Wednesday, January 8

Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amejumuika na waumini wa Masjid Riyaadh Amani katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amejumuika na waumini wa Masjid Riyaadh Amani katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Akiwasalimia waumini hao Alhajj Hemed amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kupinga vitendo viovu nchini ambavyo vinamchukiza Allah (S.W) na kuondoa taswira ya Zanzibar.
Amesema zipo njia nyingi zinazopelekea kuongezeka kwa vitendo hivyo ikiwemo kuwakaribisha watu tusiowajua dhamira na malengo yao, ambao pia  tunashirikiana nao katika harakati za kila siku.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ulimwengu umetawaliwa na utandawazi hivyo, ni vyema kusimamia misingi ya Dini ya Uislamu katika maisha yetu ili kupunguza athari zitokanazo na utandawazi huo.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Barabara na kufafanua kuwa ujenzi huo utazingatia miundombinu ya upitishaji wa maji iliyopo bila ya kuathiri upatikanaji wa huduma hiyo pamoja na makaazi ya wananchi.
Akitoa Khutba katika Sala hiyo Sheikh Othman Khatib Faki amewakumbusha waumini kutumia Neema walizopewa na Allah (S.W) katika kuendeleza Dini ya Uislamu.
Amesema Miongoni mwa Neema walizopewa wanadamu ni Mali na watoto ambapo ni vyema kila mmoja kuhakikisha anatumia Neema hizo kwa umakini ili zisije kuwa miongoni mwa sababu za kupata adhabu mbele ya Allah (S.W)
 Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)