Sunday, November 24

Elimu ya msaada wa kisheria kufika maeneo yenye mazingira magumu.

NA ABDI SULEIMAN.

WADAU wa Msaada wa Kisheria Kisiwani Pemba, wamesema kuelekea Wiki ya Msaada wa Kisheria mwaka 2023, wanapaswa kujikita zaidi kutembelea maeneo yenye mazingira magumu na kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wananchi.

Wamesema baadhi ya maenneo ya mjini tayari wananchi wanajuwa umuhimu wa watoa msaada wa kisheria, lakini bado baadhi ya vijijini wananchi wanakosa hata haki zao kutokana na kutokua na elimu hiyo.

Wadau hao wametoa maoni hayo katika kikao cha kujadili maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria 2023, kikao kilichochayika Gombani nje kidogo ya Mji wa Chake Chake.

Akichangia katika mkutano huo Hakimu wa Mkoa Abdalla Yahya Shamuuni, alisema wakati umefika wa kubadilisha maeneo ya kutoa elimu ya msaada wa kisheria, kwa kufika kwenye maeneo ambayo wananchi waliowengi elimu ya maada hawana.

Alisema kufika huko kutaweza pia kuwatambulisha wasaidizi wa msaada wa kisheria ambao wapo Pemba na kutoa elimu kwa wananchi, kwani bado baadhi ya maeneo wananchi wanakosa elimu hiyo.

“Tutafanya jambo kubwa sana, kuna baadhi ya maeneo hapa Pemba wananchi wake hawajuwi lolote kuhusu masuala ya sheria sisi tutakua wa kwanza kutoa elimu kwao,”alisema Hakimu Abdalla.

Nae Mwanasheria kutoka Kamisheni ya Wakfu Pemba Masoud Ali Masoud, alisema kambi inapaswa kuwa sehemu tafautitafauti na sio eneo moja kama inavyofanyika miaka iliyopita.

“tukifanya sehemu tafauti wananchi wengi watapata elimu, elimu itakua mkombizi kwao na wengine elimu itasawaidia na kujuwa wapi haki zao wazipate,”alisema.

Mapema Afisa Mdhamini Wizara ya Ncho Ofisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi na utawala wa Umme Pemba Halima Khamis Ali, alisema lengo la wiki ya Msaada wa kisheria ni kuifikia jamii na kuipatia elimu mbali mbali juu ya masuala ya haki zao.

Alisema wananchi wengi wahawa elimu ya msaada wa kisheria, wapo wanaohitaji mawakili, wasaidizi wa kisheria ili kutatua changamoto zinazowakabili.

“Kila mmoja kama atashuhulika kwa nafasi yake, migogoro mbali mbali iliyoko kwa jamii itapata kuondokana, watapataka kujua haki zao na wapi wazifutae,”alisema.

Aidha aliwataka wadau hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa pamoja, ili kuona mafanikio makubwa yanapatikana kupitia wasaidizi wa sheria waliopo kisiwani Pemba.

Kwa upande wake afisa Sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Unguja Ali Haji Hassan, alisema lengo la kujadili wiki ya Msaada wa kisheria Zanzibar, ni kuona wadau mbali mbali wanashiriki kikamilifu katika wiki hiyo.

Alisema wiki hiyo inaratibiwa na Wizara kupitia Idara ya katiba na msaada wa kisheria Zanzibar, hivyo watahakikisha wanazifikia shehia zote 388 za Unguja na Pemba.

Nae afisa sheria kutoa idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Pemba Bakari Omar Ali, alisema maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria ni moja ya njia ya ufikishaji wa utoaji huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wasiokua na uwezo na wenye mahitaji maalumu.

Kauli mbiu ya Wiki ya Msaada wakisheria mwaka 2023 ni “Mazingira wezeshi kwa watoa msaada wa kisheria ni daraja la upatikanaji haki”

MWISHO