Sunday, November 24

Vijiji sita vyanufaika na huduma ya umeme wa uhakika.

NA ABDI SULEIMAN.

JUMLA ya Vijiji sita vyenye nyumba 216 kutoka Wilaya ya Mkoani, Micheweni na Wete, vinanufaika na huduma ya umeme wa uhakika baada ya kuzinduliwa kwa miradi ya umeme ndani ya mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 2023 Kisiwani Pemba. 

Vijiji hivyo kwa Wilaya ya Mkoani ni Mtadoda, Mikinduni na Mgelele, Wilaya ya Wete ni kijiji cha Mitondooni na Wilaya ya Micheweni ni Mtondoo Jeuri na Raha Leo shehia ya Makangale.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika uzinduzi wamiradi hiyo ya umeme, Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar Tawi la Pemba Mohamed juma Othman, alisema vijiji vya Mtandoda, Mikinduni na Mgelele kwa Wilaya ya Mkoani mradi huo umegharimu shilingi Milioni 151.28.

Alisema fedha hizo zimetumika kwa kazi upimaji wa kilomita 1.1km, uwekaji wa tansfoma yenye uwezo wa KVA 100, usambazaji wa njia ndogo zenye urefu wa kilomita 2.8.

Alisema jumla ya wananchi 18 wamelipwa fidia ya vipando vyao vilivyogharimu shilingi Milioni 31.71, kutokana na kazi hiyo, huku ZECO limefanikiwa kuwaunganishia huduma ya umeme wananchi 96.

Kwa upande wa vijiji vya Mtondoo jeuri na Rahaleo katika shehia ya Makangale Wilaya ya Micheweni, jumla ya shilingi Milioni 97.61 zimetumika kufikishia huduma ya umeme kwenye vijiji hivyo.

Alisema vijiji hivyo vinawastani wa nyumba 50 zinazotakiwa kuungiwa huduma hiyo, kwa wananchi wa shehia hizo wanajishuhulisha zaidi na kazi za uvuvi, kwani kukamilika kwao kutaongeza thamani na kurahisisha usanifu wa bidhaa zinazozalishwa kutokana na shuhuli zainzofanywa na wananchi.

“kazi hii imetokana na usambazaji wa laini ndogo, ujenzi wake na uwekaji wake wa tansfoma na kuwafanya wananchi waweze kutumia huduma hiyo,”alisema.

Katika Wilaya ya Wete kijiji cha Mitondooni, kazi ya upelekaji umeme umegharimu jumla ya shilingi Milioni 83.59,ikiwa na wastani wanyumba 50 zitakazonufaika na huduma hiyo.

Alidha ameneja huyo alisema ZECO linawaungia wananchi huduma ya umeme kwa shilingi laki mbili (200,000) na fedha zinazobakia zinalipwa na serikali, lengo ni kufanya wananchi wote wanatumia huduma hiyo.

Aliwasisitiza wananchi kuendelea kutumia fusra hiyo iliyotolewa na serikali, nakuwataka kuhakikisha wanalinda miundombinu hiyo ya umeme ili idumu kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2023, Abdalla Shaibu Kaimu aliwataka wananchi kuitumia fura hiyo iliyotolewa na serikali, kwa kuhakikisha wanaunga umeme katika nyumba zao.

Alisema umeme umeweza kurahisisha maendeleo kwa mtu mmoja mmoja, ikiwemo kukuza kipato chao kwa kuanzisha miradi ya maendeleo ikiwemo maduka, kuuza malai hata kupikia vyakula.

Nao wananchi wa shehia hizo, wamepongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane kwa kuwafikishia huduma ya umeme ambayo wameisubiria kwa muda mrefu.

MWISHO