Sunday, December 29

VAR aliyependekeza VIN kupewa kadi nyekundu afutwa kazi

Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF) limewafuta kazi Waamuzi 6 wa VAR akiwemo Mwamuzi Ignacio Iglesias Villanueva ambaye alipendekeza Vinicius Junior kutolewa kwa kadi nyekundu katika mechi ya Valencia dhidi ya Real Madrid

Kwa mujibu wa vyombo vya Habari Nchini Uhispania, Shirikisho hilo halikufurahishwa na utendaji kazi wa Villanueva ambaye inadaiwa aliondoa picha iliyokuwa ikionesha mchezaji wa Valencia Hugo Duro akimkaba koo Vini Jr kwa nyuma.

Villanueva alimwita mwamuzi wa kati, Ricardo de Burgos Bengoetxea kujiridhisha kwenye skrini ya VAR lakini VAR ilionyesha kipande kilichoonesha Vini Jr akimpiga Hugo usoni pekee huku kipande ambacho Duro akimkaba Vini Jr kwa nyuma kikiwa hakipo. Baada ya kujiridhisha Mwamuzi wa kati alitoa kadi nyekundu.

Licha ya kuandamwa na kauli za matusi na ubaguzi wa rangi kwa kipindi chote cha mchezo Vinicius Junior alioneshwa kadi nyekundu lakini Duro ambaye alianzisha uchokozi aliendelea kusalia uwanjani.

Vinicius Junior alikejeli kwa kupiga makofi baada ya uamuzi wa mwamuzi na baadae alirudia ishara iliyofanywa na Hugo Duro ya kukabwa kwa nyuma na kuhoji ukweli kwamba Duro hakuadhibiwa katika dimba la Mestalla ambapo Real Madrid ilipoteza 1-0 dhidi ya wenyeji Valencia siku ya Jumapili.