Saturday, December 28

UWT wamkabidhi kadi ya uananchama Mama Mariam Mwinyi

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi amewahimiza Wanawake CCM, kupigania nafasi za maamuzi kwenye uongozi ili kuendelea kuwainua wanawake wasio na sauti na kuwasihi kamwe wasirudi nyuma kwa hatua waliopiga.

Amesema amefurahishwa na kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na aliwataka waongeze juhudi katika kutetea maslahi ya mwanamke nchini.
Mama Mariam Mwinyi aliyasema hayo alipozungumza na kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Amani Kichama, iliyofika Ofisini kwake Migombani Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Bi. Fransisca  Clement waliofika kwa lengo la kumkabidhi kadi ya uanachama wa (UWT).
Aidha, alisisitiza zaidi suala la kumkomboa mwanamke kujikwamua kiuchumi pamoja na kuwasihi kila penye jitihada ya mwanamke wasisite kuweka mikono yao ili kuwasaidia wanawake wenzao kuzifikia ndoto za mafanikio yao.
“Kila penye juhudi, tuhakikishe tunaweka mikono yetu, ili tuwaongoze wanawake wenzetu, wanajitahidi sana kuchangia maendeleo ya nchi yetu, hawachoki kwaajili ya familia zao na nchi yao” Kwa hisia alizungumza Mama Mariam Mwinyi.
Mama Mariam ambae pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) alisema lengo la kuunda taasisi hiyo ni kumkomboa mwanamke ili atambue haki zake katika kuzikimbilia fursa za maendeleo.
Aliwaeleza UWT kwamba kazi kubwa zinazofanywa na ZMBF ni pamoja na kuungamkono harakati za wananwake na kinamama wanaojikwamua kimaendeleo pia kuwashajihisha juu ya kuzingatia lishe bora ili kuimarisha afya za mama wajawazito na kuepusha vifo wakati wa kujifungua, kushajihisha jamii kufanya mazoezi ili kujizuia na maradhi yasiyoambukiza yakiwemo moyo, kisukari na saratani pamoja na kumsitiri mtoto wa kike aendelee kuwa kwenye hedhi salama kwa mustakbali mzima wa maendeleo yake kielimu.
Alieleza ZMBF ni chachu ya maendeleo ya wanawake, vijana na watoto dhidi ya changamoto wanazokumbana nazo kwenye jamii, zikiwemo za afya, elimu na jamii kwa kushajihisha wanawake kuinuka kiuchumi kupitia ukulima wa mwani na kupinga udhalilishaji wa watoto.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa (UWT), kutoka Wilaya ya Amani Kichama, Bi. Fransisca  Clement aliueleza Mama Mariam Mwinyi lengo la UWT Wilaya ya Amani kumkabidhi kadi hiyo ya uanachama ni kwasababu Mama ni Mwanachama wa CCM wa Jimbo la Kilimani ambalo limo ndani ya Wilaya ya Amani Kichama.
Pia, Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumualika Mama Mariam Mwinyi kuwa mgeni rasmi kwenye Bonanza la kuwakabidhi kadi wanachama 500 ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 24 mwaka huu.
Alisema Bonanza hilo linatarajiwa kuhusisha michezo na mashindano ya aina mbalimbali ikiwemo mchezo wa kufukuza kuku, kukuna nazi, nage, kula mandazi, matembezi ya hiari, mazoezi ambapo michezo yote hiyo inawashirikisha wanawake watupu wakiongozwa na DJ mwanamke.
Aidha, alieleza kutakua na zoezi la kupima afya ikiwemo kuchangia damu salama, kupima maradhi yasiyoambukiza yakiwemo moyo, kisukari, presha na COVID 19.
Akizungumza kwenye halfa hiyo, Mwakilishi kutoka Viti maalum (CCM) ambae pia ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita alimfikishia Mama Mariam Mwinyi, salamu za wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba, walizompa kupitia Baraza la Wawakilishi kwenye kipindi cha maswali na majibu baada ya kumuuliza kwanini taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” haifanyi mabonanza yake kwenye mkoa huo.
Hivyo, Waziri Tabia, alimuomba Mama Mariam Mwinyi kuangalia uwezekano wa kuwafikia wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba ili ashiriki nao kwenye mazoezi na matembezi ya hiari kama anavyofanya mikoa mengine ya Zanzibar.
Kamati tekelezaji ya Umoja wa Wanawake Wilaya ya Amani kichama iliyofika ofisi za ZMBF Migombani, ni wasimamizi wa siasa za wanawake wa Wilaya ya Amani kichama ambayo inaundwa na majimbo matano likiwemo la Amani, Chumbuni, Kilimani, Magomeni na Shaurimoyo.
IDARA YA MAWASILIANO – IKULU, ZANZIBAR