MIKAKATI, maelekezo na mipango madhubuti inahitajika kuwekwa ili kusaidia kuona sekta ya utalii inazidi kukuwa na kuingiza Pato zaidi.
Sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta mama ambayo imekuwa ikiingiza na kuipatia fedha nyingi katika Nchi.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud wakati wa akifungua mkutano wa Kamati za ulinzi na usalama za mikoa miwili ya Pemba na kupokea maoni ya kanuni ya makaazi ya watalii ulioandaliwa na Kamisheni ya utalii huko katika Ukumbi wa Kiwanda Cha Makonyo Wawi Chake Chake Pemba.
MKUU huyo wa Wilaya alieleza kuwa anafahamu sana juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali kupitia Kamisheni ya Utalii ili kuhakikisha kwamba malengo yake yanafikiwa ipasavyo.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya alifahamisha kuwa hivi Sasa tayari Kamisheni imeanzisha Polisi Utalii lengo lake ni kuona wale watalii wanapoingia nchini wanakuwa katika Hali ya usalama wakati wote.
“Tumekuwa na ushawishi mkubwa wa kuwatafuta wawekezaji mbali mbali ili wawekeze katika sekta hii ya utalii,” alieleza Rashid.
“Leo tupo hapa Ili kuweza kuchangia hii kanuni ya Makaazi ya watalii, kwani hivi Sasa kumekuwa na nyumba nyingi ambazo zinatumika katika kutoa huduma Kwa watalii wakati hazitambuliki Kisheria, hivyo kuwepo Kwa kanuni hii itasaidia sana kuondosha changamoto zilizopo,” alifahamisha Mkuu huyo wa Wilaya.
” Niwaombe sana washiriki wenzangu tuweze kutoa maoni yetu katika kanuni hii ili watalii wetu watakapokuja kwetu waweze kuwa na mpangilio mzuri wa makaazi yao na Wala sio kukaa sehemu ambazo haziko salama kwao lakini pia hata kukosa Pato la taifa,” alisema Rashid.
Mapema Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zuhura Mgeni Othman alizitaka Kamati hizo Kisiwani Pemba kushirikiana pamoja katika kuhakikisha kuwa wanapambana na kanuni ambazo haziko na Faida yeyote Kwa wageni pamoja na taifa Kwa ujumla.
Aidha Zuhura alieleza kuwa kinachotakiwa ni kuona watalii wanapoingia ndani ya Nchi wanapaswa kukaa katika maeneo yaliyo salama na yanayotambulika Kisheria na Wala sio vyenginevyo.
“Hivi Sasa kumekuwa na nyumba nyingi ambazo zinatoa huduma Kwa watalii lakini hazitambuliwi (hoteli bubu) hivyo Wizara ya Utalii kupitia Kamisheni ya Utalii tunalaani sana na hatuko pamoja nazo na tunazipiga vita, tutazufanyia kazi kupitia kanuni hii,’ alifahamisha Ofisa huyo.
Nao wajumbe wa Kamati za ulinzi na usalama za mikoa miwili ya Pemba waliuhakikishia uongozi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kushirikiana nao pamoja katika kusimamia kanuni hiyo.
Aidha wajumbe hao waliomba uongozi wa Kamisheni ya Utalii kutafanyia kazi mapendekezo yote ambayo wameyatoa katika kikao hicho.