Thursday, November 14

Wizara ya afya yatoa maelekezo kwa waandishi wa habari Kisiwani Pemba.

NA ABDI SULEIMAN.

WAANDISHI wa Habari Kisiwani Pemba, wametakiwa kuendelea kuhamasisha na kuelimisha jamii, kuhusu umuhimu wa huduma za chanjo katika kukinga magonjwa yanayozuilika kwa chanjo na kuepusha vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kupatia Chanjo.

Hayo yameelezwa na Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali, wakati alipokua akifungua mkutano wa tathmini ya Chanjo mwaka 2022, kwa waandishi wa habari kutoka Vyombo mbali mbali vya habari Pemba na kufanyika Mjini Chake Chake.

Alisema ni wakati sasa kuwahimiza wanafamilia kuwapeleka watoto wote wanaostahiki kupata chanjo, katika vituo vya afya vya serikali na binafsi vinavyotolewa chanjo, ili watoto wanastahiki wapatiwe chanjo kwa wakati.

Aidha alisema lengo la kuu ni kuwahamasisha na kuelimisha jamii, juu ya umuhimu wa huduma za chanjo katika kuokoa maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Alisema chanjo ni mkakati muwafaka katika kutokomeza magonjwa na kupunguza vifo vya watoto, kwa lengo la kupunguza agharama kubwa ambazo familia zetu na taifa kwa ujumla ingetumia katika kutibu maradhi ya yanayozuilika na chanjo.

“Chanjo zimethibitishwa kuzuia takribani vifo Milioni mbili (2,000,000) hadi Milioni tatu (3,000,000)kila mwaka kutokana na maradhi yanayozuilika kwa chanjo duniani,”alisema.

Alisema WHO limethibitisha usalama wa chanjo hizo, mikakati mbali mbali huchukuliwa na Wizara ya Afya, hivyo chanjo ni gharama kubwa na mtu binafsi kugharamia ni ngumu.

Hata hivyo alisema nchi imefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa nduwi, kwani jukumu la SMZ ni kuona upatikanaji wa chanjo, ambapo serikali ya awamu ya 8 kwa kushirikiana na mashirika ya chanjo kuona chanjo zinapatikana nchini.

Mdhamini huyo alisema bado kuna changamoto kwa mabinti wa miaka 14 ambao hawapati au kukamilisha chanjo ya Mlango wa Kizazi, sambamba na kuwapeleka watoto kukamilisha chanjo zao.

Nae Mkurugenzi Mkuu kitengo cha Chanjo Zanzibar Abdull-himid Ameir Salehe, aliwataka waandishi kuhakikisha elimu inawafikia wananchi kwa wakati, ili jamii kupata uwelewa wa kutosha juu ya suala la chanjo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Wizara ya Afya ya Tanzania LOtalis Gadau, alisema chanjo ni gharama kubwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano inanunua chanjo Bilioni 30, mbali ya chanjo zinazotolewa na mashirika hisani.

Aliwasihi wazazi kuhakikisha wanawakamilishia chanjo watoto wao, kwani chanjo zinasaidia katika kuwakinga na magonjwa mbali mbali ikiwemo yalioambukiza.

Mratibu wa Chanjo Pemba Bakar Hamad Bakar, alisema lengo la kikao hicho ni tathmini ya chanjo zilizotolewa mwaka jana 2022, ili kuongaliwa wapi hawakufanikia ili 2023 waweze kufanikiwa kwa asilimi 100.

MWISHO