Kassim Nyaki na John Mapepele, Arusha.
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatarajia kufanya maadhimisho ya siku ya Kimondo duniani ambayo itafanyika eneo la Kimondo cha Mbozi, Mkoani Songwe kuanzia Juni 26 – 30, 2023.
Kwa mujibu wa wataalam wa anga, Kimondo cha Mbozi chenye uzito wa tani 16, urefu wa futi 9.80, kimo cha futi 3.30 na upana wa futi 3.30 kwa mara ya kwanza kiligunduliwa na Mzee Halele mkazi wa Kijiji cha Ndolezi kutoka kabila za Wanyiha na baadaye Kimondo hicho kuwekwa katika maandishi na mpelelezi William Nott mwaka 1930.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohammed Mchengerwa amesema
Iengo la maadhimisho ya siku ya Kimondo ni kuendeleza uhifadhi wa urithi wa anga, kuendeleza sayansi na elimu ya anga kwa jamii pamoja na kutangaza zao jipya la utalii wa Anga ( *Astro tourism).*
“Maadhimisho haya yanaenda sambamba na kutambulisha zao jipya la utalii wa anga (astro tourism). Hii ni sehemu ya mkakati wa Wizara kendelea kubuni mazao mapya utalii na kutangaza vivutio vilivyoko mikoa ya kusini, natoa rai kwa wakuu wa Mikoa hiyo na wakuu wa Wilaya kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko mikoa hiyo ili wananchi waijue na kuwa mabalozi kwa wageni wengine wa kimataifa” amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa maadhimisho ya siku kimondo yataambatana na programu mbalimbali ikiwemo kongamano la kimataifa la wanasayansi na wabobezi kuhusiana na elimu na utalii wa anga, utoaji wa elimu kwa jamii pamoja na shule za msingi na Sekondari Wilayani Mbozi.
Programu nyingine ni pamoja na kufanya shughuli za utamaduni, michezo na mbio za Kimondo ( _Kimondo marathon_ ), kupata simulizi kutoka kwa wenyeji kuhusiana na matumizi ya kimondo katika maisha na tamaduni zao pamoja kushindanisha wanafunzi katika ubunifu wa kutengeneza maumbile ya urithi na utalii wa anga.
Akielezea kuhusu tukio la mbio za Kimondo (Kimondo Marathon), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa NCAA anayesimamia Urithi wa Utamaduni na Jiolojia, Mhandisi Joshua Mwankunda ameeleza kuwa Mbio za Kimondo marathon zitafanyika Juni 30, 2023 zitaanzia katika Mji wa Vwawa kuanzia saa 12 asubuhi na kuishia eneo la Hifadhi ya Kimondo kwa umbali wa Km 21.
“Tunategemea mbio hizi zitajumuisha wananchi wengi na zitakuwa katika makundi matatu ambayo ni, kukimbia Kilomita 21 kwa wanaume na wanawake, kilomita 10 kwa wanaume na wanawake na Kilomita 5 kwa watoto na watu wazima.
Mhandisi Mwankunda ameongeza kuwa ada kwa kila mshiriki wa mbio za Kimondo itakuwa Shilingi 30,000 ambayo italipwa kupitia Bank ya NBC kwa akaunti namba *011103033* iliyosajiliwa kwa jina la *The Open University Consultancy Bureau* .
Akielezea zawadi kwa washindi wa mbio hizo Kamishna Mwankunda ameeleza kuwa katika mbio za kilomita 21 mshindi wa Kwanza (Mwanamke na Mwanaume) atapata shilingi 1,000,000, mshindi wa pili shilingi 700,000, mshindi wa 3 Shilingi 500,000, mshindi wa nne Shilingi 300,000, mshindi wa 5 shilingi 200,000 na mshindi wa 6-10 atapatiwa shilingi 100,000.
Katika mbio za kilomita 10 mshindi wa Kwanza (Mwanamke na Mwanaume) atapata 500,000, mshindi wa pili 300,000, mshindi wa 3 Shilingi 200,000, mshindi wa nne Shilingi 150,000, mshindi wa 5 shilingi 100,000 na mshindi wa 6-10 atapatiwa shilingi 50,000 ambapo washiriki wote katika mbio hizo watapatiwa tisheti na Medali.