Sunday, December 29

Taarifa ya Uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi Yatolewa Zanzibar

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui akimkabidhi cheti maalum Meneja wa kitengo cha maradhi yasioambukiza Zanzibar (NCD) Dkt.Omar Muhammed Sleiman wakati wa hafla ya kuwaaga madaktari kutoka Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China ambao waliendesha zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi hivi karibuni katika vituo mbalimbali vya Afya ,hafla iliyofanyika Ofisi za Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui akiwakabidhi vyeti vya ushiriki baadhi ya madaktari kutoka Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China ambao waloshiriki zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi liliofanyika hivi karibuni katika vituo mbali mbali vya afya , wakati wa hafla ya kuwaaga madaktari hao iliyofanyika Ofisi za Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui akiwakabidhi vyeti maalum watendaji wa Afya kitengo cha maradhi yasiambukiza walioshiriki zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi liliofanyika hivi karibuni katika vituo mbali mbali vya afya ,wakati wa hafla ya kuwaaga timu ya madktari kutoka Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China ambao waliongoza zoezi hilo,hafla iliyofanyika Ofisi za Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui akizumza na madaktari wa Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China ambao waliendesha zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi liliofanyika hivi karibuni katika vituo mbali mbali vya afya , wakati wa hafla ya kuwaaga madaktari hao iliyofanyika Ofisi za Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.

Na Rahma Khamis -Maelezo  Zanzibar.

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amewataka wananchi kuwahi Hospitali  na kupatiwa tiba mapema ili kuepusha vifo visivyotarajiwa.

Ameyasema hayo huko Ofisini kwake Mnazmmoja wakati alipokuwa akipokea taarifa ya matokea ya Uchunguzi wa  saratani ya shingo ya kizazi uliofanyika hivi karibuni katika vituo mbalimbali vya Afya Mjini na Vijijini.
Amesema kuwa maradhi hayo yameshamiri katika jamii hivyo ipo haja kwa wananchi kujitokeza mapema kufanya uchunguzi pindi zikitokea fursa kama hizo.
Aidha amesema kuwa amefurahi kuona maradhi hayo yanapatiwa matibabu Zanzibar hivyo watahakikisha vifaa tiba vinakuwepo katika kitengo cha maradhi hayo.
Waziri  amesema Serikali ina nia ya kufanya kazi na Madaktari kutoka China  ili wananchi wafanyiwe uchunguzi na kupatiwa matibabu ya uhakika.
Hata hivyo Waziri  amewashukuru na kuwaomba madaktari hao  kuendelea kuwa na ushirikiano kati yao na Serikali ya Zanzibar Kwani uhusiano wao unaleta tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla
Akitoa taarifa  ya uchunguzi huo Meneja  wa Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza (NCD) Omar Mohamed Suleiman amefahamisha kuwa jumla ya  akina 4412 wamefanyiwa uchunguzi ambapo kati yao wanawake 151 wamegundulika kuwa na tatizo hilo katika hatua tofauti.
Katika hatua nyengine Meneja amefahamisha kuwawaanawake 131   wamegundulika kuwa na ugonjwa huo katika hatua za awali na wanawake 20 wamethibitika kuugua saratani ya shingo ya kizazi katika hatua za juu ambapo hatua za matibabu zimeanza kuchukuliwa kwa wagonjwa hao.
Ameongeza kuwa uchunguzi umebaini kuwa  jumla ya wanawake  854 wamebainika kuwa na magonjwa mengine katika via vya uzazi ikiwemo magonjwa ya zinaa.
Nae Mkurugenzi  mkuu wa Wizara  ya Afya Zanzibar Amour Sleiman mohammed amesema  Wizara  inatumia gharama kubwa katika kuwapatia matibabu wagonjwa wa saratani  hivyo kufanyika kwa  zoezi hilo kumepunguza gharama za serikali kufanya matibabu hayo nje ya nchi .
Aidha Ameishukuru timu ya  madaktari kutoka Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China kwa ujio wao na kufanikisha kuwagundua wagonjwa wa tatizo hilo na kuwapatia matibabu.
Hata hivyo mkurugenzi  ameiomba timu ya madaktari hao kuongeza muda na awamu za kufanya uchunguzi ili  kupunguza ongezeko la wagonjwa wa maradhi hayo.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni timu ya  madaktari kutoka Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China wakishirikiana na Wizara ya Afya kupitia kitengo cha maradhi yasioambukiza waliendesha zoezi la uchunguzi wa Saratani ya shingo ya kizazi wakikadiria kufanya uchunguzi kwa wanawake 4000 na wamefanikiwa kuchunguza zaidi ya hao.