RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, kuanzishwa bima inayofuata misingi ya Kiislamu (TAKAFUL) kwa Zanzibar, ni fursa adhimu kwa nchi kujitangaza kama eneo bora la uwekezaji kwa mwambao wa Afrika Mashariki.
Alisema, Zanzibar imeweka misingi imara katika kuhakikisha inatoa fursa kwa makampuni mbalimbali na watu binafsi kupata huduma mpya ya Takaful.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi alikozindua huduma ya bima inayofuata misingi ya Kiislamu itakayotolewa na Kampuni Tanzu ya Shirika la Bima la Zanzibar, ijulikanayo kama “ZIC TAKAFUL”.
Alisema, huduma ya Takaful tayari inatumiwa na nchi mbali mbali za bara la Afrika, Ulaya na bara la Asia katika kutoa fursa kwa biashara mbalimbali zinazofuata misingi ya Kiislamu kwa kupata huduma za bima zenye miongozo ya Uislamu.
Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuja kuwekeza Zanzibar kwenye huduma za bima za Kiislamu kupitia Re- Takaful.
“Natumia hadhara hii kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi yetu kuchangamkia fursa hii kwa kuja kuwekeza katika huduma za bima za aina hii kupitia Re- Takaful ili kuongeza uwezo wa kukatia bima miradi mikubwa itakayochochea ukuaji wa uchumi wetu”. Alishauri Dk. Mwinyi.
Alisema, kupitia mfumo wa uwekezaji utakaofanywa kwa fedha zitokanazo na ada za bima, utafuata miongozo sahihi iliyowekwa ili kuhakikisha fedha hizo haziwekezwi katika mambo yanayokwenda kinyume na misingi ya Kiislamu.
“Ni dhahiri kwamba, uanzishwaji wa huduma hii mpya ni hatua nyengine muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi ili kuchochea maendeleo ya shirika la Bima la Zanzibar” Alieleza Rais Dk. Mwinyi.
Aidha, alieleza huduma za Takaful ni kiungo muhimu cha ukuaji wa huduma za fedha zinazofuata misingi ya Kiislamu nakuongeza kuwa huduma hiyo hutoa fursa kwa Mabenki yanayoendeshwa kwa misingi hiyo, kutoa huduma za bima jambo ambalo halikuwezekana kabla ya uanzishwaji wa Takaful.
Alisema, Zanzibar ina kazi kubwa ya kufanya ili kuongeza kasi ya kufikisha huduma za bima kwa wananchi waliopo maeneo ya mbali mijini na vijijini kwa huwafikishia elimu sambamba na kubuni njia mbali mbali za kuwafikia wananchi wanaohitaji huduma hiyo kwa maendeleo ya kiuchumi nchini.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Ali Suleiman Ameir alisema, huduma ina manufaa makubwa kwa nchi na serikali kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na tozo kutokana na shughuli za bima nchini.
Alieleza huduma hiyo pia itawasaidia wananchi kujikinga na hatari zinazoweza kutokea kama majanga ya asili, magonjwa na ajali kwa kuzingatia misingi ya dini pamoja na kulinda mali zao, kuendeleza biashara zao kwa uhakika na kusaidia kujiwekea hakiba kwa mda mrefu.
Naye, Mkurugenzi Mwezeshaji wa Shirika la Bima Zanzibar, Afarat Ali Haji alieleza lengo la kuanzishwa kwa huduma za Takaful Zanzibar ni kuwapa uhuru wananchi kuchagua huduma bora na kupata suluhisho la kukata bima isiyo na riba sambamba na kukuza uchumi na maendeleo ya jamii na kuwajengea taswira njema kwa taifa.
Aidha, alieleza nia ya Shirika la Bima kuanzisha huduma ya bima ya Takaful mbali nia ya kukuza na kuongza mitaji pia kuongeza jitihada za kuanzisha bima ya maisha hapo baadae baada ya kuimarika kwa huduma za TAKAFUL nchini, hivyo, aliiomba Serikali kuwaongezea mtaji wa kufanikisha huduma hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dk. Baghayo Abdalla Saqware alisema sekta ya bima imepunguza umasikini nchini kwa kuisaidia jamii kukuza biashara zao na kuongeza kampuni nyingi za bima nchini.
Kampuni Tanzu ya Shirika la Bima Zanzibar (ZIC TAKAFUL) ni kampuni inayotoa huduma za bima kwa kufuata misingi ya Sheria za Kiislamu, Zanzibar.
IDARA YA MAWASILINO IKULU, ZANZIBAR