Walimu wakuu wametakiwa kutowa mashirikiano na taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kwa juhudi wanazozichukuwa kuisaidia Wizara kuinuwa kiwango cha Elimu kwa kuwatowa watoto katika dimbwi la kutojuwa kusoma, kuandika na kuhesabu kupitia mradi wake wa TaRL.
Wito huo alitolewa na Mratibu wa Idara ya Elimu ya watu wazima Pemba Salim Kuza Sheikhan , huko katika ukumbi wa Baraza la Mji Chake Chake Pemba wakati akizungumza na walimu ,wanafunzi ambao walishiriki katika mafunzo mbinu mpya za ufundishaji ambazo zimewafanya wanafunzi kutoka katika dimbwi hilo.
Alisema kitendo kilichofanywa na taasisi hiyo ni kizuri kwani mradi huo umeondowa kilio cha muda mrefu na Wizara ya Elimu na mafunzo ya amali itaendelea kuungana nao ili kuona dhamira ya milele inafikiwa.
Mratibu huyo alisema TaRL imetowa mwanga kwa wanafunzi kwa kuweza kuondowa wimbi la watoto wasiojuwa kusoma , kuandika na kuhesabu kwani tatizo hilo lilikuwa linawakumba wanafunzi waliowengi.
Alifahamisha kuwa taasisi ya Milele Zanzibar Foundation ni kazi ya CCM ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama hicho ya mwaka 2020-2025 kifungu cha 182 sehemu ya Elimu mbadala na elimu ya watu wazima kipengele C.
“ Pamoja na juhudi hizi zinazochukuliwa na taasisi ya Milele Zanzibar Foundation za kuongeza kiwango cha Elimu lakini pia wameweza kuisaidia Serikali na Chama cha Mapinduzi katika Utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi,” alisema.
Alisema kuwa Wizara ya Elimu itaendelea kushirikiana na taasisi ya Milele ili kuona inawalea Walimu waliowapatia mafunzo hayo ya TaRL ili kuona wanapiga hatuwa kubwa kwani kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawajuwi kusoma , kuandika na kuhesabu.
Aliwataka Walimu ambao walipatiwa mafunzo hayo kuyatendea haki kwa kuwafundisha Wanafunzi wao kile walichopatiwa kwa kuelewa kuwa kazi wanayoifanya ni ya wito na malipo yake hayataishia hapa Duniani tu.
Mratibu huyo wa Elimu ya watu wazima Pemba Salim Kuza Sheikhan aliwasisitiza Walimu kuelewa kuwa wao ni kigezo chema na hivyo waende kuwafundisha Wanafunzi wao mambo mema na kujiepusha na mambo maovu , ikiwemo udhalilishaji, ushoga na madawa ya kulevya.
“ Nawaomba musafishe nyoyo zenu ili mukitowe kile ambacho kimo moyoni mwenu kwa ajili ya kuwafunza wanafunzi wenu mambo yenye maslahi kwao”, alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa Milele Zanzibar Foundation Pemba Abdalla Said Abdalla, aliwashukuru Walimu kwa ushirikiano wao katika kufanikisha mradi huo ambao lengo lake kuu ni kumtowa mtoto katika madhila ya kutokujuwa kusoma, kuandika na kuhesabu.
Alisema mradi huo ambao ulizinduliwa mwezi February 2022 ambao ni wa miaka mitano uliwashirikisha Walimu 61 kwa Zanzibar ambapo kwa Pemba ni walimu 30 ambao wamepatiwa vyeti vya uhitimu wa mafunzo ya mbinu bunifu za ufundishaji na kuwatowa watoto 750 wameweza kufanikiwa kutoka walipokuwa mwanzo na wamefikia katika kiwango kinachotakiwa na
mradi huo.
“Niwapongeze Walimu na wanafunzi muliofanya vizuri katika masomo yenu haya kwani mbinu muliozotumia ni za kirafiki zaidi ambazo mumewafanya wanafunzi kuelewa haraka katika masomo yao kupitia mbinu hizi”, alisema.
Nae Mratibu wa mradi huo wa TaRL , Eshe Haji Ramadhan alisema mradi huo wa mbinu bunifu TaRL na mbinu bunifu za Kumpima Mwanafunzi (Teaching at the Right Level) ulikuwa na lengo la kuwawezesha wanafunzi wa darasa la 3 mpaka la 6, kujuwa kusoma , kuandika na kuhesabu.
Alifahamisha kuwa mradi huo uliwajumuisha walimu 61 kwa Zanzibar ambapo Unguja walikuwa 31 na Pemba 30 na ulifanywa kwa Wilaya 10 ambapo jumla ya wanafunzi 2,150 walishirikishwa wakiwemo wanawake 1155 na wanaume 850 mradi ambao ulifanya kwa majaribio.
Alieleza kuwa jumla ya watoto 2,478 kwa Wilaya hizo walifanyiwa tathmini wakiwemo wanawake 1,305 na wanaume 1,173 ambapo tathmini hiyo ilibaini kuwa kati ya watoto 677 wanatatizo la ufahamu wa jukuwa herufi, kusoma maneno, aya wala kusoma hadithi.
Eshe alisema, mradi huo utaendelea kuwawezesha walimu ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi sambamba na kuwaongezea nyenzo zinazoweza kuwasaidia katika kazi zao.
“Tutaendelea kuwawezesha Walimu hawa ili muweze kufanya kazi zenu kwa ufanisi zaidi ili lengo la mradi huu liweze kufikiwa “, alisema.
Hata hivyo Ofisa Elimu idara ya Maandalizi na msingi Pemba maalim Omar Hamad aliishukuru taasisi ya Milele Zanzibar Faundation kwa kusimamia mradi huo ambao utaleta maslahi bora kwa watoto.
MWISHO.