Friday, March 14

WATANO WAKAMATWA NA POLISI KWA WIZI KASKAZINI UNGUJA

NA OMAR HASSAN – ZANZIBAR 
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja limefanikiwa kuwakamata watu watano kwa tuhuma za  wizi wa waya wa umeme wenye thamani ya shilingi milioni 70 na wizi wa mafuta ya dizel madumu 20.
Akizungumza na vyombo vya habari huko Ofisini kwake Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja Kamanda wa Polisi Mkoa huo Kamishna Msaidizi wa Polisi Daniel Shila amesema Juni 3 mwaka huu majira ya saa 8.30 usiku watuhumiwa Said Juma Said (30) mkaazi wa Nyarugusu, Juma Khamis Juma (34) mkaazi wa Mahonda, Robert Simon Makala (38) mkaazi wa Kiwengwa na Juma Haji Omar (46) mkaazi wa Magogoni wanatuhumiwa kuiba waya wa umeme mita 1064 wenye thamani ya milioni 70 huko katika eneo la ujenzi wa Hoteli ya Zanzibar Wave Kiwengwa.
Aidha Kamanda Shila ameeleza kuwa Juni 7 mwaka huu, saa 8.30 usiku huko Kazole, Wilaya ya Kaskazini B Jeshi la Polisi katika Mkoa huo limemkamta Makame Kondo Ali (45) mkaazi wa Kazole akiwa na madumu 14 yenye lita 280 za mafuta ya Dizel ambayo yanasadikiwa kuibiwa katika Mradi wa ujenzi wa barabara huko mangapwani, Wilaya ya Kaskazini B.
kamanda shila amesema doria za mara kwa mara  zitaendelea na kuwataka wananchi kushirikiana na jeshi la polisi katika kudhibiti uhalifu kwenye mkoa huo.