Thursday, November 14

Tatizo la mgao wa maji Zanzibar linatarajiwa kuwa historia.

NA ABDI SULEIMAN.

MWENYEKITI wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Balozi Mstaafu na Meja jenerali Mstaafu Issa Suleiman Nassor, amesema baada kukamilika kwa miradi ya Maji Uviko 19 tatizo la mgao wa maji nchini linatarajiwa kuwa historia.

Alisema miradi hiyo uchimbaji wa Visima vipya 38 na ujenzi wa matangi ya maji 10, ambapo kukamilika kwake kutaweza kuliondosha kabisa tataizo la mgao wa maji nchini.

Mwenyekiti huyo aliyaeleza hayo mara baada ya kuamiza ziara ya kutembelea miradi hiyo ya maji ya Uviko 19 Kisiwani Pemba, ili kuona imefikiwa hatua gani.

Alisema kwa sasa wananchi wanapaswa kukaa katika hali nzuri na kusubiri mabadiliko makubwa katika sekta ya maji, hivyo aliwasihi wananchi kuwa makini katika matumizi ya maji kwa kuacha upotevu wa maji kiholela.

Aidha alisema malengo waliojiwekea ni kuona tataizo la maji linaondoka nchini, hivyo miradi hiyo kukamilika kwake itakua mkombozi mkubwa wakuliondosha tataizo hilo.

“Julai 10 mwaka huu miradi hii ya Uviko 19 inatakiwa tukabidhiwe hakuna kuongeza muda kwa sasa, wakandarasi muelewe mapema tusije tukaonana wabaya,”alisema.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Dr.Salha Mohamed Kassim, alisema kwa sasa visima vipo katika hatua za mwisho kukamilika, hayo ni mafanikio makubwa kwetu kuona maji yanapatikana masaa 24 bila ya kukatika.

Alisema mradi mzima wa maji kupitia fedha za UVIKO 19 ni shilingi Bilioni 34.2, lengo la wananchi ni kupata maji licha ya Miundombinu ya maji kutokua rafiki ya mwanzo.

“Bado wananchi wanahitaji huduma ya maji ipasavyo kukamilika miundombinu hii, tatizo la maji litakua limeshaondoka kabisa,”alisema.

Akizungumzia suala la matangi alisema yapo asilimia 95%, ambapo madhumuni makubwa ni kutatua tatizo la maji Unguja na Pemba, kwa sasa miradi hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo.

Kwa upande wao wananchi waliopitiwa na miradi hiyo, wamepongeza ZAWA kwa juhudi kubwa waliozifanya kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana.

Aidha waliomba kujengewa matangi kwenye visima vya maji ili kuweza kuzipumzisha mashine zinazosukumia maji, kwa lengo la kuepuka kuungua.

MWISHO