NA MARYAM SALUM, PEMBA
SKULI ya sekondari ya Connecting Continent iliyopo nje kidogo ya mji wa Chake chake, ni miongoni mwa skuli 10 binfsi zilizopo kisiwani Pemba.
Skuli hiyo ipo nje kidogo ya mji wa Chake Chake, imekuwa ikiwavutia zaidi na wanafunzi wasichana kutokana na upasishaji wake mzuri wa kila mwaka.
Conecting ni miongoni mwa skuli 10 binafsi kisiwani Pemba, zilizobahatika kuruhusiwa kuwekeza katika elimu kwa ngazi ya sekondari.
Skuli hiyo ilianzishwa mwaka 2006 ikimilikiwa na wawekezaji wajerumani, ikiendeshwa na michango midogo midogo ya wafadhili wenyewe na ada nyepesi zinatolewa na wazazi na walezi.
Skuli hiyo ilianza kufanya mitihani ya taifa mwaka 2008, na kufika mwaka 2022, wanafunzi 671 walihitimu.
Kati ya wanafunzi hao wanawake walikuwa 332 na wanaume walikuwa 339 kwa wakati huo, wakitokea skuli mbali mbali za msingi kisiwani Pemba.
Mwandishi wa makala hii hakutaka hadithi za mdomo alitaka kujua kinaga ubaga historia japo fupi ya skuli hio hadi ilipofika.
Mwalimu mkuu skulini hapo mwana mama Mwache Juma Abdalla, anasema kuwa mwaka 2020 wanafunzi 58 walifanya mtihani wa taifa kidato cha nne, 24 wanawake na 34 wanaume,mwaka 2021, 43 wanaume 17 wanawake 26, mwaka 2022, 83 wanaume 28 na wanawake 55.
Mwaache anaeleza kutokana na ufaulu kupanda mwaka hadi mwaka ni uthibitisho tosha kuwa, skuli hiyo, jambo ambalo litaweza kufikia malengo waliyojipangia.
Anaeleza kuwa, idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu ni wanawake, na ndio maana kila mwaka wanapokea zaidi wanafunzi wa jinsi hiyo.
Anaona Serikali ya Mapinduzi inafanya jitihada mbali mbali kuhakikisha kila mtoto, anapata haki ya msingi ikiwemo elimu.
Kutokana na umuhimu huo, ndipo Serikali ikaruhusu mashirika na taasisi mbali mbali hata kutoka nje kuwekeza tasnia hiyo nchini, kwa maendeleo zaidi.
Hatuwa hiyo ni pamoja na kuanzisha skuli za maadalizi, msingi na Sekondari kwa kufuata misingi na kanuni zilizowekwa.
LENGO LA WAMILIKI KUANZISHA SKULI HIYO
Moja ni kuwasaidia wananachi wa Zanzibar, kupata skuli bora itakayoinua maisha yao kwa maendeleo, na kupata elimu yenye kiwango.
Anafahamisha kuwa, skuli hiyo inachukuwa wanafunzi wa kawaida na wenye mahitaji maalum, ili makusudi lengo liweze kufikiwa.
Lengo ni kuona kila mmoja, anapata haki hiyo ya elimu sawa kama wanavyopata wengine katika jamii mbali mbali.
Akielezea suala la kupokea wananfunzi kwanza zipo taratibu mbali mbali hufanyika ikiwemo usaili utakaoleta majibu mazuri.
‘’Tunafanya mitihani mara mbili kwa kipimo zaidi na ili mwanafunzi turidhike nae na kuendelea na darasa la tisa nilazima afikie daraja C, bila hapo skuli haichukui kwani itakua ni mzigo bila matunda,’’anasema Mwalimu huyo Mkuu.
Akigusia mafanikio, anasema ni mengi na makubwa, ikiwemo kupasisha wanafunzi katika kiwango cha juu kila mwaka, kuengezeka kwa madarasa kutoa vyumba vinne (4) na kufikia 10, maabara tatu (3) na maktaba.
WANAFUNZI WA SASA
Fatma Mohamed Bakar anaesoma kidato cha tatu mwenye ulemavu wa viungo, anaeleza sababu zilizomfanya kujiunga skulini hapo, ni pamoja na kiwango kizuri cha ufaulu hasa wanawake.
‘’Waalimu wa skuli hii wanakua na juhudi binafsi katika ufundishi, ambao unatufanya kila mmoja kufahamu na kisha kufaulu,’’anasema.
Husna Mohamed Haji anaeleza amejiunga katika kituo hicho mwaka 2021, akiwa darasa la tisa baada ya kupasi michepuo katika skuli ya Pindua.
Anaeleza kuwa licha ya kuwa na upungufu wa usikivu haikuwa changamoto kwake, kutoendelea na masomo katika skuli hiyo kubwa.
“Nashukuru kwa kuwapa moyo wa imani wazazi, walimu wangu pamoja na wanafunzi wenzangu na jamii iliyonizunguka hadi nilipofika,’’anasema.
‘’Walimu wanaposomesha hutoa sauti ili niweze kusikia na kufahamu vizuri kinachosomeshwa na kisha hufanya vizuri kuanzia mitihani ya ndani hadi taifa,” anaeleza.
Kwa upande wa malengo yake ya baadae Husna anasema ni mengi moja ni kuhakikisha anasoma kwa bidi hasa masomo ya sayansi ili kufikia ndoto zake yakuwa ijinia.
‘’Lengo langu nikuhakikisha najikita zaidi kusoma masomo ya sayansi ikiwemo physics,Chemistry na hesabati,(PCM)ili niwe injinia,” alieleza.
KWA UPANDE WA MATOKEO KWA MWAKA
Mwaka 2022 katika ufaulu wa wananfuzni walipata daraja la tatu, nne, lakini miaka ya karibuni kiwango cha ufaulu kilipanda.
Mwalimu huyo anaeleza kuwa, hiyo ni kutokana na ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe, kuhakikisha wanatoka walipokuwa na kufika pale wanapotaka kimaendeleo.
Anaeleza kuwa mashirikiano hayo ndio njia pekee iliyopelekea kuondosha daraja la nne na zero, na kupata daraja la kwanza, la pili na tatu tu.
Ambapo kwa mwaka 2022 skuli ilifanikiwa kupasisha kwa kiwango cha daraja kwanza wanafunzi 4, daraja la pili wanafunzi 43, la tatu wanafunzi 30, na daraja la nne walikuwa wanafunzi wawili (2).
Hivyo matokeo hayo ni ushahidi tosha kwamba skuli hiyo inatoa matokeo mazuri zaidi kuliko skuli nyengine za binfsi zilizopo Kisiwani humu, ni takribani miaka 8 sasa hakuna zero.
MASHIRIKIANO NA SERIKALI.
Mwalimu huyo anasema mashirikiano baina yao na Wizara ya elimu ni mazuri, na ndio maana wakaweza kufikia hapo walipo sasa.
‘’Bila mashirikiano na Wizara tusingalifika hapa tulipofika kimaendeleo, kwani kila jambo linahitaji mashirikiano.
CHANGAMOTO
Alisema kuwa nikukosa dahalia la uhakika kwa watoto wanafunzi, kwani sehemu wanalala ni nyumba za watu binafsi.
‘’Zipo yumba za watu binafsi wazazi ndio wanatoa fedha zao kwa ajili yakulipia kodi na chakula, jambo ambalo linawapa mashaka, kwa kuwepo uangalizi mdogo hasa kwa wanaume.
Akizungumzia suala la kodi kwa Mamlaka ya Mapato Zanzibar ZRA, ameomba wafanyiwe msamaha kwani kituo hicho hakipo kibiashara kipo kusaidia jamii zaidi kupata elimu.
‘’Kwa mfano hapa wapo wanafunzi 300, lakini wapo waliofiliwa na mzazi, wenye mazingira magumu na wenye kipato duni hawalipi ada,’’anasema.
Hivyo mamlaka hiyo ni vyema kumuunga mkono mfadhili huyo, kwani lengo ni kusaidia watoto hasa mayatima na wenye hali ngumu na sio kibiashara.
WALIOWAHI KUSOMA
Juma Kitwana Bilali anaeleza kuwa, Connecting ni miongoni mwa skuli binafsi yenye kiwango kizuri cha kupasisha hasa watoto wa kike.
‘’Mimi nimesoma connecting na kwa sasa nasomesha wenzagu katika kituo hichi,” anaeleza.
Hivyo kuwataka wazazi na walezi kuendeleza mashirikiano kwa walimu, ili wapate kuboresha taaluma hiyo kimaendeleo.
Mwanafunzi Omar Ali Juma, anasema ameshawahi kuwa baharia katika meli za nje, baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari skuli hapo.
MALENGO YA SKULI BAADAE
Mwalimu huyo anasema ni kufika mbali zaidi kielimu, kutoka walipo kimatokeo, na pia kuwa na wanafunzi hadi wa kidato cha sita.
Akizungumzia suala la upasishaji anasema kuwa wanaka kuwa na kiwango cha daraja daraja la kwanza, na pili tu sio tatu, nne wala zero.
Skuli ya Conecting Continent Organization iliyopo Mgogoni Wilaya ya Chake Chake imeanzishwa mwaka 2006, ikiwa na wanafunzi 18 tu wa darasa wa tisa.
Ambapo kwa sasa wapo na wanafunzi wakidato cha nne 58, wakiwemo wakike 29 na wakiume 29, wanaotarajiwa kufanya mitihani yao ya taifa kwa mwaka 2023.
Mwenyekiti wa bodi ya wazazi skulini hapo Said Mohamed Ali anasema kuwa skuli ipo vizuri kiutendaji kwani kimatokeo takribani miaka 8 sasa hawajawahi kufelisha.
Anachojivunia Mwenyekiti huyo ni umoja, mshikamano uliopo baina ya waalimu, wazazi na Bodi ya wazazi skuli hapo.
Afisa Mkurugenzi wa mamlaka ya mapato ZRA Pemba Jamal Hassan Jamal, amewataka watendaji wa skuli hiyo kujisajili na kulipa kodi ili kuondosha changamoto zisizokuwa za lazima.
Anaeleza kuwa Serikali haina nia ya kumkwaza mtu bali ipo kusaidia wananchi wake, hivyo kuwataka kujisajili mamlaka kwa mujibu wa kipato chao.
“Ipo sheria namba 7 ya mwaka 2009 inasema yoyote anayeanzisha biashara kwa ajili yakujipatia kipato, lazima kuomba usajili mamlaka ya mapato Zanzibar.
Aidha kuwataka kufuata sheria kuomba usajili ZRA, ili kuepusha kwa ujenzi wa taifa.
MWISHO.