MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amewataka wazanzibari kujipangana kushiriki ipasavyo katika mchakato wa katiba muda utakapowadia ili kuweza kuyasema vyema masuala mbali mbali kwa maslahi ya Zanzibar.
Mhe. Othman ameyasema hayo huko katika Viwanja vya Garagara wilaya ya Mgharibi ‘A’ Unguja alipozungunza katika Mkutano wa hadhara wa chama hicho ulioelezea juu ya masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya Zanzibar.
Amesema kwamba wananchi ni lazima watimize wajibu wao huo katika kuhakikisha wote wanashiriki kikamilifu kwenye mchakato huo wa katiba kwa kuwa hakuna mtetezi wa maslahi ya Zanzibar bila wazanzibari wenyewe.
Mhe. Othman amefahamisha kwamba suala hilo la mchakato wa katiba ni fursa muhimu kwa wazanzibari katika kuyasemea na kutetea mambo muhimu yanayohusu Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba fursa hiyo ilishindikana mwaka 2014.
Mhe. Othman amesisitiuza kwamba hatua itasaidia sasa kupatikana kwa Zanzibar mpya yenye mamlaka kamili ambayo ndio utajiri wa nchi katika kufikia malengo mbali mbali ya kimaendeleo kupitia uwezo wa kuamua na kutekeleza masuala ya miradi mbali mbali kwa maslahi ya nchi.
Akizungunzia suala la Muuungano na Mamlaka ya nchi Mhe. Othman, amesema kwamba hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kupiga hatua bila ya kuwepo mamlaka na kwamba suala hilo la mchakato wa katiba liwauanganishe wazanzibari katika kutetea wanayoyahitaji kuwepo ndani ya Muungano.
Amefahamisha kwamba ni vyema wazanzibari wote kuhakikisha kwamba nchi inaingia katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ikiwa na katiba mpya yenye kuzingatia maslahi ya pende mbili muungano wenye haki na maslahi sawa kwa pande zote mbili.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho , Ismail Jussa Ladhu amesema kwambna ni muhimu nchi kuendesha shughuli zake mbali mbali katika kuzingatia taratibu zilizowekwa pamoja na kuwepo uwazi katika masuala mbali mbali yanayotekelezwa kwenye miradi ya maendeleo ya nchi.
Aliwataka wananchi kuelewa kwamba ACT ni chama kilichodhamiria kuleta mabadiliko yakweli katika kutetea maslahi ya wazanzibari na kuleta maendeleo ya Zanzibar mpya wanayoihitaji wananchi.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo cha Habari leo