NA HAJI NASSOR, PEMBA
HAPO zamani Magofu ya Mkama Ndume yalikuwa makaazi ya waswahili, ya enzi za kati, ambayo yaliachwa na wakaazi wake katika karne ya 16.
Ambapo hapo, ilikuwa ni kabla ya Wareno Afrika Mashariki inajulikana kwa uimarishaji wake kwa kutumia mawe.
Magofufu hayo yako wastani wa kilomita 10 kutoka katikati ya mji wa Chake chake, ambao ndio makao makuu kwa kisiwa cha Pemba.
Kwa wakati huo mji huo ulitawaliwa na kiongozi mmoja aitwaye Mohammed bin Abdul -Rahman, ambaye alijulikana sana kwa ukatili wake kwa raia wake.
Na kwa wakati huo alipewa jina la utani la Mkama Ndume lenye maana ya mkamua wanaume kwa lugha ya kiswahili cha zamani.
Ndio maana, hadi leo eneo hilo lililojaa historia sio kwa kisiwa cha Pemba pekee, bali baraza zima la Afrika na duniani, pakaitwa Mkama Ndume.
Kwa kuwa mtawala alikuwa akifanya ibada, alijenga msikiti wa asili wa Ijumaa, miaka 700 iliyopita, ambao ulikuwa na nguzo tisa.
Nguzo tatu mbele, tatu nyuma na katikati ya msikiti huo, ambapo wenyeji wa kijiji cha Pujini waliutumia kwa swala la Ijumaa pekee.
Mkama Ndume, alionekana kusoma mno, maana alikuwa akitunga na kusoma mwenyewe hutuba ya swala la Ijumaa kwa wakati huo.
Alikuwa ni muumini mkubwa, hasa kwa ushajaa wake wa kutunga na kusoma hutuba ya kwenye sala ya Ijumaa.
Kisha Mkama Ndume, baada ya kusikia kuwa, wapo watu wengine zaidi yake kuweza kutunga na kusoma hutuba, alitoa nafasi hiyo.
‘’Ikiwa hao watu wapo wanaoweza kutunga na kusoma hutuba na watu kumuelewa kama mimi, nitamarithisha msikiti huu na uwe milki yake,’’alinukukuliwa Mkama Ndume.
Ingawa alisema iwapo hutuba hiyo hatoiweza na kuiharibu, aliahidi kuondoa kichwa, ingawa siku nyingine yupo mtu aliyepanda kwenye kiriri cha msikiti na kutoa hutuba na kufahamika mno.
Kwenye karatasi aliyoiandaa mtu mwengine, inasemekana Mkama Ndume, alichomoa, ili baada ya swala apate kumuadhibu mtu huyo, ingawa alifanikiwa na kuisoma vyema.
Kisha baada ya kumaliza hutuba, Mkama Ndume aliridhishwa na mtunzi na msomaji na hapo alisimama mbele ya waumini na kumrithisha mtu huyo, kwa wakati huo.
Nyuma ya Mskiti huo, kuna kisima kilichokuwa kikitumika wakati huo, ambapo hadi wenyeweji wa Pujini baadhi yao hukitumia kwa maombi mbali mbali ya makusudio ya mambo yao kwa sasa.
Kwa wakati huo wa Mkama Ndume, Ng’ombe, kuku walikuwa wakifungwa kwenye nondo za madirisha ya Msikiti kama ishara ya sadaka au kafara.
Hapo ilikuwa kila mmoja, alikuwa na uwezo wa kuchukua atakachokikuta, hata vyakula mfano pilau ni jambo lililozoeleka eneo hilo, kwa watu kuondosha mfano wa nadhiri, kwa muombaji kupata alichokiomba.
Kwa sasa eneo hili, ambalo limeshaimarishwa na wizara husika, limeongeza umaarufu na hasa baada ya kuimarishwa kimajenzi.
Kwa mfano kuanzia mwaka wa fedha wa 2021/2022 Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kwa wakati huo, ilipanga kuyaimarisha maeneo ya kihistoria, likiwemo la Mkama Ndume.
Lakini pia, maeneo mengine kwa Pemba yaliopangwa kuimarisha, ni pamoja na Pango la Watoro na Pango la kijiji yaliyopo Makangale Pemba, Misikiti na Makaburi ya kihistoria yaliyopo Chwaka Tumbe.
Kwa wakati huo mradi huu kwa ujumla Unguja na Pemba ulitengewa shilingi bilioni 3.5, lengo likiwa ni kuimarisha sekta ya utalii.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Simai Mohamed Said, anasema mpango wa kuimarisha utalii kwa wote ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 mradi ulitengewa shilingi bilioni 2, ingawa hadi mwezi Machi 2022, haukuingiziwa fedha.
Pamoja na hayo, tayari Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale ilipokea wananchi mbali mbali 3,698 ambao wametembelea maeneo na sehemu za kihistoria yaliyopo Unguja na Pemba.
Tena kati ya watu hao, wenyeji waliotembelea maeneo hayo walikuwa ni 761, wageni kutoka nje ya nchi ni 1,437 na wanafunzi ni 1,500.
Mwaka mwengine wa fedha, wa 2022/2023 Wizara ilipanga kukamilisha malipo kwa kampuni ya Shamjo Co. LTD ambayo ni shilingi bilioni 284.097 ambayo iliyojenga eneo la kihistoria la Mkama Ndume.
Mkuu Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba Khamis Ali Juma, anasema historia ya Pemba, haiwezi kukamilika bila ya kumtaja Mkama Ndume.
Mkama Ndume, ni kigezo kikubwa, na wengi wanafikiria kuwa alikuwa ni mithili ya jini, bali ni mtu kutoka nchi ya Iran.
‘’Kule nchi ya Iran, ambako alitokea huyu Mkama Ndume, kuna kijiji kinaitwa Shirazi, na hao ndio washirazi waliofika kisiwani Pemba karne ya 15,’’anasema.
Eneo aliliofikia Mkama Ndume kama jina lake la utani, kabla likiitwa mjini Pujini, ingawa kwa sasa, limebeba jina la Mkama Ndume.
Mohamed Bin Abrhaman (Mkama Ndume), alikuwa na uhusiano wa karibu na wanajamii wa Pujini kwa wakati huo, ingawa alikuwa pia akitoa adhabu kwa wakosaji.
‘’Kwa mfano wale wazee wanaume ambao wameshang’oka meno, wanapofanya makosa akiwapa tunda ngumu aina chikichi ili wavunje,’’anasema Khamis.
Mtawala huyo ambae baadae alikuwa mfalme, kwa upande wa wazee wanawake, waliofanya makosa akiwabebesha mawe zaidi ya kilomita 8 kutoka eneo moja hadi hapo Pujini.
Kwa waliofanya makosa makubwa ya jinai, kama ni wanaume akiwakamua uume zao, mithili ya mtu anaekamua maziwa ya Ng’ombe.
Mkuu huyo wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba, Khamis Ali Juma, anasema hapo ndipo lilipozaliwa ramsi jina Mkama Ndume.
‘’Ingawa kwanza jina hilo, lilitambulika kama, ‘mkama waume’ na kisha baada ya miaka kadhaa, likaitwa Mkama Ndume hadi leo,’’anafafanua.
UTAWALA ULIVYOKUWA PEMBA
Kwa wakati huo, kisiwa cha Pemba kilikuwa kimegawiwa na kutawaliwa kijadi, na chenyewe kugawiwa katika diwani tano, ikiwemo ya Chwaka wilaya ya Micheweni (zamani ikiitwa Twaka), ambapo inasemakana alikuwa ni mtoto wa Mkama Ndume, aliyeitwa Haroun.
Diwani ya pili ya utawala, ilikuwa ikiitwa Kambaluu (sasa Mkumbuu) wilaya ya Chake chake, huku diwani ya tatu ilijulikana kwa jina la ‘Utenzi au Ngwane’.
Hili ni eneo la Ziwani, kwendea Vitongoji na Ole wilaya ya Chake chake, na diwani ya nne ikiitwa Pokomo, ni aina ya watu waliotoka Somalia, ambao walianzisha utawala wao wa jadi kisiwani Pemba.
Diwani ya tano ikijulikana ‘Ukoma’ ambazo diwani hizi ndio zilizoijenga Pemba kijadi na hasa eneo la utawala.
Mtawala wa jadi zote hizo tano alikuwa ni Mohamed Bin Abrhman ‘Mkama Ndume’ ambae kwa wakati huo alikuwa muumini mkubwa dini ya kiislamu, licha ya vituko vyake alivyokuwa navyo.
KISIMA
Ni kweli Mkama Ndume alikuwa na wake wawili, waliokuwa wakitumia kisima kimoja na kuishi nyumba moja bila ya kuonana, ambapo mmoja alitumia roda na mwengine kutumia ngazi maalum kuchuta maji.
MZIMU
Mkama Ndume pamoja na kuwa muumini wa kweli, alikuwa na eneo maalum, kwa ajili ya shughuli zake mbali mbali za kijadi.
KIFO CHA MKAMA NDUME
Pamoja na kuwa alikuwa na watoto wanne akiwemo Haroun, Mjawiri, Mwanamtoto, lakini kifo chake hakuna kumbu kumbu zinazoonesha, kama alididimia au alifariki baharini.
Hivyo hakuna pahala ndani ya Pemba, kuwepo kwa kaburi la Mkama Ndume, na wala wake zake wawili, kama ilivyo kwa watoto wao.
Eneo lake la makaazi, lilizungumkwa na kuta nne, na kila moja ikiwa na mlinzi, ambapo kuta ya kwanza ilikuwa na urefu wa mita 6, ya pili mita 4, mita 2 na mita moja.
Pemba inayo zaidi ya maeneo ya kihistoria 45, kama vivutio vya utalii kisiwani humo.
Omar Khamis Makame, mzee wa Jadi Mkama Ndume, anasema hadi leo, eneo la mizimu anaedelea kulitumia, na amekuwa akitoa maelezo kwa wageni mbali mbali.
Mwisho