa kamati ya amani zanzibar.

MWISHO