Sunday, November 24

Watu 23865 wamepima afya zao katika kipindi cha Julai 2022 hadi Mach 2023 Kisiwani Pemba.

NA ABDI SULEIMAN.

JUMLA ya Watu 23865 wamepima afya zao katika kipindi cha Julai 2022 hadi Mach 2023 Kisiwani Pemba, Wanaume 11,408 na Wanawake ni 12457, huku wananchi 58 waligundulika na maambukizi mapya ya VVU.

Kwa mujibu wa ripoti za Makabidhiano ya Mwenge wa uhuru kitaifa 2023, Mkoa wa Kaskazini Pemba kwenda Mkoa wa Kusini Pemba na Mkoa wa Kusini Pemba Kwenda Mkoa wa Tanga.

Kwa Mkoa Kaskazini Pemba kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, Jumla ya watu 10,298 wanaume 4387 na wanawake 5911 wamepatiwa ushauri nasaha na kupima Virusi vya Ukimwi.

Wilaya ya Wete watu 5412 wanaume 2,238 na wanawake 3,174, huku Wilaya ya Micheweni watu 4886 wanaume 2,149 na wanawake 2,737 kati ya watu 20 waligunduliwa na maambukizi ya VVU Wilaya ya Wete 14 na Micheweni watu sita (6).

Kwa upande wa Mkoa wa Kusini Pemba katika kupambana na VVU kupitia kauli mbiu”Pima, Jitambue, Ishi” kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 jumla ya wananchi 13,567 walipatiwa ushauri nasaha kupimwa maambukizi ya VVU.

Aidha kati ya hao Wanaume 7,021 na wanawake 6,546, huku uchunguzi ulionyesha kwamba wananchi 38 waligundulika na maambukizi mapya sawa na asilimia 0.3, Wanaume 18 na Wanawake 20.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mratib wa Tume ya Ukimwi Pemba Ali Mbarouk Omar, alisema wanaendelea kutoa elimu kupitia makundi maalumu, na kupita katika vijiwe vya vijana wanaojidunga sindano.

Alisema kupitia baadhi ya Jumuiya mbali mbali huwafikia wananchi moja kwa moja, kwa kuwapatia ushauri nasaha juu ya upimaji wa afya zao mara kwa mara.

“Maambukizi ya VVU yapo wananchi watakiwa kuchukua tahadhari ikiwemo kujikinda na maambukizi mapya, sabamba na kupima afya zao mara kwa mara”alisema.

Hata hivyo alisema wataendelea kutoa elimu kwa jamii, kupitia makundi maalumu ambayo yanaonekana maambukizo kuwa makubwa, ikiwemo wanaume wanaofanya mapenzi jinsia moja, wanawake kwa wanawake na wanawake wanaojiuza.

Kwa mujibu wa hutuba ya waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa kwanza Rais Zanzibar, kuhusu makadirio ya Mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 iliyosomwa na Waziri Harusi Said Suleiman, imesema hadi kufikia Disemba 2022 jumla ya watu 8,975 wamesajiliwa katika klink za tiba mwaka jana.

Alisema watu waliosajiliwa walikua 7,589 takwimu zinaonyesha kuna ongezeko la watu 1,386, huku uzito wa maradhi unaendelea kuwaelemea wanawake kuliko wanaume, kwani kati ya watu 8,975 walioambukizwa VVU, watu 6,074 ni wanawake sawa na asilimia 67.6 na wanaume ni 2,901 sawa na asilimia 32.3.

MWISHO