Thursday, January 9

MAKALA: MAABARA ya Afya ya Jamii Pemba kuwekwa vifaa vipya, vinaweza kutambua sababu za magonjwa mengi.

     

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

“HAKUNA haja sasa ya kwenda Tanzania bara kupeleka vipimo, kwani vifaa vilivyofungwa hapa Maabara ya Afya Jamii Wawi, vina uwezo mkubwa,’’anaeleza waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui.

Anaeleza kuwa, zipo baadhi ya sampuni ambazo zilitarajiwa kufanyiwa uchunguuzi ndani ya maabara hiyo, ingawa hapo awali ilishindikana kwa kutokuwepo mashine zenye uwezo.

Hili lilionekana kuwavutia wananchi hasa waliosikia maneno hayo kutoka kinywani kwa Waziri huyo, ambapo ilikuwa ni kwenye hafla ya uzinduzi wa huduma hizo.

Shughuli iliyofanyika papo hapo Maabara ya Afya ya Jamii, iliyopo Wawi Wilaya ya Chake chake mkoa wa kusini Pemba.

Muda ukafika sasa wa kwenda kukagua vyumba vya maabara ya kisasa ya kuchakata molekuli za baiolojia, iliyomo ndani ya maabara hiyo na hapo sasa kuthibitisha msemo wa Waziri.

Kila mmoja aliweza kuacha mdomo wazi, na hapo maeneo ya chini chini, yakaanza kutoka, kufuatia kuonekena na kutolewa maelezo juu ya umuhimu wa vifaa vilivyomo ndani ya maabara hiyo.

“Hapa sasa, tunaweza kupima sampuli za maradhi mbali mbali ikiwemo hata Uviko 19, na kupata majibu hapa hapa ndani ya saa 24, na hatuna haja ya kusafirisha kwenda Tanzania bara, kama ilivyokuwa zamani,’’anasema Mtaalamu wa maabara Ghanil Mohamed Khatib.

Anasema mashine hizo zimekuja wakati muwafaka, kipindi cha uwepo wa ugonjwa wa Uviko 19, maana walikua na kazi kubwa katika usafirishaji wa sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa washukiwa wa ugonjwa huo, kukusanywa na baadae kusafirishwa hadi Tanzani bara.

Muda ukafika wa shughuli husika kuanza ya uzinduzi na makabidhiano ya maabara ya kisasa ya kuchakata molekuli za baiolojia.

WIZARA YA AFYA

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, anasema baada ya kusafirisha na kupelekwa Tanzania bara, sasa kila kitu kitakua kinafanyika hapa hapa Pemba na majibu kupatikana.

‘’Uwepo wa vifaa hivi ni utekelezaji wa dhamira na maono ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika kuimarisha sekta ya afya nchini, na kutoa huduma bora kwa wananchi wake.

Niwazi wataalamu wetu wa maabara hii ya jamii, kuzitunza maabara hii ya kisasa na kuvithamini vifaa vilivyowekwa, viweze kudumu kwa muda mrefu.

“Sote tunaona miundombinu iliyopo ni miziru na ya kisasa zaidi, niwakati wetu kuimarisha miundombinu iliyomo, ili iweze kuinufaisha jamii ya Zanzibar na Tanzania,” anasema Waziri.

Vifaa vilivyomo vimegharimu fedha nyingi, hivyo vinapaswa kuheshimiwa ili jamii, iweze kunufaika hasa pale yanapotokea maradhi mbali mbali na kuweza kuchunguzwa.

“Sote leo ni mashahidi, tupo hapa leo kwa ajili ya makabidhiano na uzinduzi wa maabara ya kisasa, maabara hii imegharimu shilingi bilioni 3.5,’’anasema Waziri.

Hapa aliwashukuru sana American Rescue Plan Act of 2021 (ARPA), mradi unaotekelezwa na shirika la Management and Development for Health (MDH) na UNICEF chini ya ufadhili wa U.S CDC katika kuanzisha maabara mpya ya molekuli za baiolojia,” amesema.

Akasema Serikali, itahakikisha inaendelea kufanya kazi na wadau wa maendeleo, katika kuimarisha huduma za afya, ambapo wakati umefika, wa sampuli za maradhi mbali mbali sasa kuchunguzwa Pemba.

Anona huu ni msaada muhimu na utasaidia kufanya shughuli za uchunguzi wa maradhi, yanayotishia jamii ya wananchi wa Pemba na Unguja kwa ujumla.

Kwa mfano mwengine jinsi misaada ya kifedha na kiufundi ya U.S  CDC, invyosaidia kutekeleza hatua, mabali mabli za afya ya jamii Zanzibar, katika uzuiaji na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza

Sote tunafahamu asilimia 40 ya mapato ya Zanzibar yanategemea utalii, kwa nchi kama hii, ni muhimu kuwa na mifumo ya afya, inayostahamili milipuko ya magonjwa, na yenye ufanisi katika kugundua na kukabiliana na dalili za awali za magonjwa ya mlipuko.

Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dk. Amour Suleiman Mohamed, anasema maabara hiyo imekuja kuondosha changamoto zilizokua zikijitokeza wakati wa mripuko wa magonjwa kama ya COVID 19.

Mana anasema, hapo kabla ya ujio wa mashine hizo za kisasa kwenye maabara hiyo, sampuli zilikua zikichukua kati ya siku tano hadi saba kupatikana kwa majibu yake.

“Nilikua naumizwa na sampuli mfano za COVIDI 19 Pemba, zinakusanywa siku nzima, halafu jioni zisafirishwe, wakati mwengine mgonjwa anakufa, hatujuwi tunafanya nini, uwekezaji huu unatufanya kutembea kifua mbele,’’anaeleza.

Maabara hii ikitumika vizuri itaondosha tatizo la kusubiri majibu ya sampuli za magonjwa muda mrefu, sasa ndani ya saa 24 majibu yanapatikana ndani ya kisiwa cha Pemba.

Kwake anaona ni wakati sasa kwa wataalamu nchini, kuitumia maabara hiyo, ipasavyo kwa ajili ya kuchunguzia maradhi mbali mbali ya mripuko, na kuiweka Zanzibar salama, ikizingatiwa watalii wanaofika kwanza wanahoji suala la afya.

Nae Mkurugenzi wa Huduma za kinga Wizara ya Afya Zanzibar Dk. Salim N. Slimi, amesema uwepo wa vifaa hivyo vitaimarisha sekta ya utalii Zanzibar, kwani watalii wengi wanaokuja wanaangalia kwanza suala la afya liko vipi nchini.

MKUU WA MKOA

Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema lengo la uwepo wa maabara hii ya kisasa, ya uchunguzi wa maradhi mbali mbali Pemba, inakwenda sambamba na azma ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi ya kuimarisha huduma za afya nchini.

Mattar anasema sasa wananchi watajenga imani na serikali yao, katika utoaji wa huduma bora Unguja na Pemba, kwani huduma zitakazotolewa zitakua bora zaidi.

Anaona sasa mwisho wa kusafirisha vipimo na sampuli kwenda Tanzani bara imefika mwisho, baada ya maabara hiyo kuimarishwa kwa huduma za kisasa za uchunguuzi wa maradhi mbali mbali.

Hapa akavigeukia vyombo vya habari, kuvitaka kutumia juhudi na nguvu zao mbali mbali, ili kuwatangaazia wananchi, juu ya uwepo wa maabara hiyo na mashine zake za kisasa.

SHIRIKA LA MANAGEMENT AND DEVELOPMENT FOR HEALTH (MDH)

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika ya ‘MDH’ Dk. David Sando, amesema ‘MDH’ inafanya kazi katika kuimarisha utoaji wa huduma ya magonjwa yanayoambukiza na yasioambikiza, pamoja na kusaidia huduma za kinamama.

Anasema ‘MDH’ Tanzania, imesaidia vitu vya uchunguzi katika maabara mbali mbali, kwa lengo la kufanya uchunguzi wa magonjwa ya mripuko, na yasio ya mripuko ambayo hujitokeza na kuathiri jamii iliyokubwa.

“Kuanzishwa kwa maabara hii hapa Zanzibar yenye vifaa vya kisasa, ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa vipimo vya kama ya UVIKO19, na kusaidia kuimarika kwa uwezo wa ufuatiaji, kupunguza muda wa kusubiria na kuimarika kwa maandalizi na kinga ya magonjwa ya mripuko,”anasema.

Anasema Zanzibar inaowakaazi milioni 1.8 na zaidi ya watalii 390,000 wanatembelea visiwani humo kila mwaka na suala la kwanza kwa wageni wanaulizia huduma za afya.

Anafikiria kuwa hawa wote ikiwa wanakuwa na magonja au maradhi ambayo yanahitajika vipimo vya haraka, sasa imekuwa rahisi zaidi kwa Zanzibar.

MDH imesaidia huduma na matengenezo ya vifaa vya usalama wa viumbe na kununua vifaa vya kupima maabara, kwa ajili ya kujilinda na magonjwa ya mripuko kama ebela, MonkeyPox, homa ya Manjano na vimelea vyengine.

“Msaada huo unajumuisha kuimarisha shughuli za ufuatiliaji na uwezo wa uchunguzi kupitia ITF, CARES na ufadhili wa ARPA, sasa shughuli zote za ufuatiliaji na utoaji wa majibu zitafanyika ndani ya maabara hii,”amesema.

MSIMAMIZI WA MAABARA YA AFYA JAMII PEMBA

Mapema Afisa Mtendaji Mkuu Maabara ya Afya ya Jamii Wawi Pemba Dk. Said Mohamed Ali, amesema lengo la maabara hiyo ya kisasa ni kusaidia serikali katika utambuzi wa maradhi ndani na nje ya nchi.

Hapo akawataka wananchi kufahamu kuwa, hali ya maradhi haitambuliki, hivyo lazima kila mmoja kuwa salama muda wake na kuhakikisha anachunguza afya yake ipasavyo.

WANANCHI NA WADAU WA AFYA WANASEMAJE

Ali Omara Khamis mkaazi wa Chake Chake, amesema kuwepo kwa maabara hiyo ya kisasa ya uchunguzi, itakua mkombozi kwa wananchi wa Pemba, kuondokana na shida ya kusafirishwa kwa baadhi ya sampuli kwenda kuchunguzwa.

“Huu ni ushahidi tosha kuwa, sekta ya Pemba inaanza kuimarika, majengo makubwa ya hospitali za kisasa zipo na tumeona uzinduzi wa maabara hii ya kisasa,” amesema.

Zuwena Haji Ali mtoa huduma za afya Wete, amesema walikua wakipata shida kusafirisha baadhi ya vipimo vya wagonjwa kwenda Tanzania bara au Unguja, sasa kila kitu kinapatikana Pemba.

Aidha amewataka watoa huduma katika maabara kuhakikisha vifaa hivyo wanavitumia kwa uangalifu na kuvitunza ili vidumu kwa muda mrefu.

MWISHO