Thursday, January 9

TAMWA-ZNZ Yazindua Sera ya Kijinsia

 

 

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa, ametoa wito kwa wadau wote wa masuala ya maendeleo ya jinsia kutumia muongozo wa sera ya jinsia ulioandaliwa kwa ajili ya vyombo vya habari ikiwemo vyuo vikuu, taasisi za serikali na binafsi ili kuweza kufikia usawa wa kijinsia.

Dkt. Mzuri ametoa wito huo wakati wa uzinduzi rasmi wa muongozo wa sera ya jinsia uliofanyika huko katika ofisi za TAMWA ZNZ, Tunguu Mkoa Kusini Unguja.

Dkt. Mzuri aliongeza kuwa sera ya kijinsia itatambua kanuni mbalimbali zitakazoundwa na chombo cha habari ambazo kitaipa mamlaka dawati la jinsia ya kusikiliza na kupokea taarifa mbalimbali za unyanyasaji wa kingono au viashiria vitakavokuweko sehemu za kazi ili kuweza kuchukua hatua za kinidhamu.

“Ni lazima tukubali kwamba kazi bila ya unyanyasaji wa kijinsia inawezekana, hivyo ni lazima kuweko kwa fursa sawa ambazo zitaepuka ukatili wa kijinsia”.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar ndugu Suleiman Abdallah amesema ni muhimu kwa vyombo vya habari kufuata na kutumia muongozo huo wa sera ya jinsia ili kuweza kuweka usawa wa kijinsia katika maeneo ya kazi lakini pia kuondosha changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake.

Naye, Mwenyekiti wa Mtandao wa Kijinsia (ZGC) Bi.Asha Aboud ameipongeza TAMWA-ZNZ kwa kutayarisha na kuzindua muongozo wa sera ya kijinsia na kuwataka wakuu wa vyuo vikuu hapa nchini kuwa na sera hiyo pamoja na dawati la kijinsia ili kuweza kuepuka rushwa ya ngono ambayo moja ya athari zake ni kutoa wasomi ambao hawana sifa.

Sera ya kijinsia imezinduliwa kufuatia utekelezaji wa maradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL) ambao unatekelezwa na TAMWA ZNZ, ZAFELA na PEGAO kwa ushirikiano mkubwa wa balozi wa Norway.

  • Mwisho –